Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-04-20 21:20:01    
China na Tanzania zaimarisha ushirikiano katika sekta za elimu na utamaduni

cri

Hivi karibuni waziri wa elimu na utamaduni wa Tanzania Bwana Joseph Mungai amefanya ziara nchini China, yafuatayo ni mahojiano kati ya mwandishi wetu wa habari na Bwana Mungai.

Kwanza mheshimiwa waziri ningependa kujua madhumuni hasa ya ziara yako pamoja na ujumbe wako hapa China.

Tupo hapa katika utaratibu ambao tumejiwekea na wenzetu wa Uchina, utaratibu wa ushirikiano katika nyanja ya utamaduni. Kwa hivyo tunatembelea na kuona maendeleo yao na kujifunza kutoka kwao, na wao huwa wanakuja kwetu, na huwa tunabadilishana pia vikundi vya utamaduni ambavyo vinakuja kufanya maonyesho hapa. Kwa hiyo alipokuja nchini Tanzania waziri anayesimamia masuala ya elimu na utamaduni madam Chen Zhili, alinialika nitembelee hapa, niwe mgeni wa wizara ya utamaduni ya hapa. Nione mambo yao ya utamaduni, lakini pia nipate fursa ya kuona maendeleo ya China ya leo, mimi niliwahi kutembelea nchi hiyo mwaka 1970, kwa hiyo leo nakuja kuona pia China mpya baada ya miaka 34. Kwa hiyo pamoja na mambo ya utamaduni ambayo tuna mkataba rasmi wa ushirikiano, nikiwa hapa nitaona pia maendeleo ya Uchina, na kukua kwa uchumi wa China, kwa karibu asilimia 12 ambayo hiyo ni kasi kubwa sana ya kukua kwa uchumi. Tunapata fursa ya kujifunza mambo hayo pamoja na maendeleo ya elimu.

Umezungumzia uhusiano katika sekta ya utamaduni, lakini hujazungumzia kwa undani sekta ya elimu, uhusiano kati ya China na Tanzania katika sekta ya elimu, hasa elimu ya msingi na elimu ya sekondari ukoje kwa sasa hivi?

Hatuna ushirikiano wa moja kwa moja katika ngazi ya elimu ya msingi na sekondari, lakini alipokuja waziri wa nchi (Chen Zhili) kututembelea Tanzania, alitoa misaada ya kompyuta kwenye shule zetu za msingi na shule ya sekondari ya Benjamin William Mkapa, kwa hiyo, ushirikiano katika ngazi hiyo ni wao wanatupatia misaada ya kusaidia shule hizo mbili, na alipokuwa kule pia aliahidi kuwa angetoa msaada wa piano na ninafurahi kusema kuwa piano hizo zimekwishafika. Kwa hiyo ushirikiano wetu katika elimu ni mkubwa zaidi katika elimu ya juu, ambapo kila mwaka, serikali ya Uchina inatupa sholarship kiasi cha 40, wanafunzi kutoka Tanzania wanakuja kupata mafunzo ya elimu ya juu hapa.

Hivi karibuni ulikuwa mwenyekiti wa mkutano mmoja ambao unataka kuinua kiwango cha elimu ya kompyuta kwa walimu wa shule za msingi, je kuna uwezekano wowote wa kuwa na uhusiano na China katika eneo hilo?

Uwezekano upo mkubwa, na tumeamua kwamba tunataka kuwa na elimu ya kompyuta katika shule zetu, lakini tumeamua tuanze na kuwafundisha walimu, kwa hiyo tuna mpango wa kuanzisha mafunzo ya kompyuta kwenye vyuo vyetu vya ualimu. Baada ya hapo ndipo yatafuatiwa na mafunzo sasa katika shule. Tumeamua tuanze na kile kitu ambacho ni muhimu kuanzia, huwezi kuanza kufundisha kompyuta kama huna walimu. Nina hakika kwa kadiri walimu watakavyokuwa wanatoka vyuoni ndivyo uwezo wa kufundisha utakavyoongezeka. Tutakuwa na mahitaji makubwa sana, ambapo rafiki zetu wote pamoja na Uchina tutawashirikisha, litakuwa ni suala la kuwa na kompyuta za kutosha kuweza kufundisha katika shule zetu za sekondari na pia shule za msingi.

Kitu kingine, mheshimiwa waziri, ni kwamba kwa muda ambao mimi nimekaa hapa China kwa mwaka mmoja na miezi saba, nimeona kuwa idadi kubwa sana ya wanafunzi kutoka nchi za kigeni hata nchi za dunia ya kwanza wanakuja hapa China kujifunza lugha ya Kichina, wao wanalenga kwamba katika miaka labda nusu karne ijayo, huenda Kichina ikawa ni lugha moja muhimu duniani, sasa sijui sisi Tanzania kuna mpango wowote wa kuifanya lugha ya Kichina ifundishwe Tanzania katika ngazi yoyote?

Kwa sasa hivi hatujawa na mpango wa kuanzisha kufundisha lugha ya Kichina, lakini ninahakika muda utafika, kwa sababu Wachina ni watu wengi sana duniani, nchi hiyo ni kubwa, wingi wao zaidi ya bilioni 1, kadiri lugha yao itakavyotumika kimataifa itakuwa vizuri na watu wetu wataweza kujifunza. Kwa hiyo sasa hivi naweza kusema kwamba katika shule zetu, hasa ninazosimamia mimi kwa maana ya shule za msingi na shule za sekondari, lugha ya Kichina hatuifundishi, lakini tunayo fursa ya kuleta Watanzania wanaotaka kujifunza Kichina kuweza kuja kujifunza hapa China. Sina hakika kama katika ngazi ya chuo kikuu lugha ya Kichina inafundishwa.

Na kuna ule mpango wa maendeleo ya elimu ya msingi, ule mpango nakumbuka ulikuwa unahusisha hata ujenzi wa madarasa. Hawa wenzetu wana uwezo mkubwa katika ujenzi na kiwango chao naweza kusema kinakubalika na gharama za chini, sijui labda umewahi kufikiria kuna uwezekano wa kuwashirikisha watu hao siku moja kusaidia kujenga shule?

Kusema kweli, katika mpango wa elimu ya msingi MMEM 2002 mpaka 2006 ambao nadhani ndio unaozungumzia mpango huo sasa umeingia mwaka wa nne, kwa hiyo uko katika hatua ya ngazi ya juu ya utekelezaji, na mpango ule umepewa msaada, msaada mkubwa sasa kuliko yote unaotoka benki ya dunia. Sasa unaweza ukasema kwa vile Uchina ni miongoni mwa wenye benki katika benki ya dunia, kama vile Tanzania ilivyo, kwa hiyo unaweza ukasema kwamba wanatusaidia kwa njia hiyo, kwa hiyo hakuna mpango maalum kwamba katika utekelezaji wa MMEM, tunawalenga Wachina watusaidie kwa sababu tayari wametusaidia kwenye mpango wetu.

Idhaa ya Kiswahili 2005-04-20