Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-08-23 16:52:32    
Barua 0821

cri

       Msikilizaji wetu George Wanabwa wa sanduku la posta 2287, Bungoma Kenya ametuletea barua kwanza akitaka kuishukuru idhaa ya Kiswahili ya Radio China Kimataifa kwa kupokea tuzo maalum katika mashindano ya chemsha bongo mwaka 2004 hadi 2005. Vile vile anampongeza Bwana Xaviel Tellya Wambwa kwa kufuatilia kwa makini vipindi vyetu vya idhaa hii kila siku.

Pia anataka kuwapongeza wasikilizaji walipata nafasi ya kwanza, ya pili na ya tatu, na kuwaambia wasife moyo na wafanye bidii zaidi wakitumai kuwa siku moja mungu atawajalia. Ombi lake kwa kila mtangazaji na msikilizaji anaposoma au kusikia barua hii, ajipongeze kwa kusema, "Hoye! Hoye! Hoye! CRI imara na inedelee kuangaza".

Anasema wao huko Bungoma nchini Kenya wameunda kikundi kwa jina la "Nalondo CRI", kwa kupitia muungano huu waliweza kuandaa tafrija ili washerehekee tuzo yao maalum nchini China tarehe 25 Juni mwaka huu chini ya uongozi wa Bwana Xaviel L.Telly Wambwa. Katika hiyo sherehe iliyoanza saa kumi kamili ilihudhuriwa na wasikilizaji kumi na wawili, watatu hawakufika kutokana na sababu maalum, maombi yalitoka kwa Askofu Sypriano Simiyu kutoka Lurende.

Baadaye walipokaa walisomewa maneno matakatifu kutoka kwa Bwana John Wanjala Injini, maneno hayo yaliwahimiza wasikilizaji wawe na upendo kwani upendo huvumilia, hauhesabu mabaya, hufurahia ukweli na hautafutii mwingine mabaya. Aliwaambia kuwa kama wasikilizaji wakizingatia hayo basi kikundi cha CRI Nalondo kitaendelea kudumu na kuboreshwa zaidi.

Katika kipindi cha maoni na mapendekezo Bwana Martin Nyongesa aliuliza kuhusu utendaji wa kazi wa Idhaa ya kiswahili ya Radio China Kimataifa. Bwana Wambwa aliyeshuhudia alijibu, "kama kusingekuwa na bidii, katika kujitolea kufanya kazi bila kuchoka, wasingeweza kupata matangazo yao kwa njia nzuri kama wanavyoyapata sasa. Tena wanafanyakazi hadi usiku. Hawana nafasi hata kuongea." Hapo aliona wasikilizaji wakitikisa vichwa kama ishara ya kutosheka na jinsi Bwana Wambwa alivyojibu swali hilo. Na Bwana Rudolf Churchill Konje alimwuliza Bw Wambwa: "alionaje hatua kubwa sana katika maendeleo. Hasa majengo ya kupendeza, barabara safi na pia kuhusu ujuzi mwingi katika viwanda. Bw Wambwa alijibu watu wa China ni wakarimu sana, wenye nidhamu, hasa maofisa ofisini mwao na maaskari katika kazi zao, tena hawana maringo," hapo alisikia mbung! Mbung! waligonga meza kufurahia jibu hilo.

Naye Bi Doroth Sitawa Wambwa alimwuliza Bwana Wambwa: "Ulipotoka hapa ukienda China ulikuwa mrefu, lakini sasa umekuwa mfupi, tena ngozi yako imekuwa laini na nyororo, kwanini? Swali hilo liliwachekesha na kufurahisha mno, Bwana Wambwa alicheka kidogo halafu akasema, kule nchini China mtindo wa kupika vyakula ni tofauti sana na kwetu, tena vina ladha nzuri na vinaandaliwa kwa wingi. Hiyo ndiyo maana afya yangu inapendeza sana. Bibi Magreate Wanjala Injini aliuliza kuwa :"sasa bibi mzuri ni nani?"

Kufikia hicho Kiwango kila mmoja alikuwa amejaa furaha isiyo kifani wakisema Bibi mzuri ni Doroth, Idhaa ya Kiswahili, kila mmoja alisema vile alivyopenda. Wakati huo huo walikuwa wanaelekea nje ili waweze kupeperusha ndege yao iliyoundwa kutokana na makaratasi ya kawaida. Hiyo ndege ilizawadiwa na upepo kupaa angani. Bibi Sylvia Nakhumicha Simiyu akiwa rubani wao alikuwa tayari kuipeperusha. Wakati huo kila mtu alikuwa ametulia tuli kama maji ya mtungini. Ndege yao ilipaa angani polepole kwa umbali usiopungua mita 15. Ndege yao ilipoanza kutua ilitua katika Shamba la Bwana Xaviel L.Telly Wambwa, kisha kuchukua dakika 7.11, kikundi chao cha CRI Nalondo kilishangilia kwa shangwe, vigelegele na nderemo wakisema Bwana wao Yesu Kristo atukuzwe kwa kuwasaidia katika safari hii.

Tunamshukuru Bwana George Wanabwa kwa barua yake iliyotuelezea kuhusu hali ya kumkaribisha, kumpongeza kwa furaha na kumwuliza maswali Bwana Telly Wambwa aliyepata tuzo maalum katika shindano la chemsha bongo la mwaka jana, na kuja kuitembelea China.

