Hivi sasa, China inatekeleza sera ya elimu ya lazima ya miaka 9 kuanzia shule ya msingi hadi shule ya sekondari. Ingawa wanafunzi hawatakiwa kulipa gharama za masomo, lakini bado wanatakiwa kulipa yuan mia kadhaa hadi elfu moja kila mwaka kwa ajili ya vitabu vya kiada, mabweni ya shule na huduma nyingine. Gharama hizo ni rahisi kwa familia za mijini, lakini ni mzigo mkubwa kwa familia maskini za vijijini, na baadhi ya wanafunzi wamelazimika kuacha masomo yao kutokana na hali hiyo.
Kuhusu hali hiyo, katika miaka minne iliyopita,China ilianza kutekeleza hatua kwa hatua sera ya kusamehe gharama hizo kwa wanafunzi maskini vijijini.
Wilaya ya Yijinhuoluo katika mkoa unaojiendesha wa Mongolia ya ndani ni sehemu iliyoko nyuma kiuchumi. Mkulima wa huko Li Feirong aliwahi kuishi maisha mazuri kwa kufuga sungura, lakini ugonjwa wa Sungura ulilipuka ghafla mwaka jana na kuwaua sungura wake wote na kuleta hasara kubwa kwa familia yake. Kutokana na hali hiyo, alishindwa kulipa gharama za shule kwa ajili ya watoto wake wawili. Wakati huohuo, sera ya kusamehe gharama za shule kwa watoto maskini ilianza kutekelezwa huko. Bw. Li Feiring alimwambia mwandishi wetu wa habari kwa furaha:
"Kwa ujumla, gharama za shule kwa ajili ya binti yangu mkubwa ni yuan mia nane hadi mia tisa kila mwaka, na mtoto mdogo bado anasoma katika shule ya msingi, gharama zake ni yuan 170 kwa mwaka, ninashindwa kumudu gharama hizo. Hivi sasa sera hiyo mpya imeondoa wasiwasi wangu mkubwa."
Sera hiyo inaagiza kuwa serikali kuu, serikali ya mkoa na serikali za wilaya za China zinalipa gharama hizo za shule kwa pamoja, na watoto wa familia za vijijini zenye mapato chini ya kiwango cha wastani cha huko wananufaika na sera hiyo.
Lakini kwa mujibu wa maagizo husika, wakati wa kutekeleza sera hiyo, idara za serikali za mitaa za sehemu mbalimbali zinapaswa kufanya kazi nyingi, zikiwemo kupata idadi ya familia zinazostahili kupewa misaada kwa kupima mapato ya wastani ya huko, kuzihamasisha familia hizo zitoe maombi ya misaada, idara husika kuchunguza na kutangaza orodha ya familia zilizotoa maombi ya misaada na hatimaye kuamua familia zipi zipewe misaada.
Kwa kuwa wilaya ya Yijinhuoluo iko nyuma kiuchumi, mapato ya wakulima na wafugaji wa huko ni ya chini, hivyo serikali ya huko imeamua kutekeleza sera hiyo kwa watoto wa familia zote. Mkuu wa wilaya hiyo Bw. Liu Wenshan aliainisha kuwa, ili kuendeleza uchumi, kwanza inapaswa kuendeleza elimu. Alisema:
"kwa mujibu wa sera ya taifa, ili kutekeleza sera hiyo, tunapaswa kutoa fedha yuan laki moja, lakini tulitoa yuan laki 1.6, ingawa hali ya fedha ya wilaya hiyo si nzuri sana. "
Hivi sasa, wanafunzi wote zaidi ya elfu 16 wa shule za msingi na sekondari katika wilaya hiyo wanapewa misaada ya fedha kutokana na sera hiyo.
Kuhusu hali ya utekelezaji wa sera hiyo kwenye mkoa unaojiendesha wa Mongolia ya ndani, naibu mwenyekiti wa mkoa huo Bw. Lian Ji alieleza,
"mkoa wetu una wilaya 101, na wilaya 81 kati ya hizo zinatekeleza sera hiyo. Uchumi na jamii ya mkoa wa Mongolia ya ndani vimeendelea kwa haraka katika miaka ya hivi karibuni, lakini tunakosa wataalamu wa kutosha, hivyo tunapaswa kuweka mkazo kwenye elimu ya watoto, na hilo pia ni lengo letu muhimu la kimkakati katika kutekeleza sera hiyo."
Takwimu husika zinaonesha kuwa, hivi sasa, wengi wa wanafunzi maskini milioni 30 kote nchini China wanapata vitabu vya kiada bure, na karibu nusu kati yao wamesamehewa gharama nyingine za shule.
Waziri wa elimu wa China Bw. Zhou Ji alisema kuwa, utekelezaji wa sera hiyo umewapatia watoto wa familia maskini haki ya elimu kama ilivyo kwa watoto wengine wa kawaida, na pia utaandaa watu wengi zaidi wenye umaalum kwa ajili ya maendeleo endelevu ya China. alisema:
"tunatekeleza sera hiyo hatua kwa hatua kwa wanafunzi maskini milioni 30 wa shule za msingi na sekondari kote nchini China. kwa kila mtoto aliyepewa misaada, atakuwa na fursa ya kupata elimu; na familia zao, zitakuwa na matumaini; na vijiji vyote, vitaweza kuinua kiwango cha elimu ya wakulima, na hatimaye kiwango cha elimu ya wananchi wote. Hivyo, utekelezaji wa sera hiyo ni muhimu sana."
habari zinasema kuwa, kuanzia mwaka huu hadi mwaka 2007, serikali kuu ya China itatenga fedha yuani zaidi ya bilioni 22 katika utekelezaji wa sera hiyo.
Idhaa ya Kiswahili 2005-04-13
|