Mjumbe wa kamati ya siasa ya chama cha kikomunisti cha China ambaye ni naibu waziri mkuu wa serikali Bw Zeng Peiyan tarehe 4 huko mji wa Chongqing alishiriki kwenye mkutano wa kuhifadhi Mto mama na sherehe ya uzinduzi wa upandaji miti pembezoni mwa bwawa la maji la Magenge Matatu, aliwahamasisha vijana washiriki kwenye harakati ya kuhifadhi Mto mama pamoja na shughuli za kuhifadhi mazingira ya asili.
Harakati ya kuhifadhi Mto mama ni harakati inayonufaisha umma ambayo ilianzishwa mwaka 1999 na wizara na idara nane kwa pamoja ikiwemo kamati kuu ya chama cha vijana cha kikomunisti. Hadi hivi sasa vijana zaidi ya milioni 300 wameshiriki kwenye shughuli hizo na kujenga misitu 1103 yenye hekta 266,000, ambayo imeboresha sana mazingira ya asili kwenye maeneo ya mitiririko ya mito mikubwa.
Toka mwaka 1989 wizara ya maji imechukuliwa udhibiti wa mmomonyoko wa ardhi kwenye eneo la bwawa la Magenge Matatu kuwa kazi muhimu katika shughuli za kuhifadhi maji na ardhi nchini China. Hadi kufikia mwishoni mwa mwaka jana mmomonyoko wa ardhi kwenye eneo la kilomita za mraba elfu 17.7 umedhibitiwa ipasavyo na kuanzisha mashamba yenye hekta 138,666, ambapo udongo na mchanga ulioingia kwenye eneo la bwawa la Magenge Matatu ulipungua kwa kiasi cha 60%.
Bw. Zeng Peiyan alisema kuwa nchi ikitaka kustawi inahitaji wataalamu wengi; jamii ikitaka kuwa na maendeleo endelevu inahitaji misitu mingi. Vijana wako katika kipindi cha kujenga msingi wa maisha na itikadi yake, hivyo harakati ya kuhifadhi Mto mama inaweza kuunganisha kuwaelimisha vijana na hifadhi ya mazingira ya asili. Katika miaka mingi iliyopita sehemu mbalimbali zilipoendeleza harakati hiyo zilizingatia kuifungamanisha harakati hiyo na hali halisi za huko, kufuatilia ufanisi, mambo ambayo si kama tu yameinua mwamko wa vijana kuhusu hifadhi ya mazingira, bali pia yametoa mchango mkubwa katika kuendeleza ujenzi wa mazingira ya viumbe. Lakini tunapaswa kufahamu kuwa mwelekeo wa jumla ya mazingira ya asili ya China kuwa mbaya haujapata kudhibitiwa, kwa hiyo tunapaswa kuhamasisha sekta mbalimbali za jamii kujitahidi kwa pamoja, kuimarisha hifadhi ya mazingira ya viumbe na kujenga China iwe nchi nzuri.
Bw. Zeng Peiyan alitoa matarajio manne kwa idara husika na vijana wa China. La kwanza, kuelimisha watu kuhusu harakati hiyo na kuendeleza ustaarabu wa mazingira ya viumbe. Tunatakiwa kuelimisha watu kuhusu utamaduni wa mazingira na kukuza moyo wa uadilifu wa kuhifadhi mazingira. Vijana wanatakiwa kupiga hatua kutoka mwanzo, kutoka kila familia, shule na idara ya kazi yake, kufanya kutoka shughuli ndogo anayoweza, kuathiri na kushirikisha watu wengi zaidi katika hifadhi na ujenzi wa mazingira ya viumbe. La pili, kuendeleza harakati ya mazingira ya viumbe kwa kufuatana na umaalum wa vijana. Tunatakiwa kuwahamasisha vijana kushiriki kwenye ujenzi wa miradi muhimu ya mazingira ya viumbe, kuhamasisha vijana kuwa karibu mazingira ya kimaumbile na kufuatilia hali ya mazingira, kuhifadhi maskani yao na kuboresha mazingira ya taifa. La tatu, kuimarisha usimamizi wa mpango na kuweka kipaumbele katika ujenzi wa miradi ya mazingira ya viumbe. Ujenzi wa miradi hiyo unatakiwa kuendana na kanuni za kimaumbile, kuweka mpango wa kisayansi, kuwa na majadiliano ya kutosha kabla ya kufanya ujenzi. Tunatakiwa kuunganisha harakati ya kuhifadhi Mto mama na shughuli za kuboresha mazingira ya eneo la bwawa la Magenge Matatu na kuonesha mfano wa kuigwa kwa sehemu nyingine. Nne, kuhamasisha sekta mbalimbali za jamii kuunga mkono shughuli za kuhifadhi na kuboresha mazingira ya viumbe. Katiba za chama cha kikomunisti cha China na serikali katika ngazi mbalimbali zinatakiwa kufuatilia na kuunga mkono shughuli za kuhifadhi Mto mama. Kamati za chama cha vijana cha kikomunisti cha China katika ngazi mbalimbali zinatakiwa kushirikiana na idara husika, kuhamasisha sekta mbalimbali za jamii na kuhimiza maendeleo ya harakati ya kuhifadhi Mto mama.
Baada ya mkutano huo kumalizika, Bw. Zeng Peiyan alifika katika kijiji cha Jianming wilayani Yunyang na kushiriki kwenye mkutano wa "Kuboresha mazingira ya bwawa la Magenge Matatu na kuhifadhi Mto mama" pamoja na sherehe ya uzinduzi wa harakati ya upandaji miti kwenye eneo bwawa la Magenge Matatu.
Idhaa ya Kiswahili 2005-04--05
|