Msikilizaji wetu Isaac Kulwa wa sanduku la posta 69041, Dar es Salaam Tanzania anasema katika barua yake kuwa, kwa mara nyingine anapenda kutumia nafasi hii kutusalimu, yeye hajambo akitumai kuwa na sisi hatujambo na tunaendelea na kazi zetu kama kawaida. Ila anatuomba tuendelee kuwapatia huduma nzuri wasikilizaji wetu, anapenda kutuhakikishia kuwa wataendelea kuwa bega kwa bega na sisi ili kuweza kuiboresha idhaa ya Kiswahili ya Radio China kimataifa.

Wito wake ni kuwa wasikilizaji wote wa idhaa ya Kiswahili ya Radio China kimataifa kutoka kila kona ya dunia ni kwamba kila mwenye ndoto za maendeleo ili kuboresha matangazo ya idhaa ya Kiswahili atoe maoni, na kila aliye na chochote akitoe kupitia jarida safi liitwalo Daraja la urafiki.

Kusema kweli kazi imekwisha, kama wajuavyo daraja ni mkombozi wa maendeleo bila daraja hakuna maendeleo, kwa hiyo nao kutokana na taswira hii ya Daraja la urafiki, yeye binafsi anaona kama kazi imekwisha, kwanza moja kwa moja kama endapo barua yake itachapwa kwenye jarida hilo anaweza kupata marafiki mbalimbali kutoka pande zote za dunia, kama ilivyo sasa Radio China kimataifa ambaye ndiye rafiki yake mkuu. Mwisho anapenda kutoa hongera! Kwa aliyetoa wazo kuhusu kuwepo kwa Daraja la Urafiki.

Tunamshukuru Bwana Isaac Kulwa kwa maelezo yake juu ya jarida dogo la Daraja la urafiki linalochapishwa na idhaa ya kiswahili ya Radio China kimataifa, tumetiwa moyo sana wasikilizaji wetu wengi wanalipenda jarida hilo na kulithamini sana, tutafanya juhudi kuliwezesha jarida hilo liwafurahishe zaidi wasikilizaji wetu.

Msikilizaji wetu Yaredi Mkama wa sanduku la posta 30 kupitia kwa Naomi Stephano Magu Mwanza Tanzania, ametuletea barua akisema kuwa, anazituma salamu zake zilizojaa wingi wa furaha zitufikie popote tulipo, anashukuru kama sisi ni wazima Anasema lengo la barua yake ni kutaka kutuambia kuwa anapenda kuwa msikilizaji wa Radio China kimataifa, yeye ni mwanafunzi wa darasa la 6 katika shule ya msingi Nyalikungu, umri wake ni miaka 14 kwa sasa anapenda kusikiliza vyombo mbalimbali vya habari hasa Radio China kimataifa. Alikuwa mtu mwenye furaha sana pale aliposikia matangazo ya Radio China kimataifa.

Anasema Radio China kimataifa ni mwanga wa ulimwengu mzima kwa sababu inatoa vipindi motomoto, yeye anatoa shukrani kwa watangazaji wa Radio China kimataifa na wasikilizaji wote wa Radio China kimataifa, na anaitakia izidi kung'ara katika dunia nzima. Anasema huko Mwanza wanaipata vizuri kabisa Radio China Kimataifa.

Tunamkaribisha kwa mikono miwili Bw Yaredi Mkama kuwa msikilizaji wetu, ni matumaini yetu kuwa atakapokuwa mwanachama wetu ataendelea kusikiliza vipindi vyetu kwa makini na kutuletea maoni na mapendekezo. karibu sana.

Bwana Mogire Machuki wa kijiji cha Bogeka sanduku la posta 646 Kisii Kenya ametuletea barua akisema kuwa, yeye ni mzima wa afya na ana furaha kwa kuwa anaendelea kuburudika na matangazo yetu ya masafa mafupi. Ni muda tangu awasiliane nasi na kwa kweli mambo kadha wa kadha yametendeka hususani katika sekta ya utangazaji. Baada ya kurejea Kisii alishangaa kidogo, kwani kumechipuka vituo karibu kumi vya FM, kutokana na kuja kwa ushindani huo angependekeza Radio China kimataifa nayo ianzishe mipango ya kufungua kituo cha FM kitakachosikika kote Afrika mashariki na kati, kama njia moja ya kulitangaza taifa la China kwa waafrika.

Anapongeza hali ya usikivu wa vipindi vyetu kwenye 11600 kHz, ila kwenye vipimo vya 15125 kHz mara nyingi usikivu hauridhishi. Siri ya kufurahia matangazo ya Radio China kimataifa ni umilikaji wa radio nzuri na ya kisasa. Anatutakia kazi njema na maisha marefu na tuendelee kuwatangazia wasikilizaji kutoka Beijing China.

Tunamshukuru sana Bwana Mogire Machuki ambaye ameeleza wasiwasi wake juu ya matangazo yetu katika Afrika ya mashariki, kabla ya hapo kweli tulikuwa na wasiwasi pia, lakini kutokana na ushirikiano kati ya Radio China kimataifa na shirika la utangazaji la Kenya KBC, matangazo yetu yanayopitia KBC yataongezwa muda kuanzia tarehe 1 Septemba, na matangazo yetu kwenye masafa mafupi pia yataongezwa muda kuanzia tarehe 1 Septemba, na huenda tutakuwa na ushirikiano na Sauti ya Zanzibar Tanzania siku zijazo, na tumeambiwa kuwa serikali ya Kenya imekubali Radio China kimataifa ijenge kituo chake cha FM, tuna imani kuwa chini ya ushirikiano kati ya China na nchi za Afrika, Radio China kimataifa itaendelea vizuri na kuvutia wasikilizaji wengi.

Idhaa ya Kiswahili 2005-08-23