Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-05-30 14:59:07    
Shamrashamra katika sikukuu ya kikabila

cri

Tarehe 15 Mei ilikuwa ni sikukuu ya jadi ya makabila yaliyoko kusini magharibi mwa China, katika siku hiyo shamshara zilipamba moto katika mji wa Guiyang mkoani Guizhou. Guiyang ni mji wenye makabila mengi madogo madogo ya Wamiao, Wabuyi, Wadong na Wayao na mengine jumla 52. Kila mwaka watu wa makabila hayo hufanya sherehe kubwa za aina mbalimbali katika mji huo. Mashindano ya michezo ya jadi yalifanyika katika mitaa yote kumi, wanamichezo kutoka makabila madogo madogo 52 walishiriki kwenye mashindano huku wakishangiliwa na watazamaji. Na katikati ya mji watu wa makabila madogo madogo waliovaa mavazi rasmi ya kikabila walicheza ngoma huku waskipiga filimbi, tarumbeta na ala nyingine za muziki, watazamaji kiasi cha laki moja walikuja kuwashangilia. Mwandishi alizungumza na wachezaji kadhaa,

"Mimi ni m-miao, leo ni sikukuu yetu."

"Leo pia ni sikukuu ya kabila letu Wabuyi".

"Tumekuja kuwapongeza wenzetu."

"Leo ni sikukuu yetu ya jadi ya kuwakumbuka mashujaa wetu wa kabila la Wamiao."

Sikukuu hiyo ina masimulizi mengi, lakini wengi wanaeleza kuwa hii ni siku ya kuwakumbuka mashujaa wa kabila la Wamiao wa enzi za kale waliokufa na kuzikwa katikati ya mji wa Guiyang. Ili kuwakumbuka mashujaa hao kila mwaka watu hukusanyika mjini hapo kuwakumbuka. Guiyang ni mji wenye watu wa makabila madogo madogo 52, uhusiano kati ya makabila hayo ni mzuri, kwa hiyo siku hiyo ya kuwakumbuka mashujaa wa kabila la Wamiao imekuwa sikukuu ya makabila yote, kila mwaka wanaoshiriki katika sherehe hiyo hufikia zaidi ya laki mbili.

Ili kudumisha utamaduni wa jadi, licha ya kuwapangia waimbaji wa kulipwa jukwaa la michezo yao, pia yanaandaliwa mashindano ya waimbaji wa kienyeji na mashindano ya insha yenye jina la "Mimi na kabila langu". Ofisa wa Idara ya Shughuli za Dini mjini Guiyang Bi. Tan Xiaochun alisema, shughuli zote hizo ni kwa ajili ya kuenzi utamaduni wa kikabila na kuwaibua wapenda utamaduni na sanaa za kikabila. Alisema, " Mwaka huu tumeunganisha michezo ya kisasa na ya jadi ili kuhifadhi na kuenzi utamaduni wa jadi wa kikabila. Kwenye mashindano ya waimbaji hapo kabla tuliwaalika tu waimbaji kutoka makundi ya wasanii lakini mwaka huu pia tumewapatia waimbaji wenyeji nafasi za kuonesha uhodari wao, tumegawa makundi mawili ambayo moja ni kundi la waimbaji wa makundi ya wasanii, na kundi jingine ni la waimbaji wenyeji ambao zamani hawakuwahi kuonesha uhodari wao hadharani."

Katika mashindano ya michezo ya wenyeji, watu wa makabila mbalimbali walionesha uhodari wao. Kuna michezo ya kuchezesha simba wa bandia, maonesho ya sanaa ya utarizi wa kabila la Wamiao, opera za kienyeji zilizochezwa kwa miaka mingi, na mchezo wa kibao cha kukalia chenye urefu wa mita moja hivi kilichoshikwa na vijana wanne na kucheza cheza na kuunganisha vibao hivyo vingi kama dragoni. Mtoto wa kike ambaye hajatimiza umri wa miaka 14 alizungusha sahani kwa ncha ya jambia akisimama juu ya mayai manne mabichi. Mchezo ulioshangaza zaidi ni jinsi mzee Ji Jingyu alivyocheza bila viatu kwenye makali ya upanga mkubwa wenye urefu zaidi ya mita sita na wenye uzito kilo 400, kwenye makali hayo mara alitembea mbele mara alirudi nyuma, mara alisimama kwa mguu mmoja. Mchezo wake uliwashitusha na kushangiliwa sana na watazamaji. Imefahamika kuwa mzee huyo alipenda mchezo huo toka utotoni mwake, alifanya mazoezi kwa miaka kumi, alipohojiwa na waandishi wa habari alisema, "Jamii inaendelea, sanaa pia lazima iendelee. Wasanii wa jadi wanapaswa kuendeleza sanaa yao."

Mwaka huu sherehe ya sikukuu imewapatia nafasi waimbaji wa kienyeji kuonesha uhodari wao. Wamiao watatu waliimba huku wakicheza ngoma kwa fimbo za mianzi zenye rangi. Nyimbo na ngoma zao za kiasili ziliwafurahisha sana watazamani na waamuzi wa mashindano, waimbaji hao walipata tuzo ya kwanza. Mkuu wa Kundi la Nyimbo na Ngoma la Mkoa wa Guizhou alisema, "Mimi nashughulika na muziki wa kikabila, kwa hiyo nafuatilia sana hali ya muziki wa kikabila. Hivi sasa utamaduni wa kiasili wa aina nyingi umekuwa katika hatari ya kutoweka. Nyimbo za kiasili walizoimba zinanitia msisimko, naona kuwa ni kwa kufanya hivyo tu ndio tunaweza kurithi muziki wa kiasili, na baada ya kuurithi tu ndipo tunapoweza kuuendeleza."

Katika sherehe ya siku hiyo pia yalipangwa mashindano ya warembo, kwa jina la "ua la kikabila", wasichana kutoka makabila ya Wamiao, Wahui, Wabuyi, Watibet, Wayi, walivutia kwa sura na pia kwa uhodari wao wa kisanii.

Ofisa wa Idara ya Shughuli za Dini Bi. Tan Xiaochun alisema, kwa kufanya mashindano ya warembo pamoja na mashindano ya insha, licha ya kuonesha uzuri wa vijana wa makabila hayo pia yanawafanya wapende zaidi utamaduni na usanii wao.

Idhaa ya kiswahili 2005-05-30