Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-06-23 21:43:52    
Wazee wa Beijing wapenda kufanya mazoezi kwa kuandika maandiko ya kichina sakafuni

cri

Katika miaka ya karibuni, wazee wa Beijing wanaopenda kufanya mazoezi ya asubuhi ya kujenga mwili kwenye bustani, licha ya kucheza michezo ya jadi kama vile mchezo wa Taiji na ngoma, sasa pia wanapenda shughuli nyingine yenye umaalum wa kiutamaduni, yaani kuandika maandiko ya kichina sakafuni.

Maandiko ya kichina ya jadi huandikwa kwa brashi iliyochovywa wino kwenye karatasi zilizotandikwa mezani. "Kalamu" ya kuandikia maandiko ya kichina sakafuni inatengenezwa kwa kufunga kipande cha sponji kilichokatwa kama kichwa cha kalamu kwenye mpini wenye urefu wa mita moja. Wazee hutumia "kalamu" hiyo ya sponji kuandika kwenye sakafu kwa kuchovya maji. Kwenye bustani ya Summer Palace iliyoko sehemu ya magharibi ya Beijing, mwandishi wetu wa habari alimkuta Bw. Zhou Shude na wazee wengine waliokuwa wanaandika sakafuni.

Bw. Zhou Shude mwenye umri wa miaka 60 amefanya mazoezi ya kuandika sakafuni kwa miaka minane. Anasema:

"Kuandika maandiko ya kichina sakafuni kunanisaidia sana kujenga mwili. Zamani nilipenda sanaa ya kuandika, lakini nilikuwa naandika kwenye karatasi kwa brashi iliyochovya wino, hivyo nilikuwa sina nafasi nyingi za kuandika maandiko makubwa namna hii, kutokana na gharama kubwa. Kuandika sakafuni hakuna gharama yoyote, sina haja ya kununua karatasi na wino, naweza kuandika ninavyopenda."

Kwenye bustani nyingine ya Yuyuantan, mwandishi wetu wa habari aliwakuta wazee zaidi ya 20 wanaopenda kufanya mazoezi hayo. Miongoni mwao, mzee Lian Qixian mwenye umri wa miaka 72 aliwavutia zaidi watalii, si kama tu kutokana na maandiko yake mazuri, bali pia kutokana na "kalamu" yake maalum aliyoitengeneza mwenyewe. Kwenye mpini wa "kalamu" yake kulikuwa na chombo cha kuwekea maji, ambacho kinaweka maji kwenye sponji, na maji yenyewe yanaweza kurekebishwa kutokana na mahitaji, hivyo wakati wa kuandika sakafuni, hana haja ya kutia sponji kwenye maji mara kwa mara.

Mzee Lian Qixian amekuwa na historia zaidi ya miaka 10 ya kuandika maandiko ya kichina sakafuni. Alivumbua "kalamu" hiyo kwa ajili ya kuandika sakafuni na kuipa jina la "kalamu ya kuandikia sakafuni ya watu wa China", na ataomba hakimiliki ya kitaifa. Mzee Lian kila anapoandika sakafuni kwa "kalamu" hiyo, huwavutia watu wengi ambao wanamzunguka na kumsifu kwa maandishi yake mazuri na "kalamu" yake maalum. Bw. Lian alisema kwa fahari kuwa, hivi sasa watu wengi wanataka kuagiza "kalamu" kutoka kwake. Lakini nia yake ya kuvumbua "kalamu" hiyo siyo kutokana na kujipatia faida, bali ni kuwarahisishia wazee wanaopenda kufanya mazoezi hayo. Anasema:

"Sasa idadi ya wazee inaongezeka siku hadi siku, kufanya mazoezi ya kuandika maandiko ya kichina sakafuni kunawasaidia wazee kujenga mwili, kuburudisha roho zao na kuinua hali yao ya kiutamaduni."

Mwandishi wa habari aliona kuwa, wazee hao wanaandika sakafuni huku wakijadiliana kuhusu ustadi wa sanaa ya kuandika. Wengi wao ni wachangamfu, wanapenda sana kuwaelekeza wapita njia jinsi ya kuandika vizuri sakafuni. Hivi sasa shughuli hiyo imekuwa kivutio kwenye bustani za mjini Beijing, ambacho kinawavutia sana watalii wa nchini na ng'ambo.

Kwenye bustani ya Jingshan, katikati ya mji wa Beijing, mtalii mmoja kutoka Korea ya Kusini aliwatazama wazee wakiandika sakafuni kwa muda mrefu. Anasema:

"Nyumbani kwangu kuna maandiko yaliyoandikwa na msanii maarufu wa Korea ya Kusini, maandiko yake yanafanana sana na yale yanayoandikwa na wazee hao. Wazee wa nchi yangu wanapenda kupanda mlima, na kukimbia, lakini wazee wa China wanaonekana wanapenda zaidi kufanya mazoezi kwa kuandika sakafuni au kurusha tiara."

Kuandika sakafuni kunahitaji maji tu, shughuli hiyo haina gharama yoyote, pia haileti uchafuzi wowote, hivyo inaungwa mkono sana na wasimamizi wa bustani.

Hivi sasa, kuandika maandiko sakafuni kumekuwa njia maalum ya sanaa ya kuandika, kunapendwa siku hadi siku na mashabiki wa sanaa hiyo nchini na wa ng'ambo. Mwalimu mmoja aliyefundisha sanaa ya kuandika kichina hapa Beijing alisema kuwa, katika darasa lake, kuna wanafunzi zaidi ya 10 kutoka Marekani, Ujerumani, Ufaransa, Japan, Korea ya Kusini na Singapore, wanapojifunza sanaa ya maandishi ya kichina ya jadi, pia wana hamu kubwa ya kujifunza sanaa ya kuandika sakafuni.