Enzi ya Tang (618-907) ni kipindi ambacho michoro ya kale ya China ilipata maendeleo ya pande zote. Katika Enzi ya Sui na Enzi ya Tang ulikuwa na muungano wa taifa, hasa katika miaka zaidi ya 100 ya kipindi cha katikati cha Enzi ya Tang, hali ya kisiasa ilikuwa tulivu, nguvu ya nchi ilikuwa kubwa, uchumi ulistawi sana, uhusiano kati ya makabila mbalimbali ulikuwa mzuri, na mawasiliano kati ya China na nchi za nje yalikuwa mengi, hivyo kipindi hicho ni kipindi muhimu sana katika historia ya michoro ya China.
Wakati huo kulikuwa na wachoraji wengi mashuhuri. Kwenye vitabu vya historia kuna kumbukumbu za wachoraji zaidi ya 200. Wachoraji hao walijifunza kutoka kwa utamaduni wa nchi za nje na nje ya sehemu zao nchini, ustadi wao wa kuchora ulikuwa mzuri zaidi, na kulikuwa na aina mbalimbali za michoro. Michoro ya watu ilionesha zaidi maisha halisi. Maendeleo ya uchoraji yaliyopatikana katika Enzi ya Tang yalikuwa makubwa kuliko enzi za kale, na yaliathiri uchoraji wa nchi mbalimbali za Asia Mashariki, hivyo Enzi ya Tang ni kipindi ambacho uchoraji ulistawi sana katika historia ya sanaa ya China.
Michoro ya watu iliyochorwa na Wu Daozi ni yenye mtindo wa kipekee. Michoro yake ya wanawake iliyochorwa kwenye kuta ni mizuri sana. Mtindo wa michoro yake uliathiri michoro ya Japan na Korea.
Kulikuwa na wachoraji wengi hodari katika mji wa Chang'an (mji wa Xi'an wa sasa) ambao ulikuwa mji mkuu wa Enzi ya Tang. Kwa mfano, Yan Lide, Yan Liben waliokuwa kaka na mdogo wake, na Yuchi Bazhina, Yuchi Yiseng waliokuwa baba na mtoto kutoka sehemu ya magharibi ya China walikuwa wachoraji mashuhuri katika kipindi cha mwanzo cha Enzi ya Tang; Zhang Xuan na Zhou Fang walikuwa wachoraji mashuhuri katika kipindi cha katikati cha enzi hiyo; na Lu Lengjia na Sun Wei walikuwa ni wachoraji mashuhuri katika kipindi cha mwisho cha enzi hiyo. Picha ya wanawake wenye maua kwenye nywele zao ambayo ni picha maarufu iliyochorwa na Zhou Fang imeonesha maisha ya raha mustarehe ya wanawake katika kasri la kifalme. Kwenye picha hiyo kuna wanawake watano na mtumishi msichana anayechukua feni mkononi. Sura na mitindo ya nywele za wanawake hao watano zinafanana. Baadhi yao wanacheza na mbwa, wengine wanatazama maua mikononi mwao, au kutembea. Hii imeonesha maisha ya kitulivu katika kasri la kifalme. Han Huang alikuwa mchoraji mwingine mwenye mafanikio makubwa, alikuwa hodari katika kuchora picha za ng'ombe na mbuzi.
Ufundi wa michoro iliyochorwa kwenye kuta ambayo ni aina muhimu ya michoro ya watu katika Enzi ya Tang ulikuwa wa juu. Wachoraji walichora picha mbalimbali nzuri kwa hamu zao. Michoro mingi imeonesha kuwa, michoro ya Enzi za Sui na Tang ilikuwa na uhusiano wa karibu na maisha halisi.
Idhaa ya Kiswahili 2005-07-21
|