Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-06-15 20:39:44    
mfumo wa kisasa wa usafiri wa mabasi wa Beijing

cri

Watu wanaopanda mabasi mara kwa mara labda wote wamewahi kusubiri basi kwa muda mrefu, hali hiyo inatokana na kuwa watu wanaosubiri mabasi hawawezi kujua wakati sahihi wa kufika kwa mabasi.

Lakini hivi sasa, watu wanaopanda basi No. 420 kwenye sehemu ya mashariki ya mji wa Beijing hawana tena usumbufu kama huo. Kwa sababu mabasi ya No. 420 ni mabasi ya njia ya kwanza mjini Beijing yaliyowekwa mfumo wa kisasa wa usafiri wa mabasi, watu watajua saa sahihi ya kufika kwa mabasi yanayokuja kwa kuangalia vibao vya vituo vya mabasi.

Kwa ufupi, mfumo huo unaundwa na sehemu tatu: sehemu ya kwanza ni zana za elektroni zilizowekwa kwenye mabasi, kazi yake kuu ni kukusanya taarifa ya usafiri wa mabasi hayo na kuituma kupitia antenna; sehemu ya pili ni kituo cha taarifa katika idara ya usimamizi ya mabasi, inaweza kupokea taarifa zilizotumwa kutoka kwenye mabasi. Baada ya kushughulikiwa na kompyuta, taarifa kuhusu saa sahihi ya kufika kwa mabasi zitatumiwa kwa sehemu ya tatu ya mfumo huo, yaani vibanda vya kisasa vya vituo vya mabasi.

Hivi sasa, vibanda hivyo vimewekwa kwenye kila kituo cha mabasi ya No. 420. kibanda hicho kina nguzo moja ya pembe tatu yenye urefu wa mita 3, na kila upande wa nguzo hiyo kuna skrini moja.

Mhandisi mmoja aliyeshiriki kusanifu mfumo huo Bw. Chen Wenlong alieleza,

"skrini hizo zinaonesha taarifa kuhusu usafiri wa mabasi. kwa mfano, mabasi yamefika kwenye vituo gani na saa ngapi yatafika kituo hiki."

Habari zinasema kuwa, mfumo huo umetumika kwa majaribio katika mabasi ya No. 420 kwa mwaka mmoja, abiria wa mabasi hayo wameridhika sana na mfumo huo. abiria mmoja alisema:

"naona vibanda hivyo vinavyoonesha saa za kufika kwa mabasi, ni vizuri sana."

mbali na uwezo wa kuonesha saa za kufika kwa mabasi, mfumo huo pia una uwezo mwingine. skrini hizo pia zinaonesha saa na taarifa nyingine, zikiwemo habari muhimu, taarifa ya serikali, utabiri wa hali ya hewa na hali ya mawasiliano barabarani. Wakati matukio ya dharura, yakiwemo hali mbaya ya hewa au ajali kubwa za barabarani au maambukizi ya maradhi, yakitokea, skrini hizo zitaonesha mara moja taarifa kuhusu matukio hayo, hata wakati wa usiku, taarifa hizo zinaonekana vizuri.

Bw. Jiang anapanda mabasi ya No. 420 mara kwa mara. Alisema:

"vibanda hivyo vinaonesha saa au hali ya hewa, ni vizuri sana. siku moja, nilipokuwa nasubiri mabasi kwenye vituo hivyo, niliona kuwa mvua itanyesha alasiri ya siku hiyo, hivyo nilirudi nyumbani na kuanua nguo nilizokuwa nimezianika."

Aidha, kwenye paa la vibanda hivyo, kuna kamera inayoweza kuzunguka kwa nyuzi 270. kupitia kamera hizo, sio tu maofisa wa idara ya usimamizi ya mabasi wanaweza kusimamia hali ya mawasiliano barabarani, bali pia wanaweza kujua idadi ya abiria wanaosubiri mabasi vituoni, na kudhibiti usafiri wa mabasi njiani.

Mfumo huo pia una uwezo mwingine muhimu yaani kuelekeza abiria wasioona kupanda mabasi. Hivi sasa, wahandisi wa China wamefanikiwa kusanifu zana za mikononi kwa ajili ya abiria wasioona. Bw. Chen Wenlong alieleza:

"abiria wasioona wanaotumia zana hizo wakikaribia kwenye vituo vya mabasi, zana hizo zitatoa ishara ya sauti na kuwatambulisha wapo kwenye kituo gani, mabasi gani yatapita kwenye kituo hicho. Wakati basi fulani ikifika kwenye kituo hicho, zana hizo zitatoa ishara ya sauti."

Bw. Chen alisema kuwa, mbali na uwezo huo, zana hizo za mikononi pia zitatoa taarifa kuhusu hali ya hewa au habari muhimu. Aidha, abiria wasioona pia wataweza kutumia zana hizo kuomba misaada.

Habari zinasema kuwa, ili kuzidi kupanua uwezo wa mfumo huo, wahandisi wa China wanaendelea kufanya utafiti, na kutarajia kuwa mfumo huo utaweza kutoa huduma ya Internet na huduma ya kuongeza fedha kwenye kadi ya kupandia basi.

Ingawa mfumo huo bado unatumika katika mabasi ya njia moja, lakini ili kuongeza kiwango cha huduma kamili za usafiri wa umma mjini, Beijing itachukua hatua madhubuti na kuweka mfumo huo kwenye mabasi yote mjini humo kabla ya michezo ya Olimpiki ya mwaka 2008. mbali na Beijing, mji wa shanghai pia umeanza kufanya majaribio ya mfumo huo.

Idhaa ya Kiswahili 2005-06-15