Tukizungumzia vivutio vya Mlima Wuyi, mwandishi wa vitabu wa China alimnukuu mzee mmoja mmrekani akisema, kama iko siku nitapotea njia katika sehemu yoyote duniani, tafadhali nipelekee huko Mlima Wuyi wa mkoa wa Fujian, China. Mlima huo anaoupenda mzee huyo wa Marekani unasifiwa kuwa ni mlima wenye mandhari nzuri na vivutio vya ajabu zaidi kuliko milima mingine ya sehemu ya kusini mashariki ya China. Mwishoni mwa karne iliyopita, mandhari nzuri ya mlima huo ilitambuliwa duniani, mlima huo uliorodheshwa na Kamati ya mali ya urithi ya UNESCO kuwa mali ya urithi ya maumbile.
Mlima Wuyi unazungukwa kwa vijito vingi, na vilele vingi vyenye maumbile ya kiajabu na miamba, inajitokeza kwenye kando mbili za vijito vyenye maji safi. Mkurugenzi wa idara ya utalii ya mji wa Wuyi Bwana Yu Zelin alisema:
Sehemu ya Mlima Wuyi inapendeza zaidi kwa milima na mito inayopatana vizuri. Popote pale unaweza kuangalia milima yenye mandhari nzuri, na mito yenye maji safi.
Katika sehemu ya Mlima Wuyi kuna vivutio vingi kama vile kilele cha Tianyou ambacho ni kirefu sana, watalii wakipanda juu ya kilele hicho wataona kuwa, kilele hicho kina maumbile ya kiasili inayowapendeza. Kilele hicho kwa kweli ni mwamba mkubwa mzima, urefu wake ni zaidi ya mita 500 na upana wake ni zaidi ya mita 1000. Kutokana na kulowa kwa mvua iliyonyesha katika miaka mingi iliyopita, kuna mistari mingi imebaki kwenye mwamba kama vipande vingi vya vitambaa, hivyo watu wanasema kuwa mwamba huo ni mwamba wa kuanikia vitambaa. Na katikati ya mwamba, kuna dalili kadhaa zinazoonekana kama viganja vya mikono ya watu, hivyo kilele hicho pia kimesifiwa kuwa ni kilele cha kiganja cha malaika. Mwongozaji wa utalii Dada Liu Gonglian alisema:
Inasemekana kuwa katika siku za zamani sana, malaika mmoja aliyeacha miguu wazi alipopita sehemu hiyo alivutiwa sana na mandhari nzuri ya Mlima Wuyi, akabeba vitambaa vyake akitembea huku na huko, mwishowe akakumbuka vitambaa vyake, lakini aliona vitambaa vyake vililowa kwa umande, hakuwa na la kufanya ila kuvianika vitambaa vyake kwenye mwamba, lakini jua kali la adhuhuri liliyeyusha vitambaa, malaika alihangaika sana, alitaka kuvichukua, vitambaa vikararuka na viganja vyake vikaacha alama kubwa kwenye mwamba.
Sehemu hiyo yenye mandhari nzuri inawavuta watalii wengi. Mtalii kutoka Taiwan Bwana Meng Linjun alisema:
Sehemu hiyo yenye mawe na miamba yenye maumbile ya ajabu ambayo haionekani katika sehemu nyingine, sehemu hiyo yenye milima na mito, kwa kweli inapendeza sana.
Katika sehemu hiyo pia kuna kijito chenye matawi mengi na msitu wa kiasili, msitu huo ni kama peponi kwa ndege na wanyama wa aina mbalimbali. Eneo la msitu wa kiasili wa sehemu hiyo ni zaidi ya hekta elfu 20, ambapo kuna hewa safi na mazingira mwafaka kwa binadamu.
Idhaa ya kiswahili 2005-05-16
|