Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-08-18 20:39:43    
Maendeleo ya utalii yabadilisha maisha ya wakulima wa Zhangjiajie

cri

Zhangjiajie ni sehemu maarufu yenye vivutio vya utalii nchini China, ambayo iko katika sehemu ya kaskazini magharibi mwa mkoa wa Hunan, katikati ya China. Mandhari yake nzuri ya kimaumbile inawavutia watalii wengi wa nchini na ng'ambo, sehemu ya vivutio vya utalii ya Wulingyuan iliyoundwa na sehemu ya Zhangjiajie na sehemu nyingine mbili zenye mandhari ya kimaumbile imeorodheshwa kwenye urithi wa kimaumbile duniani na shirika la elimu, sayansi na utamaduni la Umoja wa Mataifa UNESCO. Tangu miaka ya 90 ya karne iliyopita, idadi ya watu wanaotembelea Zhangjiajie inaongezeka siku hadi siku, hivi sasa barabara za kasi, reli na ndege za abiria kila siku zinawafikisha watalii wengi kutoka sehemu mbalimbali duniani kutembelea huko.

Zamani, uchumi wa sehemu ya Zhangjiajie ulikuwa nyuma sana, maisha ya wakazi wa huko yalikuwa siyo mazuri. Lakini baada ya kuendeleza shughuli za utalii maisha ya wakulima yameboreshwa.

Kila siku kunapopambazuka, mkulima Lu Tangyou mwenye umri wa miaka 53 anaenda kwenye sehemu ya utalii ya Huangshizhai ya Zhangjiajie, kupasua mawe kuwa makokoto kwa kujenga barabara. Bwana Lu anaishi katika kijiji cha Yuliang karibu na Huangshizhai. Alisema kuwa, karibu na kijiji chake kuna milima mingi ya mawe, eneo linalofaa kwa kilimo cha nafaka ni dogo sana. Kijiji chake kina watu zaidi ya 1000, zamani maisha yao yalitegemea tu kilimo cha mahindi na kupewa msaada wa chakula na serikali, hivyo waliishi maisha duni sana.

Tangu shughuli za utalii zianze kustawi katika sehemu ya Zhangjiajie, miundombinu mingi ya utalii imejengwa ikiwa ni pamoja na barabara na hoteli, na miti mingi pia imepandwa. Bwana Lu Tangyou anayejua kufanya shughuli za ujenzi alikwenda mjini na sehemu ya utalii kufanya shughuli za kujenga barabara na madaraja, wakulima wengine wa kijiji chake pia wanajihusisha na kazi zinazohusiana na utalii. Bw. Lu anasema:

"Baadhi yao wanapanda miti, wengine wanapanda maua, na wengine wanafanya kazi za ujenzi au kufanya kazi za vibarua." Hivi sasa wastani ya pato la mwaka la wanavijiji wa kijiji cha Yuliang umeongezeka mara kumi kuliko zamani, na familia nyingi zimeweza kujenga nyumba mpya.

Zamani kutokana na hali duni ya kiuchumi, wakulima wengi wa sehemu hiyo walikwenda nje kutafuta kazi za vibarua, lakini hivi sasa kutokana na maendeleo ya shughuli za utalii, shughuli za utoaji huduma zinaendelea siku hadi siku, na zimeleta nafasi nyingi za ajira. Hivyo wanakijiji wengi waliofanya kazi za vibarua nje wamerudi nyumbani. Mtoto mkubwa wa Mzee Lu zamani alifanya kazi ya kibarua katika sehemu ya pwani, sasa amerudi nyumbani na kufanya kazi katika hoteli moja.

Katika miaka ya karibuni, sehemu ya Zhangjiajie imejenga majumba kadhaa za makumbusho zinazoonesha utamaduni wa mila na desturi za kienyeji. Miongoni mwa majumba hayo, jumba la makumbusho la Xiuhuashan linaendeshwa na mtu binafsi wa kabila la watujia, ambalo licha ya kuonesha vifaa vya kimaisha na vyombo vya kilimo vyenye uwakilishi vya kabila la watujia, pia linaonesha sanaa za michezo ya kienyeji, kutengeneza na kuuza michoro ya mchanga na sanaa za mikono. Kila siku jumba hilo linawavutia watalii wengi. Na kati ya watumishi wake 40, wengi ni wakulima wenyeji, michoro ya mchanga na sanaa za mikono zilizooneshwa kwenye jumba hilo pia zinatengenezwa na wakulima hao.

Mfanyakazi wa idara ya utalii ya sehemu ya Zhangjiajie Bwana Guo Tiejun alisema kuwa, maendeleo ya utalii pia yamewanufaisha wakulima wa kienyeji katika maisha yao. Anasema:

"Wakulima wamebadilisha mawazo yao. Kwa mfano, katika sehemu za utalii, hata mabibi na watoto wengi wanaweza kuzungumza kidogo kwa lugha ya Kikorea, hayo ni mabadiliko makubwa kwa wenyeji wa huko."

Watalii wa Korea ya Kusini wanapenda sana kutembelea Zhangjiajie, hivyo wakulima wengi waishio katika sehemu za utalii wamejifunza lugha ya Kikorea ili waweze kuwasalimia watalii wa Korea ya Kusini na kukubaliana nao bei za bidhaa. Kwenye kiwanja kidogo chini ya mlima mmoja, kuna maduka mengi ya kuuzia sanaa za mikono na mikahawa iliyoendeshwa na wakulima wenyeji. Mwendeshaji wa duka Bwana Wang Maosheng alisema kuwa, watalii kutoka Korea ya Kusini wanapenda kununua sanaa za mikono kutoka kwenye duka lake, hivyo yeye amejifunza lugha ya Kikorea katika shughuli zake za biashara.

Idhaa ya Kiswahili 2005-08-18