"Kongamano la uwekezaji la Asia ya mashariki" lenye lengo la kuimarisha ushirikiano wa uwekezaji kwenye sehemu ya Asia ya mashariki lilifanyika hivi karibuni katika mji wa Weihao ulioko sehemu ya mashariki ya China. Maofisa wa serikali, wanaviwanda na wataalamu kutoka China, Japan, Korea ya kusini na nchi 10 za Umoja wa Asia ya Kusini Mashariki walikuwa na majadiliano kuhusu maendeleo ya uchumi, mazingira ya uwekezaji na ushirikiano wa mambo ya fedha wa sehemu ya Asia ya mashariki. Washiriki wa mkutano wanaona kuwa ushirikiano wa uwekezaji wa kikanda kati ya nchi za Asia ya mashariki umepata mafanikio na uwezo wa ushirikiano katika siku za baadaye ni mkubwa, na China inafanya kazi muhimu katika kuhimiza ushirikiano wa uwekezaji katika sehemu ya Asia ya mashariki.
Katika miaka ya karibuni sehemu ya Asia ya mashariki zikiwemo China, Japan na nchi kumi za Umoja wa Asia ya Kusini Mashariki ni sehemu yenye ongezeko la kasi zaidi duniani. Hivi sasa pato la sehemu ya Asia ya mashariki limezidi dola za kimarekani trilioni 7.7 ikiwa ni 20% ya pato la dunia nzima. Katika maendeleo ya uchumi wa Asia ya mashariki ushirikiano wa kikanda umekuwa nguvu muhimu ya kuhimiza maendeleo ya sehemu hiyo. Takwimu zinaonesha kuwa mwaka 2004, biashara ya sehemu ya Asia ya mashariki inazidi nusu ya thamani ya bidhaa zinazosafirishwa nje na uwekezaji wa sehemu hiyo inachukua theluthi mbili za jumla ya mitaji ya nje iliyovutiwa.
Mambo yanaonesha kuwa uwekezaji umekuwa jambo muhimu katika ushirikiano wa sehemu ya Asia ya mashariki. Hivi sasa akiba ya fedha za kigeni ya sehemu ya Asia ya mashariki inafikia dola za kimarekani trilioni 2.4, kiasi hicho kinakaribia theluthi mbili za akiba ya fedha za kigeni duniani. Aidha, Asia ya mashariki ina mitaji mingi sana ya binafsi. Katika kongamano hilo la uwekezaji la Asia ya mashariki naibu spika wa kamati ya kudumu ya bunge la umma la taifa bibi Gu xiulian alisema kuwa ushirikiano wa uwekezaji utakuwa injini mpya kwa ongezeko la uchumi wa Asia ya mashariki.
"Ushirikiano wa uwekezaji utakuwa ongezeko jipya la maendeleo ya uchumi wa Asia ya mashariki. Baadhi ya nchi za Asia ya mashariki ikiwemo China, imekuwa na akiba nyingi ya fedha za kigeni na mitaji mingi isiyotumika ya binafsi. Uwezo wa uwekezaji wa binafsi wa sehemu ya Asia ya mashariki ni mkubwa sana."
Bibi Gu Xiulian alipofanya uchambuzi alisema kuwa kwanza, miundo-mbinu ya baadhi ya nchi za Asia ya mashariki inatakiwa kujengwa kwa haraka, uwekezaji kwa ujenzi wa miundo-mbinu si kama tu inaweza kuinua kiwango cha maendeleo ya uchumi wa nchi hizo, bali pia unaweza kukuza nafasi ya ushirikiano wa uchumi wa nchi za Asia ya mashariki. Pili, sehemu ya Asia ya mashariki kama iko katika makutano ya barabara ya kubadilisha uzalishaji mali, kuinuka kwa kiwango cha uzalishaji kutahimiza ongezeko la uwekezaji, na kupanuka kwa uwekezaji miongoni mwa nchi za sehemu hiyo kutasaidia nchi za Asia ya mashariki kuongeza nguvu ya ushindani ya uchumi. Tatu, maendeleo ya kasi ya uchumi wa kikanda yanataka nchi za sehemu ya Asia ya mashariki kunufaika kwa pamoja kutokana na uendelezaji na matumizi ya raslimali, kutokana na ushirikiano wa uwekezaji, uchumi wa Asia ya mashariki utahuishwa kwa uimara.
Tokea muda mrefu uliopita serikali ya China ilijitahidi kuhimiza ushirikiano wa uwekezaji wa Asia ya mashariki, na ilisaini mikataba ya uwekezaji na nchi nyingi za sehemu hiyo. Miongoni mwa nchi za Asia ya mashariki, Japan ni nchi iliyowekeza kwa kiasi kikubwa nchini China. Mratibu mkuu wa jumuiya ya uhimizaji wa biashara ya kimataifa ya Japan Bw. Yoshio Nakata alipohojiwa na mwandishi wetu wa habari alisema kuwa hivi sasa viwanda na kampuni zilizowekeza nchini China zimezidi elfu 18 na thamani ya uwekezaji imezidi dola za kimarekani bilioni 48. Alisema,
"Hivi sasa kampuni nyingi za Japan zinavutiwa na sera zinazotekelezwa nchi China kuhusu 'ustawishaji wa sehemu ya magharibi', 'ustawishaji wa sehemu ya kaskazini mashariki'. Aidha, sehemu ya kati pia ni sehemu inayovutia kampuni za Japan."
Mbali ya kuvutia uwekezaji wa nchi za Asia ya mashariki, China vilevile inachukua hatua nyingi za kuhimiza viwanda na kampuni zenye hali bora nchini ziende kuwekeza nchi za nje, hususan nchi za Asia ya mashariki zinazopakana na China. Naibu kiongozi wa Benki ya Maendeleo ya China Bw. Yao Zhaomin katika kongamano la uwekezaji alisema kuwa katika miaka ya karibuni benki za China zimeimarisha uungaji mkono kwa viwanda na kampuni za China kuwekeza katika nchi za Asia ya mashariki.
"Benki ya maendeleo ya China inaunga mkono viwanda na kampuni kubwa za China ziwekeze katika miradi ya kilimo, misitu, mali ghafi na miundo-mbinu."
Hadi mwishoni mwa mwezi Mei mwaka huu viwanda na kampuni karibu 1,500 zimewekeza katika Asia ya mashariki ambapo mitaji iliyowekezwa imezidi dola za kimarekani bilioni 3.6 ikichukua sehemu moja kwa sita ya jumla ya uwekezaji wa viwanda vya China katika nchi za nje.
Mwandishi wetu wa habari alipata habari katika kongamano hilo kuwa mbali na Thailand, nchi nyingine za Asia ya mashariki zikiwemo Indonesia, Cambodia hata Japan zinachukua hatua mbalimbali kuvutia viwanda vingi zaidi vya China kwenda kuwekeza nchini mwake.
Idhaa ya kiswahili 2005-07-12
|