Katika miaka ya karibuni, kadiri vyuo vikuu nchini China vinavyowaandikisha wanafunzi wengi zaidi mwaka hadi mwaka, ndivyo idadi ya wanafunzi wanaohitimu inavyoongezeka mwaka. Katika majira ya joto ya mwaka huu wanafunzi zaidi ya milioni 3.3 watahitimu kutoka kwenye vyuo vikuu mbalimbali nchini China, idadi ambayo imeongezeka kwa wanafunzi laki 6. Lakini mahitaji ya jamii ya wahitimu wa vyuo vikuu hayaongezeki kidhahiri, hali ambayo inawaletea shida wanafunzi hao wakati wa kutafuta ajira.
Ili kupanga vizuri kazi ya kuwasaidia wanafunzi wanaohitimu kutoka kwenye vyuo vikuu mwaka huu, wizara ya elimu ya China ilianza kufanya maandalizi tangu majira ya mpukutiko ya mwaka jana. Mkuu wa idara ya wanafunzi ya wizara ya elimu ya China Bi. Li Huiqing alisema:
"Idara za elimu za sehemu mbalimbali na vyuo vikuu mbalimbali vitaendelea kukuza soko la ajira kwa wanafunzi wanaohitimu kutoka kwenye vyuo vikuu, na kuufanya uendeshaji wa soko hilo ufikie vigezo husika; na vitaendelea kutoa huduma nzuri na kuongeza mawasiliano na mashirika na ofisi zinazoajiri wafanyakazi wapya, na kuwajulisha wanafunzi habari za ajira kwa wakati, na pia vitashikilia sera ya kuwahamasisha wanafunzi watafute ajira kwenye sehemu ya magharibi ya China na kwenye sehemu za shina."
Katika siku za karibuni, mwaandishi wetu wa habari alikwenda kwenye Chuo Kikuu cha Lugha cha Beijing ili kufahamu hali hiyo kwa undani zaidi. Mwaka huu wanafunzi zaidi ya 460 wa shahada ya kwanza watahitimu kutoka kwenye Chuo kikuu hicho, idadi hiyo imeongezeka kwa karibu asilimia 20 ikilinganishwa na ile ya mwaka jana.
Mkurugenzi wa idara ya wanafunzi ya chuo kikuu hicho Bw. Huang Yifang alifahamisha kuwa, Chuo kikuu hicho kimeanzisha kituo cha kuwasaidia wanafunzi kutafuta ajira, na kila kitivo kina walimu wanaoshughulikia suala hilo. Alisema, kila ifikapo majira ya joto, wakati wanafunzi wengi wanahitimu, chuo kikuu hicho kitaweka mkazo katika kuwasaidia wanafunzi kupata ajira. Shughuli mbalimbali zitafanyika chuoni, kwa mfano mwaka huu, chuo kikuu hicho kinawasiliana na ofisi na mshirika yanayoajiri wafanyakazi wapya, na kuwaalika wajumbe wa ofisi hizo ili wakutane na wanafunzi watakaohitimu; kukusanya habari kuhusu ajira, na kuziweka kwenye tovuti ya chuo kikuu hicho; kuwahamasisha wanafunzi watafute ajira katika sehemu ya magharibi ya China na kwenye sehemu za shina, ili wapate fursa nyingi zaidi za ajira, mbali na hayo, chuo kikuu hicho kinawaalika wataalamu wa ajira, wajumbe wa ofisi na mashirika yanayoajiri wafanyakazi wapya kutoa risala kwa wanafunzi hao kila baada ya muda fulani.
Yu Maofeng, mwanafunzi wa chuo kikuu hicho, anasomea mambo ya fedha ya kimataifa, kwa muda wa miaka minne alikuwa anafanya vizuri kwenye mitihani, atahitimu mwaka huu, lakini aliamua kuanza kufanya maandalizi tangu mwaka jana. Baada ya kuwasiliana na mwalimu, alichagua ajira atakayotafuta, yaani ajira yenye uhakika na yenye mustakbali mzuri. Alishiriki kwenye usali wa watumishi wa serikali, lakini alishindwa. Baadaye, aliomba ajira kwenye mashirika ya mambo ya fedha, lakini kutokana na ushindani mkali, benki 4 za biashara za kitaifa ikiwemo Benki ya China hazikumpatia fursa ya usaili baada ya kupokea nakala ya sifa zake, na mashirika maarufu kadhaa ya bima na viwanda vikubwa vya ubia nchini China pia vilikataa ombi lake.
Matatizo hayo yamemsikitisha sana Yu Maofeng, wakati huo mwalimu wake alimtia moyo na kumsaidia, ili asiwe na msikitiko. Yu Maofeng alisema:
"Walimu wetu wanatusaidia kwa makini sana, viongozi wa kitivo chetu na mwalimu anayeshughulikia mambo hayo wameongea na kila mwanafunzi, na kuwapatia mapendekezo mwafaka, ambayo ni muhimu sana kwa sisi wanafunzi wakati tunapotafuta ajira."
Kutokana na mapendekezo ya mwalimu, Yu Maofeng alifanya majaribio mengi zaidi, hatimaye alifaulu kwenye usaili wa shirika la habari la Xinhua, na kuajiriwa na shirika hilo.
Kutokana na juhudi za pande mbalimbali, hadi kufikia katikati ya mwezi Juni, zaidi ya asilimia 80 ya wanafunzi watakaohitimu mwaka huu wa chuo kikuu hicho wamepata ajira.
Kama kilivyofanya Chuo Kikuu cha Lugha cha Beijing, zaidi ya asilimia 90 ya vyuo vikuu vimeanzisha vituo vinavyotoa huduma kwa wanafunzi watakaohitimu, na kuanzisha tovuti za ajira, baadhi ya vyuo vikuu vimesaini mikataba ya kunufaishana na viwanda, yaani chuo kiuu kinatoa teknolojia mpya kwa viwanda, na viwanda hivyo vinawaajiri wanafunzi wa chuo kikuu.
Idhaa ya Kiswahili 2005-07-13
|