Kadiri jamii inavyoendelea na kubadilika, ndivyo habari na ujuzi mpya zinavyoibuka kila siku, hali ambayo ni changamoto kwa walimu, na kuwafanya walazimike kujipatia sifa ya ngazi ya juu zaidi. Ujuzi waliokuwa nao kabla ya kuanza kazi ya ualimu hautoshi, hivyo wanapaswa kuendelea kujifunza ili waendane na maendeleo ya jamii. Kutokana na hali hiyo, nchi mbalimbali zinazingatia kazi ya kuwaandaa walimu, hasa walimu wa shule za msingi na sekondari, kwani elimu ya shule za msingi na sekondari ni ya muhimu zaidi.
Ofisa wa wizara ya elimu ya China Bw. Tang Jingwei alipofahamisha kazi hiyo ya China alisema:
"Katika miaka ya karibuni, tumefahamu siku hadi siku kuwa, kiwango cha elimu kinategemea sifa za walimu, hivyo China inapokuza elimu inazingatia sana kuwaongezea ujuzi walimu."
Hivi sasa, China imeanzisha utaratibu wa kuwaongezea ujuzi walimu wa shule za msingi na sekondari, na Sheria ya walimu ya China inaainisha kuwa ni haki na wajibu wa walimu kushiriki kwenye mafunzo, na walimu wote wa shule za msingi na sekondari wanatakiwa kupewa mafunzo kwa muda usiopungua saa 240 ndani ya kila kipindi cha miaka mitano. Mafunzo hayo ni kuwahamasisha walimu wapende shughuli za ualimu, kuinua kiwango chao cha ualimu, na kuinua uwezo wao wa kufundisha na kuwasaidia kuboresha njia za kufundisha.
Hivi sasa, China ina walimu wa shule za msingi na sekondari zaidi ya milioni 10 kwenye shule za msingi na sekondari, kazi ya kuwaongezea ujuzi inaelekezwa na vyuo vikuu 6 vya ualimu vilivyoko katika sehemu mbalimbali nchini China, na kutekelezwa na idara husika za ngazi za mikoa na wilaya, na gharama za kazi hiyo zinalipwa na serikali za ngazi mbalimbali. Walimu wanafundishwa ana kwa ana, au kupitia radio, televisheni na internet, na walimu wa vijijini, ambao kiwango chao ni cha chini kidogo, wanazingatiwa zaidi.
Wilaya ya Miyun ni wilaya ya kilimo iliyoko kwenye kitongoji cha mji wa Beijing, ina shule 90 za msingi na sekondari zenye walimu zaidi ya elfu 4. Kwa kuwa wilaya hiyo iko kwenye sehemu ya milimani, na hali ya mawasiliano ni duni, hivyo kiwango chake cha elimu ni cha chini. Ili kubadilisha hali hiyo, katika miaka ya karibuni, idara ya elimu ya wilaya hiyo inazingatia sana kazi ya kuwaongezea ujuzi walimu. Anayeshughulikia kituo cha kuwaongezea ujuzi walimu cha wilaya hiyo Bw. Ma Wenzhao alisema:
"Kiwango cha elimu ya lazima kinategemea kiwango cha walimu na juhudi za kuwaongezea ujuzi walimu, hivyo idara ya elimu ya mji wa Beijing na wilaya yetu inafanya juhudi kubwa."
Bw. Ma alifahamisha kuwa, kwa mujibu wa ratiba ya vipindi, baada ya mapumziko ya majira ya joto ya mwaka huu, shule za msingi za wilaya hiyo zitaanza kufundisha somo la kiingereza kuanzia darasa la kwanza, mpango huo unalifanya tatizo la upungufu wa walimu wa kiingereza lijitokeze zaidi. Ili kutatua tatizo hilo, wilaya hiyo inaimarisha kazi ya kuwaandaa walimu wa kiingereza, huku ikiwataka baadhi ya walimu wa masomo mengine wanaojua kiingereza wafundishe kiingereza. Hivi sasa, walimu zaidi ya 100 wa kiingereza wa wilaya hiyo wanashiriki kwenye mafunzo ya aina mbalimbali, na wamepata maendeleo makubwa katika kuongea na kujua kiingereza.
Bw. Han Chunhe, ambaye ni mwalimu wa kiingereza katika shule ya sekondari ya Mujiayu ya wilaya hiyo, amefanya kazi ya ualimu mwalimu kwa miaka 20, na ana uzoefu mkubwa wa kufundisha, lakini alisema, walimu wanapaswa kujifunza zaidi ili wawe na sifa zinzolingana na vitabu vya kiada vinavyotumika hivi sasa na sifa zinzotakiwa kwa kazi ya ualimu. Alisema, anapenda kutumia fursa hii ya kuongezewa ujuzi kujifunza zaidi, kuinua kiwango chake cha kiingereza na kujifunza njia nyingi zaidi na za kisasa zaidi za kufundisha.
Bi. Wang Hailian ni mwalimu wa shule ya msingi ya Shilipu ya wilaya hiyo, alisomea kompyuta kwenye chuo kikuu, lakini hivi sasa anawafundisha vipindi 7 vya kiingereza. Alisema, ingawa anapenda kiingereza, na amesomea kiingereza kwa muda wa zaidi ya miaka 10, lakini anapofundisha kiingereza anaona kuwa kiwango chake cha kiingereza hakitoshi. Hivi sasa, anasafiri umbali wa zaidi ya kilomita 200 kushiriki kwenye darasa moja linalofanyika mjini Beijing kila baada ya siku saba, pia anaendelea na kazi yake ya kila siku, anajisikia uchovu, lakini anaona kuwa hilo ni jambo linalostahili.
"Somo hilo ni la lazima kwangu, tumefaidika na somo hilo katika kuinua kiwango chetu cha kufundisha, na uwezo wetu wa kuongea kiingereza."
Idhaa ya Kiswahili 2005-07-27
|