Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-08-09 15:59:45    
Barua 0807

cri

        Leo kama kawaida, tunawaletea barua kutoka kwa wasikilizaji wetu. Bw. Kaziro Dutwa wa sanduku la posta 209 Songea Ruvuma Tanzania ametuletea barua akisema kuwa, anafarijika sana kupata fursa hii kutuandikia waraka huu akitumai kuwa sisi hatujambo na tunaendelea kuchapa kazi kama kawaida, kama ndivyo basi hii ni furaha kubwa kwake. Na yeye anasema hali yake ni nzuri.

Tunamshukuru sana Bw. Kaziro Dutwa kwa salamu zake kwetu sisi, sisi sote hapa Beijing hatujambo, na tunaendelea kuchapa kazi zetu za kila siku kama kawaida.

Bwana Dutwa anasema katikati ya mwezi Mei mwaka huu ilikuwa ni siku ya furaha kubwa kwake; ilikuwa ni kama siku ya kupata mtoto wa kwanza wa kuzaliwa, baada ya matarajio yenye mashaka na ghafla bin vuu akazaliwa mtoto mzuri wa kupendeza, kufurahisha na kumpa faraja kila mtu! Mtoto huyu si mwingine bali ni jarida jipya adhimu la "Daraja la Urafiki" lililoanzishwa na Radio China Kimataifa likitolewa kwa lugha ya Kiswahili, na kwa sehemu kubwa kubeba mawazo na michango mbali mbali iliyotolewa na wasikilizaji, hakika hii ni tunu kwa waswahili na wasikilizaji wote wa idhaa ya Kiswahili ya Radio China Kimataifa.

Jarida hili ambalo lilitolewa tarehe 20/4/2005 lina sura maridhawa kama ifuatavyo: Kwenye kilemba kuna saa na mita za matangazo ili kuwawezesha wasikilizaji kuipata kiurahisi na kiuhakika idhaa ya Kiswahili ya Radio China Kimataifa!

Usoni pamewekwa hadharani risala ya Mkuu wa CRI aliyoitoa kwenye mwaka mpya wa 2005; Ama risala hiyo imebeba uzito wa dhamira nzima ya kuwathamini na kuwaenzi wasikilizaji wake, kwani katika risala hiyo Bw. Wang Gengnian amenukuu baadhi ya mawazo na michango ya wasikilizaji ili kutia uzito hoja zake, hakika hii inadhihirisha bayana kuwa michango na mawazo ya wasikilizaji huchukuliwa kwa uzito unaostahili kulingana mantiki.

Mkuu huyu amebainisha kuwa mwaka 2004 Radio China kimataifa ilipokea barua zaidi ya milioni 18, toka nchi na sehemu 160 Duniani! Hii inaonyesha shughuli pevu inayofanywa na wahariri na watangazaji wa Radio China kimataifa kuzipitia barua moja baada ya nyingine, huku wakitafuta habari za kutangaza, kuingiza kwenye tovuti, kuandika majarida na mengine mengi yasiyohesabika, hakika mnastahili sifa kubwa na poleni sana. Baada ya Risala ya mwaka mpya ya Mkuu wa Radio China Kimataifa ulifuata utangulizi unaoonesha furaha na matumaini mapya ya mabadiliko ya jarida hili kwa siku za usoni haya ni matumaini mema kwani ni kawaida mtoto akizaliwa, ni lazima akue na kupata mabadiliko mbalimbali kila siku. Vile vile kuna picha mbili za timu za watangazaji wa Idhaa ya Kiswahili, yaani timu ya zamani na timu mpya bila shaka.

Kwenye ukurasa wa pili kuna barua mbalimbali za wasikilizaji, na pia kuna mashairi na picha tatu moja ikiwa ni ya Bw. Mogire Machuki alipotembelewa na ugeni mzito wa CRI akiwemo Mama Chen akiwa amemshika mmoja kati ya watoto mapacha wa Bw. Mogire huu ni upendo ulioje!

