Kampuni ya L'oreal ambayo ilianzishwa miaka karibu 100 iliyopita, ni kampuni ya kwanza kwa ukubwa duniani inayozalisha vipodozi. Kampuni hiyo iliingia China miaka 8 iliyopita. Ingawa si muda mrefu tangu kampuni hiyo iingie nchini China lakini imepata maendeleo makubwa na ya kasi. Hivi sasa tawi lake hilo lililoko China limekuwa la tatu kwa ukubwa miongoni kampuni za vipodozi nchini China, na ongezeko la mauzo lilichukua nafasi ya kwanza likilinganishwa na la matawi yake yaliyoko sehemu mbalimbali duniani. Katika kipindi hiki cha nchi yetu mbioni cha leo nitawafahamisha maendeleo ya kampuni ya L'oreal nchini China.
Ikilinganishwa na kampuni nyingine mashuhuri za kimataifa za vipodozi, L'oreal ni kampuni iliyochelewa kuingia katika soko la China. Mwaka 1996 Loreal iliwekeza dola za kimarekani milioni 50 kujenga kiwanda chenye eneo la mita za mraba karibu laki 1 nchini China. Baada ya mwaka mmoja Loreal katika mji wa Shanghai ilianzisha makao makuu ya tawi lake nchini China. Toka mwanzoni kabisa L'oreal iliwachukulia wanawake na wasichana milioni 100 hivi wa miji ya China kuwa ni wateja wake na kuzalisha vipodozi vya aina mbalimbali kulingana na uwezo wao wa kiuchumi, na kuweka kaunta maalumu kwenye maduka makubwa ya China.
Uamuzi wa L'oreal kuhusu uzalishaji wake na mtindo wa mauzo umefanikiwa katika soko la China, mkurugenzi mkuu wa L'oreal nchini China Bw. Paolo Gasparrini ameridhika sana na maendeleo ya L'oreal, alisema,
"Naona bidhaa zetu zinauzwa vizuri sana nchini China na maendeleo ya kampuni yetu yatakuwa mazuri, na bidhaa zetu zinapendwa na watu wa China."
Hivi sasa bidhaa za kampuni ya L'oreal zinauzwa katika miji zaidi ya 500 ya China. Baada ya kuchukua nafasi ya vipodozi vya kiwango cha juu ya soko la China, L'oreal inalenga shabaha katika soko la vipodozi la kiwango cha wastani na cha chini la China. Baada ya kununua kampuni mbili za vipodozi za China, uwezo wa uzalishaji wa kampuni ya L'oreal nchini China umeongezeka mara tatu kuliko zamani.
Pato kutokana na mauzo la L'oreal nchini China mwaka 2004 lilikaribia Yuan bilioni 3 likiwa ni ongezeko la 99% kuliko zamani. Mkurugenzi mkuu wa Loreal nchini China Bw. Paolo alisema,
"Ongezeko tulilopata nchini China ni muhimu sana kwa kampuni ya Loreal, mauzo yetu ya mwaka jana yalikaribia Yuan bilioni 3, ingawa kiasi hicho ni kidogo kikilinganishwa na Euro bilioni 14.5 ambayo ni jumla ya mapato ya L'oreal katika dunia nzima, lakini ni muhimu sana kutokana na mchango huo kwa kampuni ya Loreal".
Tawi la L'oreal nchini China linajitahidi kutumia watu wa China katika shughuli za kampuni. Hivi sasa tawi hilo licha ya kuwa na wafanyakazi wageni zaidi ya kumi, ina wafanyakazi wachina 3,000, hata katika uongozi wa ngazi ya juu kabisa kuna wasimamizi wa China. Hivi sasa bidhaa zinazozalishwa na tawi la kampuni ya Loreal nchini China zinauzwa nchini Japan, Korea ya Kusini na nchi za Umoja wa Asia ya Kusini Mashariki.
Katika kipindi cha mwanzoni, wafanyakazi wa kampuni ya L'oreal karibu wote walikuwa wanawake, watu wanaona kuwa hiyo ni kampuni ya vipodozi, huenda kazi zake haziwafai wanaume. Tawi la kampuni ya L'oreal nchini China lilitoa matangazo mengi ya kuwapa moyo wanaume kufanya kazi katika kampuni hiyo. Hivi sasa kiasi cha wafanyakazi wa kike na kiume wa tawi hilo karibu ni nusu kwa nusu. Meneja wa uhusiano na nje wa tawi hilo Bw. Zhou Genliang alisema,
"Niliingia kwenye kampuni hiyo miaka zaidi ya miwili iliyopita, ninaona kuwa kampuni hiyo inanivutia, inakuwezesha kupata mengi usiyoyatarajia. L'oreal inakaribisha watu wanaotoka kwenye mazingira ya aina mbalimbali, inapima watu kutokana na mahitaji na uwezo wake wala siyo mazingira na kiwango cha elimu yake. L'oreal inakubali kukabiliana na hali yenye kiwango fulani cha hatari ilimradi utoe pendekezo, ingawa huna uzoefu, L'oreal inakupa nafasi ya kujaribu, huu ni umaalumu muhimu wa utamaduni wa kampuni."
Bw. Zhou alisema kuwa ili kuwawezesha wafanyakazi wake wafanye kazi vizuri, kampuni ya L'oreal imebuni mafunzo ya kazi yanayoendana kabisa na uzalishaji wa kampuni na kuchagua viongozi wa baadaye wa kampuni.
Takwimu zinaonesha kuwa hivi sasa mauzo ya vipodozi ya soko la China ni kiasi cha Yuan bilioni 5 kwa mwaka, tena yanaongezeka kwa 20% kwa mwaka. Soko la vipodozi la China litazidi lile la Japan katika muda mfupi ujao, na kuwa soko la kwanza kwa ukubwa barani Asia. Hivi sasa kampuni ya L'oreal imewekeza Euro milioni 6 ili kuanzisha kituo cha utafiti duniani nchini China, ambacho kitafanya utafiti kuhusu ngozi na nywele za wachina ili kukuza soko lake nchini China.
Idhaa ya Kiswahili 2005-07-26
|