Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-06-22 21:09:51    
Maonesho ya Beijing ya bidhaa za teknolojia ya hali ya juu

cri

Kama wewe ni mfanyabiashara, ni lazima una kadi nyingi za watu za utambulisho kama uliwahi kuwa na wasiwasi kuhusu kushughulikia kadi hizo, sasa usiwe na wasiwasi, chombo kidogo kinachoweza kusoma kadi hizo kitakusaidia, kitahifadhi kumbukumbu zote zilizoko kwenye kadi ya utambulisho ya mtu fulani, na wakati wowote kama ukitaka kujua kumbukumbu za mtu huyo, unaandika jina lake tu, na kumbukumbu zake zote zitaoneshwa kwenye kioo cha chombo hicho; kama wewe ni shabiki wa filamu, chombo kipya cha kuoneshea filamu kinaweza kukidhi mahitaji yako yote, kinaweza kuonesha filamu vizuri zaidi, na kukufanya usikie sauti ya filamu vizuri.

Hivyo vyote ni vifaa vilivyooneshwa kwenye maonesho ya 8 ya bidhaa za teknolojia ya hali ya juu ambayo yalifunguliwa hivi karibuni hapa Beijing. Maonesho hayo yamefanyika kwa mara 8, na viwanda maarufu vya nchini na nchi za nje vilishiriki kwenye maonesho hayo na kuonesha bidhaa zao mpya kabisa.

Kwenye sehemu moja ya ukumbi wa maonesho, shirika moja liliipamba sehemu hiyo kama ofisi, ambapo kuna kompyuta, projekta, mitambo ya kuchapisha na vifaa vingine vya kiofisi, ingawa mwandishi wetu wa habari hakuona waya wowote unaounganisha vifaa hivyo, lakini vilikuwa vimeunganishwa, yaani vimeunganishwa bila waya wowote. Wafanyakazi wanapotaka kuwaonesha wateja bidhaa mpya kabisa za kampuni yao wataweka kompyuta karibu na projekta ndani ya mita 100, na projekta itafanya kazi na kuonesha picha zilizohifadhiwa kwenye kompyuta ukutani, kama wakati huo huo wakitaka kutumia maelezo ya bidhaa hizo zilizohifadhiwa kwenye kompyuta nyingine, wataweka kompyuta hiyo karibu na kompyuta ya mwanzo, na kompyuta hizo mbili zitaunganishwa mara moja, na wafanyakazi wanaweza kutumia data yoyote wanayoitaka kutoka kwenye kompyuta nyingine.

Vifaa hivyo vinaunganishwa vipi? DK Li Ming anayeshiriki kwenye utafiti wa teknolojia hiyo alimfahamisha mwandishi wetu wa habari kuwa teknolojia hiyo inaitwa IGRS(Intelligent Grouping and Resource Sharing), akisema:

"Teknolojia hiyo inaweza kuziunganisha kompyuta na vifaa vingine vya umeme, kwa mfano, inaweza kuziunganisha televisheni na kompyuta, na raslimali za vifaa hivyo zinaweza kutumika kwenye kifaa kingine, yaani tunaweza kuona picha na video zilizohifadhiwa ndani ya kompyuta kwenye kioo cha televisheni, vilevile tunaweza kuhifadhi vipindi vya televisheni kwenye kompyuta."

Alisema, mbali na hayo, kama ukishiriki kwenye tafrija inayoandaliwa na marafiki zako, unaweza kupeleka muziki uliohifadhiwa kwenye simu yako ya mkononi hadi kwenye televisheni au radio zilizoko karibu, bila shaka, marafiki zako watashangaa sana.

Imefahamika kuwa China imeanza kutafiti teknolojia hiyo kuanzia mwaka 2003, mashirika mengi maarufu nchini China kama vile Lenovo na Konka yameshiriki kwenye utafiti wa teknolojia hiyo. Hivi sasa wamesanifu na kutengeneza simu ya mkononi, kompyuta, projekta na televisheni zenye teknolojia hiyo na wamefungua maduka mjini Beijing, Shanghai na Shenzhen, kwenye maduka hayo watu wanaweza kujaribu wenyewe kutumia vifaa hivyo vya teknolojia ya IGRS.

Kwenye maonesho hayo, bibi Men Bing, alimwambia mwandishi wetu wa habari akisema:

"Teknolojia hiyo itarahisisha maisha yetu, nimejaribu kutumia vifaa hivyo, naona televisheni na kompyuta zinaweza kuwasiliana bila matatizo yoyote."

Hivi sasa, vifaa vyenye teknolojia hiyo vinatumiwa na mashirika mengi, na vinasifiwa, lakini bado havijaanza kutumika sana kwenye familia za kawaida.

Kwenye maonesho hayo, mwandishi wetu wa habari aliona kuwa kuna bidhaa nyingi za teknolojia ya hali ya juu zinazohusu magari, kama vile kitu kinachoweza kubandikwa kwenye mrija wa mafuta wa gari, ili kupunguza matumizi ya mafuta. Kitu hicho kiliwavutia watu wengi.

Imefahamika kuwa kitu hicho kinatengenezwa kwa aina moja ya udongo, kikibandikwa kwenye mrija wa mafuta wa gari kitafanya kazi. Mwuzaji alifahamisha kuwa kitu hicho kinaweza kubadilisha muundo wa chembechembe za mafuta ili mafuta hayo yaweze kuchomwa kikamilifu zaidi, yaani kila tone la mafuta lifanye kazi, na kupunguza matumizi ya mafuta. Baada ya kuikagua, idara husika imethibitisha kuwa bidhaa hiyo inaweza kupunguza matumizi ya mafuta kwa asilimia 5. Ndiyo maana, bidhaa hiyo ina umuhimu mkubwa kwa China, ambayo inaagiza mafuta kwa wingi kutoka nchi za nje. Hivi sasa, idara husika za China zinaieneza bidhaa hiyo kwa juhudi.

Mbali na bidhaa hiyo inayoweza kupunguza matumizi ya mafuta, bidhaa nyingine inayoweza kuliongoza gari inafuatiliwa na watu wengi. Chombo hicho ni kidogo, kikiwekwa mbele ya dereva, hakitamwathiri hata kidogo. Imefahamika kuwa chombo hicho kinaweza kuliongoza gari kwenye sehemu yoyote ya China bara kwa kupokea ishara ya setlaiti. Dereva anahitaji tu kuandika sehemu anayotaka kwenda, chombo hicho kitapendekeza njia 4 za kufika huko, na akifika njiapanda, chombo hicho kitamwarifu kwa sauti.

Bw. Gao Feng, ambaye amenunua gari hivi karibuni, alikuwa anavutiwa na bidhaa hiyo akisema:

"Najifunza kuendesha gari hivi karibuni, naona ni vigumu kuendesha gari mjini Beijing, kwani mji huu mkubwa una barabara nyingi, kama nikiwa na chombo hicho, naweza kuelekezwa njia ya kufuata, kukata upande gani, taarifa ambazo ninazihitaji sana."

Wasikilizaji wapendwa, nakufikia hapa ndiyo tumekamilisha kipindi hiki cha elimu na afya, asanteni kwa kuwa nasi, ni mtangazaji wenu ni pomboo, nasema kwa herini.

Idhaa ya Kiswahili 2005-06-22