Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-07-25 15:43:04    
China yaadhimisha miaka 600 tangu Zheng He asafiri baharini

cri

Siku chache zilizopita, kitabu cha "1421, Mwaka wa China Kugundua Dunia" kilichoandikwa na kamanda mstaafu wa jeshi baharini la Uingereza Bw. Bavin Menzies kimetafsiriwa na kuchapishwa kwa Kichina. Kitabu hicho kimechangia shughuli za maadhimisho ya msafiri mkubwa wa Zheng He yanayofanyika hivi sasa nchini China.

Mwaka 2002 kitabu cha "1421, Mwaka wa China Kugundua Dunia" kilipotolewa kilikuwa kinanunuliwa haraka sana. Ndani ya kitabu hicho Bw. Menzies alieleza safasi saba za Zheng He kuizunguka dunia zilizofanyika kabla ya Columbus kwa miongo kadhaa, na mambo ya hatari yaliyomkuta Zheng He alipokuwa katika bara la Amerika ya Kaskazini, Australia na ncha mbili za kusini na kaskazini za dunia. Alama za safari za Zheng He zilizogunduliwa nchini Canada zinavutia sana wataalamu wa mambo ya kale.

Miaka 600 iliyopita, msfiri mkubwa baharini wa China Zheng He, alianza safari na msafara wake wenye merikebu zaidi ya 200 kutoka mji mkuu wa Nanjing, na katika muda wa miaka 28 alisafiri mara saba. Safari zake ziliwahi kumfikisha kwenye visiwa vya kusini mashariki vya Asia, Ghuba ya Bengal, Bahari ya Hindi, Bahari ya Arabia na Bahari Nyekundu.

Zheng He kwa kutumia teknolojia iliyotangulia kabisa katika zama zake alisafiri mbali kwa njia iliyokuwa ya mwanzo kabisa duniani.

Katika safari zake Zheng He aliacha alama za nyayo zake katika nchi zaidi ya 30 za Asia ya Kusini Mashariki, India, nchi za Kiarabu na nchi za mwambao wa Afrika ya Mashariki. Popote alipofika alitangaza sera za urafiki wa China, kutoa zawadi kwa wafalme na raia wa nchi alizofika, kufanya biashara nao na kuwaelimisha bure teknolojia iliyotangulia ya kilimo na ufundi wa kazi za mikono. Kutokana na safari zake za kirafiki, wajumbe wa nchi mbalimbali za Asia na Afrika walikuja kwa wingi nchini China na Wachina walianza kwenda nchi za nje na kuwa watangulizi wa kustawisha visiwa vya Asia ya Kusini Mashariki.

Wachina wanajivujia sana kwa kuwa na msafiri huyo mkubwa. Serikali ya China imeagiza idara maalumu kushughulikia maadhimisho yake katika sehemu mbalimbali, na mada ya maadhimisho yote ni "Uzalendo, Urafiki na Usafiri wa Kisayansi wa Bahari". Mtaalamu wa taasisi ya utafiti wa safari ya Zheng He Bw. Li Erhe anaona kuwa, madhimisho ya miaka 600 ya safari ya Zheng He yana maana kubwa. Alisema, "Safari ya Zheng He ina maana nyingi. Katika mawasiliano ya bahari alifungua njia ya kufikia nchi za Asia na Afrika, ameanzisha njia ya kuunganisha Bahari ya Hindi na Pasifiki na kuingia Atlantiki kupitia Rasi ya Tumaini Jema, amepanua biashara ya hariri ya China na nchi za nje kwa kupitia njia ya bahari. Lakini kitu muhimu zaidi ni kuwa safari ya Zheng He ilikuwa ya urafiki na amani kabisa katika zama za kale."

Ingawa maandishi ya kale kuhusu safari ya Zheng He hayakubaki mengi, lakini watu wanaweza kufikiri jinsi safari ilivyokuwa ngumu. Ni jambo la ushupavu kuwa katika karne ya 15 ambapo sayansi na teknolojia ilikuwa bado nyuma, Zheng He alisafiri mbali katika bahari kubwa akiwa na msafara wake wenye merikebu zaidi ya 200. Hiyo ndiyo sababu Wachina wanajivunia sana safari ya Zheng He. Maonesho ya picha za kamera yanayofanyika hivi sasa mjini Beijing yameonesha vya kutosha ufahari huo.

Maonesho hayo ya picha kwa jina la "Kusafiri Tena kwa Kufuata Njia ya Safari ya Zheng He" ni moja katika shughuli nyingi za maadhimisho. Kwenye maonesho kuna picha zaidi ya mia zilizopigwa na mwandishi mmoja wa kike wa gazeti la alasiri la Mji wa Wuhan Bi. Fan Chunge katika muda wa miaka miwili.

Mwaka 2000 mwandishi huyo alisafiri kwa kufuata njia ya Zheng He, alifika kwenye nchi 18 na aliona alama nyingi kuhusu Zheng He. Alisisimka kwa kuona kuwa katika nchi za Asia ya Kusini Mashariki licha ya kuwa sehemu nyingi zinaitwa kwa jina la Zheng He pia kuna mehekalu yaliyojengwa kwa ajili ya kumkumuka. Bi. Fan Chunge alisema, "Katika nchi za Asia ya Kusini Mashariki kuna majengo mengi ya kumkumbuka Zheng He. Nilipokuwa Thailand niliongozwa mpaka kwenye hekalu moja, niliingia ndani nikaona sanamu kubwa ya Zheng He aliyekaa juu ya yunguyungi lililochongwa. Niliona ajabu kwamba mbona Zheng He amekuwa anaabudiwa kama mungu? Niliambiwa, kwa sababu safari ya Zheng He iliwakilisha nguvu kubwa ya taifa la China katika enzi zile na muhimu ni kuwa safari yake ilikuwa ya urafiki, ya ujasiri na kufanya mambo mema."

Shughuli za maadhimisho ya safari ya Zheng He hazikufanyika mjini Beijing tu bali pia katika miji ya Shanghai na Guangzhou na Nanjing, lakini maonesho yote yana mada moja, nayo ni "Uzalendo, Urafiki na Usafiri wa Kisayansi wa Bahari". Bi. Fan Chunge alisema, "Katika karne ya 15 China ilipokuwa na nguvu kubwa iliweza kuzitendea wema nchi nyingine kwa usawa, watu wa leo wanapaswa kupata mafunzo fulani kutokana na safari ya Zheng He. Kwa hiyo safari ya Zheng He sio tu ni mali ya watu wa China, bali pia ni mali ya ustaarabu wa dunia."

Ndani ya kitabu cha "1421, Mwaka wa China Kugundua Dunia" mwandishi Bw. Menzies alisema, kutokana na uchuguzi wa maandishi ya kale, katika safari zote saba, Zheng He hakuwashambulia wakazi wa sehemu alizopita ila tu alipambana na maharamia mara kadhaa, na hakuna maandishi yoyote yaliyoeleza kuwa safari ya Zheng He ilikuwa na nia mbaya ya kuziteka nchi nyingine. Mwishowe Bw. Menzies alisema, "Safari ya Zheng He ilikuwa tofauti kabisa na safari ya wasafiri wa Magharibi iliyolenga kuziteka na kuzivamia nchi nyingine. Kutokana na hayo Bw. Zheng He alikuwa ni msafiri hodari, mwanadiplomasia, mfanyabiashara wa kimataifa na ni mwakilishi wa amani na utamaduni".

Idhaa ya Kiswahili 2005-07-25