Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-05-19 16:15:06    
China imekuwa nchi inayozalisha maua kwa wingi kabisa duniani

cri

Mkutano wa pili wa baraza la wakuu wa wilaya zinazozalisha maua kwa wingi nchini China, yaani mkutano wa pili wa wakuu wa kampuni za maua wa China tarehe 18 ulifanyika huko Wuhan, mji mkuu wa mkoa wa Hubei, katikati ya China. Mkuu wa Taasisi ya Sayansi ya Misitu ya China, ambaye pia ni mkuu wa Shirikisho la Maua la China Bi. Jiang Zehui alihudhuria mkutano huo na kutoa hotuba kwenye ufunguzi. Bi. Jiang alisema kuwa, baada ya kazi ya miaka zaidi ya 20, sasa China imekuwa nchi inayozalisha maua kwa wingi zaidi duniani, na imechukua nafasi muhimu katika uzalishaji na biashara ya maua duniani.

Bi. Jiang Zehui alisema kuwa, kutokana na maendeleo ya utandawazi wa uchumi duniani, na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia nchini China, katika miaka ya karibuni uzalishaji wa maua unazidi kuhamishwa kutoka nchi zilizoendelea zenye gharama kubwa za uzalishaji hadi kwenye nchi zinazoendelea zenye gharama ndogo, na nafasi ya China katika uzalishaji na biashara ya maua duniani imekuwa kubwa siku hadi siku. Hasa katika hali mpya ya kwamba, China imepata maendeleo makubwa ya kiuchumi na kijamii, katika mchakato wa kujenga jamii yenye maisha bora, sekta ya uzalishaji maua itakuwa na umuhimu usiobadilika katika kurekebisha na kuboresha sekta ya kilimo, kuongeza mapato ya wakulima, kuboresha mazingira ya maisha na kuinua hali ya maisha ya wananchi.

Lakini kwa upande mwingine, katika miaka ya karibuni sekta ya uzalishaji maua ya China imekumbwa na hali ya kuongezeka kwa kasi kupita kiasi, na kuwa na sifa duni na ufanisi mdogo, maua ya China hayana ushindani kwenye soko la kimataifa. Kwa hivyo, Bi. Jiang Zehui aliainisha kuwa, China inatakiwa kupunguza kasi ya ongezeko la sekta ya maua, kuboresha mfumo wa uzalishaji na aina za maua, ili kutimiza lengo la kuinua ufanisi wa kiuchumi kwa kutegemea maendeleo ya sayansi na teknolojia na kuinua sifa ya wafanyakazi badala ya kuongeza uwekezaji, na eneo la kuzalisha maua.

China ina historia ya miaka 20 na zaidi tu ya kuzalisha maua, ikiwa sekta mpya ya uzalishaji mali, sekta ya maua inaongezeka kwa haraka sana. Katika miaka 20 kuanzia mwaka 1984 hadi mwaka 2003, eneo lililopandwa maua nchini China liliongezeka mara 27 na kufikia hekta laki 4.35, ambapo thamani ya uzalishaji wa maua iliongezeka kwa mara 57 na kufikia yuan bilioni 35.3, na thamani ya maua yaliyosafirishwa nje iliongezeka kwa mara 47 na kufikia dola za kimarekani milioni 97.56.

Katika China bara, sehemu zinazozalisha maua kwa wingi zaidi ni mikoa ya Guangdong, Yunnan, Fujian na Zhejiang na mji wa Shanghai. Maua hayo mengi yanasafirishwa katika nchi za Ulaya, Marekani na Japan.

Idhaa ya kiswahili 2005-05-19