Ufundi wa kuwawezesha samaki sturgeon wazaliane kwa kuhimizwa na nguvu za binadamu siku zote ni tumainio kubwa la wanasayansi wa China, baada ya kufanya juhudi za vizazi vitatu kwa wanasayansi, mpaka sasa ufundi huo bado haujaweza kupatikana. Siku chache zilizopita wanasayansi wa China walianzisha mpango wa utafiti wa kisayansi wa kupata maendeleo makubwa kuhusu ufundi huo ndani ya miaka mitatu au minne.
Samaki sturgeon ni aina moja ya samaki adimu, ambao wanapatikana nchini China tu. Katika miaka milioni 150 iliyopita, aina hiyo ya samaki ilikuwa inaishi pamoja na wanyama wakubwa wa zamani (dinosaur), hivi sasa wanyama hao walitoweka kabisa, lakini samaki wa aina hiyo bado wamebaki. Ndiyo maana, samaki wa aina hiyo wanaitwa "visukuku vihai" na "panda wa majini", yaani samaki waliokuwepo kwa muda mrefu. Urefu wa samaki wazima wa aina hiyo huwa ni mita 4, na uzito wake hufikia tani moja, na wanaweza kuishi kwa muda wa miaka zaidi ya 100.
Kila ifikapo majira ya mpukutiko, samaki wa aina hiyo wanaopevuka huogelea kwa umbali wa kilomita elfu kadhaa kutoka baharini kuelekea kwenye sehemu ya juu ya mto Changjiang, ambao ni mto wa kwanza kwa ukubwa nchini China, na kutaga mayai, na baada ya mayai hayo kuanguliwa, vitoto vya samaki vitaogelea kwa muda wa nusu mwaka kurudi baharini, na kuishi huko kwa miaka 18 mpaka watakapopevuka, halafu watafunga safari kurudi nyumbani, yaani sehemu ya juu ya mto Changjiang. Lakini kuanzia miaka ya 50 ya karne iliyopita, kutokana na uvuvi wa kupita kiasi, uchafuzi wa mazingira ya mto Changjiang na matawi yake, na wingi wa ujenzi wa miradi ya maji, maisha ya samaki wa aina hiyo yameathirika sana, wanapata shida nyingi wakati wanaporudi nyumbani kutaga mayai, hivyo hivi sasa idadi ya aina hiyo ya samaki inapungua kwa kiasi kikubwa, na wanakabiliwa na hatari ya kutoweka.
Kwa kawaida, njia nzuri zaidi ya kuwaokoa wanyama wanaokaribia kutoweka ni kuwawezesha wazaliane kwa kuhimizwa na nguvu za binadamu. Wanasayansi wa viumbe wa majini wa China walianza kutafiti ufundi huo kuanzia miaka ya 70 ya karne iliyopita. Mwanasayansi wa taasisi ya viumbe wa majini ya China Daktari Wei Qiwei, alisema kuwa kazi hiyo bado haijapata maendeleo makubwa. Alisema:
"Tumefanya juhudi kwa muda wa miaka zaidi ya 30, lakini mpaka sasa bado hatujapata mafanikio. Hivi sasa, tunaweza tu kutegemea njia ya kuvua samaki wa aina hiyo wasio wa mifugo kutoa nguvu za binadamu ili wazaliane."
Habari zinasema kuwa ufundi wa kuwawezesha samaki wa aina hiyo kuzaliana kwa nguvu ya binadamu kwenye maji baridi umepevuka sana nchini China, hivi sasa wanasayansi wa China wanafanya juhudi katika kupata ufundi wa kuwawezesha samaki wa aina hiyo waliozaliwa kwa njia hiyo wazaliane na kupata samaki wa kizazi cha pili, ili aina hiyo ya samaki inaweza kudumishwa duniani.
Baada ya utafiti wa muda mrefu, wanasayansi wamegundua kuwa ukuaji wa aina hiyo ya samaki na upevukaji wa vichocheo vyake unahitaji mazingira mazuri sana, kama wakiwekwa kwenye mazingira yasiyofikia kiwango fulani, watapevuka polepole, au hata hawatapevuka kabisa.
Hivyo, wataalamu wanaona kuwa hatua ya mwanzo ya kutatua tatizo hilo ni kuweka mazingira yanayowafaa samaki wa aina hiyo. Siku chache zilizopita, taasisi ya utafiti wa viumbe wa majini ya China ilisafirisha vitoto vya samaki wa aina hiyo waliozaliwa kwa nguvu za binadamu kwenda kwenye Jumba la maonesho ya viumbe baharini la Beijing kutoka mkoa wa Hubei, na kuwafuga kwenye bwawa la jumba hilo ambalo lilikuwa ni kwa ajili ya papa.
Meneja wa jumba hilo Bw. Hu Haifeng alifahamisha kuwa wanaweza kudhibiti ujoto na kiasi cha chumvi kwenye maji kwa kutumia chombo maalum, hivyo wanaweza kuweka mazingira yenye ubora unaotakiwa, ili samaki hao wapevuke. Pia alisema kuwa wanasayansi watapata takwimu mbalimbali kuhusu hali ya samaki hao katika kila kipindi cha ukuaji wao kwa kupitia chombo cha usimamizi ambacho ni cha kisasa zaidi.
Dakatari Wei alisema kuwa katika mazingira yao ya kawaida, wastani wa kupevuka kwa samaki wa aina hiyo ni miaka 18, na wanasayansi wanatumai kuwa watapevuka mapema kwa kufugwa kwenye mazingira yasiyo ya asili. Alisema:
"Kama samaki wa aina hiyo wakiwekwa kwenye mazingira yenye ujoto mwafaka, watakua haraka, uzito wao utafikia uzito samaki wazima wanaokuwa nao kwenye mazingira ya asili, na watapevuka mapema."
Aidha, wanasayansi wa China wametengeneza chakula maalum kwa samaki wa aina hiyo, ili kuhimiza upevukaji wa vichocheo vyake.
Kwa mujibu wa mpango wa taasisi ya viumbe wa majini ya China, samaki hao wenye umri wa miaka saba au minane wanaozaliwa kwa kuhimizwa na nguvu ya binadamu ambao hivi sasa wanafugwa kwenye jumba la maonesho ya viumbe baharini la Beijing watakuwa wamepevuka baada ya miaka mitatu au minne, na watakuwa na uwezo wa kuzaliana.
Idhaa ya kiswahili 2005-05-25
|