Wushu (mbinu za kujihami za Kichina), ambayo hujulikana kwenye nchi za Magharibi kwa jina la gongfu, imeenea duniani kote kutokana na filamu za kungu mnamo miaka ya 1960 na 1970. ingawa filamu hizo zilipendwa na kustaajabisha sana, gongfu hutiwa chumvi mno kwenye filamu hizo. Sehemu za karibu ya mwisho za filamu zinazoonyesha umwagaji wa damu hupotoshwa na kuleta athari kubwa.
Wushu ya Shaolin ilitokana na Hekalu la Shaolin kwenye misitu ya Milima Songshan walayani Dengfeng, mkoani Henan. Masufii wengi wa hekalu hilo ni mabingwa wa wushu wenye uwezo wa kusimama vichwa chini miguu juu bila ya misaada ya mikono yao, kukandamiza koo zao kwenye ncha za chusa bila ya kuumia, kuvunja mawe kwa ngumi na kuangusha miti kwa kiganja.
Tofauti na ngumi za nchi za Magharibi au karate ya kijapani, wushu ya Shaolin imeambatana sana na dini, hususan ya Kibuddha.
Hakuna ushahidi wowote kuhusu nani ni mwanzilishi wa wushu ya Shaolin wala lini ilianza. Baadhi ya watu wanasema kwamba ilianzishwa na Sufii wa kihindi Bodhidharma kwenye Hekalu la Shaolin mnamo mwaka 527 B.K. Madhehebu ya Kibuddha ya Mahayana, hufundisha kwamba nguvu ya Buddha imo kwenye mwili wa kila mtu, lakini imetulia. Si kama itachochewa kwa kusoma misahafu na kanuni za kupambanua vizuri bali ni kwa kutafakari kimyakimya kwenye pango la majabali huku ukifumba macho. Ili kutambua vilivyo nguvu ya Buddha, Sufii huyo wa Kihindi alitumia miaka mingi kwa taamuli huku akikaa tuli kwenye pango la mawe. Ili kujipa nguvu mpya baada ya taamuli ya muda mrefu, alifanya mazoezi aliyoyabuni yenye mitindo 18. mfano wake uliigwa na wanafunzi wake na kadri miaka ilivyopita ndivyo mazoezi hayo yalivyoboreshwa na kukuzwa nchini China hadi kufikia mtindo wa pekee wa wushu.
Wushu imekuwa ni sehemu ya ratiba ya kila siku ya masufii wa Hekalu la Shaolin. Hutumika kuleta mwamko wa nguvu ya Buddha, kushupaza mwili na nyakati nyingine kwa kujihami. Hata hivyo mkazo hutiliwa kwenye kuyaelewa maisha, kujenga uadilifu na kupata maisha yenye uwiano.
Dini ya Kibuddha ni falsafa iliyoingizwa China kutoka India na kuchanganyika na ya Confucius na Kidao miaka mingi iliyopita na kuifungulia njia wushu kustawi vizuri.
Wushu ya Kichina inaweza kugawanyika katika mitindo ya kaskazini na kusini. Wa kwanza ulianzia kwenye Hekalu la Kibuddha la Shaolin na wa pili ulianzia Milima ya Wudang, kwenye madhababu maarufu ya Kidao, mkoani Hubei.
Wushu ya Shaolin huchanganya mazoezi ya mikono mitupu na yenye silaha, ya mtu mmoja mmoja au jozi, yanayofanywa kwa utaratibu maalum ulioamuliwa. Katika kupambana karibukaribu husisitiza mbinu k.v. "mwangushe adui wako kwa kutumia nguvu zake," "geresha kushoto lakini shambulia kulia," "kufanya kama unashambulia kusudi uweze kurudi nyuma" na "rudi nyuma ili uweze kushambulia".
Idhaa ya Kiswahili 2005-06-17
|