Ama kwenye ukurasa wa tatu uhondo unazidi kunoga kwani kuna Maswali na majibu ambapo maswali yamejibiwa kwa kina na kwa ufasaha pia kuna picha mojawapo ikiwaonesha wasikilizaji maarufu watatu: Wa kwanza kabisa kushoto ni Bw. Franz Manko Ngogo na wa tatu kulia ni Mogire Machuki, picha hii bila shaka hata Bw Msabah Mbarouk aliizungumzia na alisema kuwa alishindwa kung'amua kuwa yupi ni Bw Ngogo. Anasema kwa kweli hili lilikuwa ni jambo la kusikitisha, kwani tulipoweka picha hiyo tulisahau kueleza wazi nani ni Ngogo,.

Ukurasa wa mwisho kuna uchambuzi wa aina 12 za wanyama na mwaka wa kuku na inaelezwa kuwa kwa Wachina kuku ana sifa 5 na hapa zimeelezwa moja hadi nyingine kwa kweli inafurahisha sana. Kwa upande wa makulaji kuna somo la mapishi ya chakula kitamu cha Kichina, bila shaka hapa ni kufaidi tu. Pia kuna safari ya kwenda Hangzhou kuonja chai ya Longjing; bila shaka hata Bw. Wambwa alipata fursa ya kuonja chai hii maarufu alipozuru China. Anasema analazimika kutia nanga hapa, japo kuwa bado kuna mengi ya kueleza, lakini kubwa la mwisho ni pongezi zake na shukrani.

Tunamshukuru sana Bwana Dutwa kwa maelezo yake mazuri juu ya jarida letu dogo la Daraja la urafiki. Ni matumaini yetu kuwa, ataendelea kutuletea maoni na mapendekezo mazuri ambayo tunaweza kuyachapisha kwenye jarida hilo, ambayo yanaweza kuchangia kuboresha jarida hilo.

Msikilizaji wetu Anari Justine wa shule ya sekondari Ikonge sanduku la posta 2424, Kisii, Kenya anasema katika barua yake kuwa, ana furaha kubwa kwa kutuandikia barua hii. Kwanza anatusalimu watangazaji na wasikilizaji wa idhaa ya kiswahili ya Radio China kimataifa. Anatoa shukrani zake za dhati kwa zawadi ndogo tulizomtumia kwa njia ya posta. Pamoja na shukrani hizo, anatuomba kwa unyenyekevu kama tukitembelea Kenya tusikose kuwatembelea hapo Kisii Kenya.

Anasema ingawa yeye ni mwanafunzi wa shule ya sekondari anatutegea sikio kila mara, kama akitukosa katika habari za saa kumi na moja, tena anatusililiza kupitia masafa mafupi na kutupata kwa habari na vipindi vinginevyo vya kila siku. Hata jamii yao nzima haiwezi kutukosa katika kututegea. Anatuomba hata siku moja tumtembelee hapo Kisii ili tujionee nyumbani kwake, baba yake ni mchoraji wa vitu vingi, kwa mfano, wanyama pori, kama vile simba, chui, ndovu na vinginevyo.

Pia anasema yeye na wenzake ambao ni wanafunzi ni wasikilizaji wazuri wa idhaa ya kiswahili ya Radio China Kimataifa, Anasema hata wanafunzi wenzake ambao wako ishirini na wawili na majina yao atatupatia hapa, na wanataka tuwatumie vitabu vya Jifunze Kichina na bahasha za kututumia barua. Majina ya wasikilizaji: Abinar, John, Moseti, Ayole, Makori, Obed, Nyonga, Mose, Anyona, Nyaanga, Zipporah, Doricah, Misiani, Bosibori, Vinic, Naomi, Kerubo, Dinah, Joicy, Mokeira, Joel, anasema tafadhali tuwatumie hivyo vitabu na bahasha.

Tunamshukuru sana Anari Justine kwa barua yake na mwaliko wake wa dhati kuwatembelea. Tukipata nafasi hakika tutakwenda Kisii tena, mkutano na wasikilizaji wetu huko Kisii bado tunaukumbuka barabara, tunaona kuwa wasikilizaji wetu wote ni wenye uchangamfu na ukarimu, tunawashukuru kwa dhati. Pia nasi tunakwambia Bw Anari usisahau kuwaambia wenzako wote, kuwa tutafanya kila tuwezalo kuwatumia magazeti na bahasha, ni matumaini yetu kuwa mtaendelea kusikiliza vipindi vyetu na kutembelea tovuti yetu, na kutoa maoni na mapendekezo yenu kuhusu matangazo yetu.

Idhaa ya kiswahili 2005-08-09