Kuanzia tarehe mosi hadi 7 mwezi Mei, maonesho makubwa yaitwayo "Ifahamu Afrika" (touch Africa) yalifanyika katika Bustani ya Dunia iliyoko kusini magharibi mwa mji wa Beijing. Meneja wa Bustani ya Dunia anayeshughulikia maonesho hayo Bwana Liu Zhen Bin alimfahamisha mwandishi wetu wa habari akisema:
"Lengo la maonesho ya 'Ifahamu Afrika' ni kuwafahamisha wachina kuhusu mila na desturi, utamaduni, vyakula, sanaa na utalii wa nchi za Afrika. Nchi sita za Kenya, Tanzania, Misri, Ethiopia, Zimbabwe na Afrika ya Kusini zilianzisha vibanda vya kuonesha picha na maelezo kuhusu vivutio vyao vya utalii."
Bw. Liu alieleza kuwa, licha ya vibanda vya kuonesha mambo ya utalii, nchi nyingi za Afrika pia ziliweka vibanda vya kuuzia vitu vya sanaa kama vile vinyago, vitambaa, picha za nyasi na vitu vya mapambo. Ethiopia licha ya kuuza vitu vya sanaa, pia iliwaoneshea wachina utamaduni wa kahawa, kuanzia namna ya kukaanga buni hadi namna ya kupika kahawa, na kuwauzia watalii kwa bei rahisi.
Licha ya hayo, Bustani ya Dunia pia ilivialika vikundi viwili vya wacheza dansi na waimbaji kutoka Misri na Liberia kufanya maonesho kila asubuhi na alasiri, maonesho hayo yamewavutia sana watalii.
Bw. Liu alisema kuwa, licha ya hayo, makampuni ya usafiri wa ndege ya Qatar, Kenya, Zimbabwe na Ethiopia yalishiriki kwenye maonyesho hayo kwa kuchangia tikiti 9 za ndege. Kila alasiri mtalii mmoja au wawili walichaguliwa kupata tikiti ya ndege ya kwenda na kurudi kutoka Beijing hadi Cairo, Nairobi, Addis Ababa na Johannesbourg. Watalii wote walioitembelea Bustani ya Dunia ya Beijing waliweza kushiriki kwenye shughuli hiyo. Siku ya kwanza watalii wawili kutoka mikoa ya Shangdong na Henan walibahatika kupata tikiti za kwenda Misri, Bwana Wen Haiquan kutoka shirika la mafuta ya Petroli la mkoa wa Shangdong ni mmojawao, anasema:
"Nafurahi sana. Najua Misri ina piramidi na sanamu yenye sura ya binadamu na mwili wa simba ( Sphinx). Nimepata tikiti ya ndege ya kwenda Misri kwa bahati nzuri, hivyo nitajaribu kupanga wakati wa kwenda kuitembelea Misri pamoja na mchumba wangu."
Misri ni nchi yenye historia ndefu ya ustaarabu, pia ni nchi yenye miujiza mingi. Kwenye Bustani ya Dunia ya Beijing yalijengwa majengo mengi ya kihistoria ya nchi hiyo kama vile piramidi, sphinix, nguzo na kadhalika. Balozi wa Misri nchini China Bw. Aly El-Hefny alipohojiwa na mwandishi wetu wa habari alisema:
"Tunafurahi sana kushiriki kwenye maonesho haya, leo ni tarehe mosi Mei, pia ni Jumapili, hivyo maonesho ya dansi na muziki wa Misri unawavutia watalii wengi. Nia yetu ni kuwavutia watalii wengi zaidi wa China kutembelea Misri. Licha ya Beijing, pia tumefanya maonesho ya vivutio vya utalii katika miji mingine nchini China. Nawakaribisha wachina wawili waliobahatika kupata tikiti za ndege watembelee Misri na nawatakia safari njema na mafanikio mema."
Bw. El-Hefny alisema kuwa, Misri imeanzisha ofisi yake ya utalii mjini Beijing ili kuwahudumia watalii wa China wenye hamu ya kwenda kutalii nchini Misri. Alisema kuwa, kampuni ya ndege ya ndege ya Misri ilianzisha safari za moja kwa moja kutoka Cairo hadi Beijing mwezi Januari mwaka 2003, lililazimika kusimamisha safari zake kutokana na kulipuka kwa maambukizi ya SARS nchini China, inatarajia kufufua safari za moja kwa moja mwezi Oktoba mwaka huu, ili kuwarahisishia watalii wa China kutembelea Misri na nchi nyingine karibuni.
Nchi ya Kenya pia ina vivutio vingi vya utalii ambavyo ni pamoja na mandhari nzuri ya kimaumbile na bustani za wanyama pori. Sekta ya utalii inachukua asilimia 12 ya pato la taifa la Kenya, hivyo serikali ya Kenya inazingatia sana kukuza utalii, imechukua hatua nyingi kuhimiza utalii kama vile kupitisha sheria ya kupiga marufuku uwindaji ili kuhifadhi wanyama pori, kuhakikisha usalama na kujenga miundombinu ya utalii. Mwaka jana Kenya ilifungua mlango kwa watalii wa China, ili kuwavutia wachina wengi kutembelea Kenya, Kenya imeweka ofisi ya utalii huko Hongkong, kampuni ya Kenya Airways itaanzisha safari za moja kwa moja kutoka Nairobi hadi Shanghai mwaka huu. Balozi wa Kenya nchini China Bi. Ruth Sereti Solitei anasema:
"Mwaka jana ujumbe mkubwa ulioundwa na mashirika ya utalii na mashirika ya ndege walikuja China kufanya maonesho makubwa huko Shanghai na Beijing. Na vituo vya televisheni vya CCTV na BTV vya China kwa nyakati tofauti vilituma timu za waandishi wa habari kwenda Kenya kutengeneza vipindi vya televisheni kuhusu utalii, utamaduni na mambo mengine kuhusu Kenya."
Idhaa ya kiswahili 2005-05-13
|