Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe imemwaga televisheni kila kata kwa ajili ya kuielimisha jamii kuhusu ugonjwa hatari wa ukimwi.
Akizungumza na Alasiri ofisini kwake, Afisa Mipago wa Wilaya hiyo Bw. Hezekia John Undongole amesema vijana watakuwa wanazunguka kila kijiji na kutoa elimu kuhusu gonjwa hilo, taarifa ambazo zitakuwa zikionyeshwa kwenye televisheni.
Bw Undongole akasema kuwa mbali na televisheni hizo pia wametoa jenereta moja moja kwa kila kata kwa ajili ya kupata umeme.
Amesema halmashauri hiyo imekuwa na ushirikiano mzuri na wadau wa maendeleo katika kuelimisha mashirika yasiyo ya kiserikali yanayojishughulisha na suala la ukimwi.
Amesema wilaya hiyo ina tarafa nne kata 15, vijiji 74 na vitongoji 240.
Kuhusu hali ya maambukizi katika eneo hilo, amesema inaonyesha yameongezeka.
Akaongeza kuwa kutokana na hali hiyo wameamua kutoa elimu ya ukimwi majumbani kwa watu wote ili wale ambao hawajaathirika waweze kujikinga.
|