Mlima Liufeng uko katika wilaya ya Lingshan mkoani Guangxi, ni moja ya sehemu nane zenye mandhari nzuri wilayani.
Mawe ya rangi yanayopatikana kwenye mlima huo, kabla ya Enzi ya Ming yaliwahi kuwa miongoni mwa vitu vilivyopelekwa kwa wafalme sawa na lulu za Hepu mkoani humo. Katika historia ya Wilaya ya Lingshan imeandikwa kuwa mawe ya rangi, yaani yale mazuri miongoni mwa mawe, nayo ni bora kama jedi, huwa na mandhari ya milima, mito, misitu, moshi, mawingu, ndege na wanyama juu yake. Vyote hivyo huonekana kama halisi na vyenye mpangilio kama picha zilizochorwa. Mabombwe mengine hata wachoraji stadi wanashindwa kuyachora. Mawe hayo yakikatwa kuwa maumbo maalumu, huwa ni kama vitu vya kuchezea. Kwa hivyo mawe ya rangi ya Lingshan hapo kale yalikuwa yakikatwa na kunolewa kuwa mapambo kwenye samani au vyombo vya ukoo wa kifalme. Vito vya aina hiyo vya kimaumbile, vingi zaidi hufichwa kwenye magenge au ndani ya mapango ya mabondeni, hivyo ni taabu sana kuvichimbua. "Hata ukikata kidogo sana tu mabombwe yake huwa yanatofautiana na ya awali." Zaidi ya hayo, katika majabali makubwa na magenge ya hatari huwa si rahisi kupata mengi. Kupeleka mawe kwa wafalme kuliwaletea wananchi kero kubwa. Mpaka kipindi cha kati cha Enzi ya Ming maofisa wa wilaya walifikiri njia moja ya kuwasaidia wapelekaji hao, waliwaambia kisirisiri wayaponde mawe hayo njiani. Kwa kuwa Baraza la kifalme lilipokea mawe yaliyopondwa, likafuta jukumu lao la kupeleka zawadi ya aina hiyo kwa kudhani kuwa ubora wa mawe ya rangi ya Lingshan ni hafifu. Kuanzia hapo wenyeji waliacha kuchimbua na kutengeneza mawe ya rangi ya aina hiyo.
Mnamo majira ya mchipuko ya mwaka 1984 Chen Yijian, kada wa Shirikisho la Utamaduni la Wilaya ya Lingshan kwaza kuchimbua mawe ya aina hiyo, na aliwatembelea baadhi ya waashi wazawa wa kale, halafu alitafiti kwa makini ufundi wa watu wa kale wa kuchimbua mawe na kuyaboresha. Baada ya miaka sita akadhibiti ufundi wao. Katika miaka ya karibuni amekuwa akikuza kwa ushupavu hulka ya uchoraji wa Kichina na kurejea njia za uchongaji na ufinyanzi wakati wa kutengeneza vitu vya sanaa.
Alifanya mchakato wa kifundi kwa kufuata maumbo ya awali, mabombwe, milia, na rangi za mawe ya namna kwa namna na aliunda vitu vya sanaa vya mawe ya rangi vyenye hulka tofauti. Sanaa hizo zina picha za kishairi na za rangi za mchipuko katika mashamba. Warembo, wanajeshi, vidau vya wino, wadudu, wanyama, milima na mawingu vyote vinaonekana kama vitu hai.
Idhaa ya Kiswahili 2005-07-01
|