Mjumbe wa ofisi ya kisiasa ya kamati kuu ya chama cha kikomunisiti cha China, ambaye pia ni naibu waziri mkuu wa China, na mkuu wa kikundi cha uongozi cha ujenzi wa Reli ya Qinghai-Tibet Bw. Zeng Peiyan tarehe 12 mwezi huu alipohudhuria mkutano wa kazi kuhusu ujenzi wa reli hiyo alisisitiza kuwa, mwaka huu ni mwaka muhimu wa ujenzi wa reli ya Qinghai-Tibet, idara husika za ujenzi huo zinatakiwa kuendelea na juhudi zao ili kuhakikisha ubora na ufanisi wa ujenzi na kujitahidi kukamilisha mradi huo mkubwa kabla ya tarehe mosi Julai mwaka kesho.
Bw. Zeng Peiyan alikutana na maofisa na wafanyakazi waliopewa tuzo na serikali ya China kutokana na kazi bora katika ujenzi wa reli hiyo na kuwapa salama za pongezi na pole za kazi. Alisema kuwa, tangu ujenzi wa mradi huo ishwe, makada na wafanyakazi walio wengi wa reli wameshinda matatizo ya aina mbalimbali, na kupata mafanikio makubwa yaliyotambuliwa duniani. Aliwataka waendelee kuchapa kazi ili kukamilisha kwa ufanisi kazi mbalimbali za ujenzi wa reli kwenye uwanda wa juu ya kiwango cha juu duniani.
Bw. Zeng Peiyan alitoa maoni manne kuhusu ujenzi wa reli hiyo ya Qinghai-Tibet.
Kwanza, ni lazima kufuatilia ubora wa mradi, na kujitahidi kuijenga Reli ya Qinghai-Tibet kuwa mradi wa mfano wa kuigwa. Hivyo idara husika za ujenzi zinatakiwa kutilia maanani usimamizi na ukaguzi wa mradi huo.
Pili, kuhifadhi mazingira ya viumbe ya uwanda wa juu. Kuchukua hatua za aina mbali mbali katika kuhifadhi mazingira ya viumbe yenye umaalum wa uwanda wa juu kandokando ya reli hiyo, kuimarisha mafanikio yaliyopatikana katika hifadhi ya mazingira, na kutafiti kuhusu jinsi ya kuhifadhi mazingira baada ya reli hiyo kuanza kufanya kazi.
Tatu, kufuatilia usalama wa maisha na afya ya kila mjenzi wa reli hiyo. Kuboresha siku hadi siku hali ya maisha ya wajenzi walio wengi wa reli hiyo, na kutekeleza hatua mbalimbali za usalama wakati wa utendaji kazi. Kuboresha huduma za afya, kukinga na kutibu maognjwa ya uwanda wa juu, na kulinda haki na maslahi halali ya wakulima vibarua.
Nne, kufanya maandalizi ya uendeshaji wa reli hiyo, na kuhakikisha ufanisi wa mseto wa Reli ya Qinghai-Tibet. Idara husika za reli zinatakiwa kufanya uchunguzi kwa kina, kutunga miswada kuhusu usimamizi, uratibu na uongozi wa matumizi ya reli hiyo, pamoja na kutengeneza zana za reli. Sehemu zilizoko pembezoni zinatakiwa kutafiti kuhusu jinsi ya kuendeleza shughuli zenye ubora maalum wa huko na kukuza soko la utalii ili kuhimiza reli hiyo iwe na ufanisi mzuri zaidi wa kiuchumi na kijamii.
Hivi sasa, ujenzi wa reli ya Qinghai-Tibet unaendelea vizuri. Miradi muhimu ya kuweka msingi wa reli, madaraja na mahandaki kimsingi imekamilika, na miradi mingine kama vile ujenzi wa vituo vya reli na mawasiliano ya simu inaendelea bila matatizo.
Idhaa ya kiswahili 2005-04-15
|