Mjumbe maalum wa Marekani anayeshughulikia mambo ya ugonjwa wa Ukimwi duniani Bw. Randy Tobias tarehe 7 hapa Beijing amesema kuwa, ahadi zilizotolewa na viongozi wa China kuhusu kukinga na kutibu ugonjwa huo, na kazi zilizofanywa na madaktari wa China zinatia moyo sana, na anatumai kuwa China na Marekani zitaweza kuendelea kuimarisha ushirikiano katika shughuli za kukinga na kutibu ugonjwa wa Ukimwi.
Bw. Tobias anashughulikia kusimamia miradi ya ushirikiano wa kukinga na kutibu ugonjwa huo nchini Marekani na kwenye nchi nyingine. Alisema kuwa, mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi bado yatachukua muda mrefu, na binadamu wataweza tu kukabiliana na ugonjwa huo kwa kushirikiana na kuchukua hatua za pamoja.
Marekani inapanga kutoa dola za kimarekani milioni 35 kwa China kuanzia mwaka 2004 hadi mwaka 2008, kwa ajili ya miradi ya ushirikiano kati ya nchi hizo mbili kuhusu shughuli hizo. Mpaka sasa, miradi mingi imeanzishwa.
|