Kuanzia mwishoni mwa jamii ya kiasili ya binadamu, watu walioishi katika mabonde ya Mto Manjano na Mto Changjiang nchini China walianza kufinyanga sanamu kwa udongo. Sanamu nyingi zilizofinyangwa na watu walioishi katika bonde la Mto Changjiang zilikuwa ni sanamu za wanyama. Mwaka 1974, Sanamu zaidi ya elfu 6 za askari na farasi ziligunduliwa huko Lintong mkoani Shaanxi, ambazo zilistaajabisha dunia nzima. Sanamu hizo za askari na farasi zilizotengenezwa katika Enzi za Qin (221 kk.-206 kk) zilisifiwa kuwa ni ajabu la nane duniani. Zimeonesha nguvu kubwa za jeshi la mfalme wa enzi hiyo Qinshihuang zilipoteka madola sita. Sanamu hizo zinafanana na binadamu, mikokoteni na farasi wa kweli, na zote zina thamani kubwa ya kisanaa. Sanamu iitwayo farasi anayekanyaga kwenye mbayuwayu anayeruka, ambayo iligunduliwa katika kaburi moja la Enzi ya Han (206 kk-220 bk) mkoani Gansu, ni sanamu ya shaba nyeusi iliyotengenezwa kwa ufundi wa hali ya juu, na imeonesha vizuri nguvu ya farasi anayekimbia kwa kasi sana.
Mawe yenye nakshi ambayo yanavuma sana katika Enzi ya Han ni aina maalum ya sanamu iliyochongwa kwa kujitokeza katika msingi wake. Mawe hayo hutumiwa kama ni mapambo katika mahekalu na makaburi. Yanaonesha maisha ya kila siku yakiwemo mashamba, magari, mikutano, tafrija, uwindaji na karakana, hivyo yana thamani kubwa katika utafiti wa historia.
Sanamu zilizochongwa ndani ya mapango ya Mogao, mapango ya Yungang, Longmen na Maijishan ni sanaa adimu. Sanamu katika mapango hayo zinahusu hadithi ya dini ya Buddha. Sanamu ndani ya mapango ya Mogao huko Dunhuang ziliendelea kuchongwa kwa miaka zaidi ya elfu moja kuanzia Enzi ya Qin hadi kufikia Enzi ya Yuan (1271 bk-1368 bk). Hivi sasa bado kuna mapango zaidi ya elfu 7 na mapango makubwa 492 huko, ambako nyaraka zaidi ya elfu 50 zinahifadhiwa ndani yake. Tena kuna picha zaidi ya mita za mraba elfu 45 ukutani, sanamu zaidi ya elfu 3 zenye rangi, nguzo zenye nakshi ya mayungiyungi na maelfu ya marumaru zenye mapambo sakafuni. Mapango ya Dunhuang ni hazina ya sanaa ya dini ya Buddha.
Sanamu kubwa ya Buddha mlimani Leshan mkoani Sichuan urefu wake karibu sawa na mlima. Sanamu za simba ni aina muhimu ya sanaa za uchongaji na ufinyanzi nchini China. Sanamu hizo hutengenezwa kwa shaba nyeusi, mawe na chuma. Sanamu kubwa zaidi ya simba iliyotengenezwa kwa chuma nchini China ni sanamu inahifadhiwa huko Cangzhou mkoani Hebei. Msahafu wa dini ya buddha na kumbukumbu ya wilaya ya Cangxian vilichongwa kwenye tumbo la sanamu hiyo.
picha husika >>
1 2 3 4
|