Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-03-31 16:44:17    
Mahakama kuu ya Libya yasikiliza kesi ya wageni wa nchi za nje kusambaza kwa makusudi virusi vya ukimwi

cri

Mahakama kuu ya Libya tarehe 29 mwezi huu ilisikiliza rasmi rufani iliyokatwa na washitakiwa ambao ni wauguzi watano wa Bulgaria na daktari mmoja wa Palestina ambao wanatuhumiwa kwa kesi ya kusambaza kwa makusudi virusi vya ukimwi, na kuamua kutoa hukumu ya mwisho tarehe 31 Mei.

Hakimu wa mahakama kuu ya Libya Bwana Ali Aruth alitangaza uamuzi huo kabla ya kumalizika kusikiliza kesi. Mabalozi wa Bulgaria na nchi kadhaa za Umoja wa Ulaya walioko nchini Libya, jamaa wa walioambukizwa na mawakili wa washitaki na washitakiwa walihudhuria usikilizaji wa kesi hiyo. Wakazi wa Libya wanaowaunga mkono walioambukizwa virusi vya ukimwi walifanya maandamano nje ya mahakama, wakiunga mkono adhabu ya kifo iliyotolewa na mahakama dhidi ya washitakiwa katika hukumu ya kwanza. Polisi wa Libya walichukua hatua kali za usalama ndani na nje ya mahakama.

Wakili wa utetezi Bw. Osman Bizante alisema kuwa, hana wasi wasi kuhusu matokeo ya hukumu hiyo, akitumai kuwa mahakama itatoa hukumu kutokana na sheria, na haitaathiriwa na mambo ya kisiasa.

Kesi hiyo ilianza kusikilizwa mwaka 1998, idara ya uendeshaji wa mashitaka ya Libya iliwashitaki wauguzi watano kutoka Bulgaria na daktari mmoja kutoka Palestina waliofanya kazi katika hospitali moja ya nchi hiyo kuwawekea virusi vya ukimwi watoto 426 na wanawake 19 kwa lengo la kufanya majaribio, matokeo yake yalisababisha vifo vya watoto 48. washitakiwa 6 wote walikana mashitaka, lakini mahakama ya Libya mwezi Mei mwaka jana iliwakuhumu adhabu ya vifo kwa kueneza kwa makusudi virusi vya ukimwi.

Kesi hiyo ilifuatiliwa sana na nchi za magharibi hasa nchi za Umoja wa Ulaya, Umoja wa Ulaya kwa mara nyingi uliitaka Libya kuondoa hukumu ya vifo, na kuwaachia huru haraka iwezekanavyo wauguzi watano wa Bulgaria, lakini Libya inashikilia kuhukumu kesi hiyo kwa mujibu wa sheria zake.

Mahakama kuu ya Libya iliamua kushughulikia ombi la rufani ya washitakiwa baada ya kukabidhiwa ushahidi na madaktari watatu kutoka Ufaransa, Italia na Uswizi. Madaktari hao watatu waliona kuwa, sababu ya tukio hilo ni kutokana na hali duni ya matibabu ya hospitali ya Libya.

Libya iliwahi kuiomba Bulgaria iisaidie kujenga hospitali ya kisasa ya ugonjwa wa ukimwi, na kuwafidia jamaa za walioambukizwa ili kufikia makubaliano na jamaa za walioambukizwa nje ya mahakama. Lakini Bulgaria ilikataa pendekezo hilo, ikiwa na wasiwasi kuwa, kufanya hivyo ni sawa kukubali kuwa, wauguzi watano wa Bulgaria kweli wana makosa.

Idhaa ya kiswahili 2005-03-31