Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-06-22 16:34:44    
Kijana Mtetezi wa Haki

cri

Yuan Xiaoping ni mtoto wa wakulima aliyebahatika kuwa mwanafunzi wa chuo kikuu, ana moyo mkunjufu wa kuwasaidia wengine katika maisha yake ya kawaida. Lakini mwanafunzi huyo alijitolea maisha yake alipomwokoa mwenzake katika mapambano dhidi ya majambazi.

Yuan Xiaoping alikuwa mwanafunzi wa kidato cha pili katika Chuo Kikuu cha Tiba mkoani Shanxi, alizaliwa katika ukoo wa wakulima. Ili kumsomesha, wazazi wake walitumia akiba yote wakitumai kuwa, baadaye angeweza kubadilisha hali yao ya umaskini.

Lakini mwezi Aprili mwanafunzi huyo Yuan Xiaoping alipopambana na majambazi alisahau matumaini ya wazazi wake na hata alijisahau binafsi yake, aliuawa.

"Tarehe 16 mwezi Aprili, saa tatu za usiku, mimi pamoja na Yuan Xiaoping tulikwenda kwenye duka la kujihudumia baada ya tamasha la nyimbo shuleni,tukiwa njiani kurudi nilituma ujumbe kwa simu ya mkononi, kabla sijamaliza ujumbe na kuutuma, nyuma yangu walijitokeza watu watatu wakitaka kunyakua simu yangu, nilipurukushana nao, ghafla mmoja wao alichomoa jambia na kutia shingoni mwangu. Wakati huo Yuan Xiaoping alimrukia kuniokoa, papo hapo yule mwenye jambia alimchoma kifuani mara tatu." Tukio hilo lilitokea miezi miwili iliyopita, lakini huyo aliyeokolewa alipotaja, macho yake yalitoa machozi. Alisema, "Jambo hilo lilitokea ghafla, dakika chache tu kabla sijafahamu jambo lenyewe, Yuan Xiaoping alikuwa ameanguka, huku damu ikimtoka."

Ilifahamika kuwa jambia lilimchoma kwenye moyo mara tatu. Alipokimbizwa hospitali alikufa njiani.

Machoni mwa walimu na wanafunzi wenzake, Yuan Xiaoping alikuwa mwanafunzi wa kawaida kabisa, lakini mwenye tabia nzuri na maadili mema kabisa. wanafunzi wenzake walisema, Yuan Xiaoping ni mvumilivu wa mambo yake binafsi. Walieleza, "Mwaka jana katika siku za likizo, tulifanya kazi katika baa moja kwa ajili ya kujipatia pesa za kusaidia masomo, tulifanya kazi kwa siku 20 hivi, lakini bosi alituachisha bila sababu na hakutulipa haki yetu hata senti moja. Ingawa pesa zilikuwa si nyingi lakini kwa Yuan Xiaoping, mwanafunzi maskini, zina maana sana. Yuan Xiaoping alikuwa kimya na mara nyingi alitushawishi tusijali sana, na tusijaribu kufanya kitendo cha kukiuka sheria na kuleta hasara kwa masomo"

Lakini mwenzake alipokutwa na hatari, Yuan Xiaping alijitokeza kumlinda bila kujifikiria mwenyewe. Huu sio msisimko wa ghafla bali unatokana na asili yake ya kupenda kuwasaidia wengine na kutokubali uonevu.

Kila muhula mpya ulipoanza, Yuan Xiaoping alikuwa akifika shuleni mapema kuliko wengine, aliwasaidia wenzake kuanika mifarishi. Mwenzake Li Gang alisema, katika bweni letu yeye alikuwa hujituma kusafisha safisha na kukinga maji ya moto kwa ajili yetu."

Katika chuo kikuu Yuan Xiaoping alikuwa ni mwanafunzi mwenye juhudi za kushiriki kwenye shughuli za shule. Katika mashindano ya michezo alijitolea kuwasaidia wachezaji kutunza nguo zao na kuwapelekea maji. Aliposoma katika shule ya sekondari ya ufundi, mwenzake mmoja alipoteza ada ya shule yuan elfu tatu, Yuan Xiaoping alipojua jambo hilo alisaidia kwa pesa zake zote alizokuwa nazo yuan mia mbili.

Baada ya Yuan Xiaoping kufariki, moyo wake wa kupenda kuwasaidia wengine na ushupavu wake wa kuthubutu kupambana na watu wabaya ulienea miongoni mwa wanafunzi na walimu na kitendo chake kiliwagusa moyo. Chuo kikuu hicho kilimpa sifa ya "mwanafunzi bora wa kuthubutu kupambana na watu wabaya". Walimu na wanafunzi kwa hiari walichanga fedha kuwasaidia wazazi wake, wanasema, yeye ni mwenzetu na daima anaishi mioyoni mwetu.

Idhaa ya kiswahili 2005-06-22