Mkoa unaojiendesha wa Tibet wenye eneo la kilomita za mraba milioni 1.2 una wafugaji wanaohamahama zaidi ya milioni 1 wa kabila la watibet, ambao wanatafuta sehemu yenye maji na malisho ya mifugo yao, lazima wapo wafugaji, maisha hayo pamoja na hali duni ya mawasiliano iliwaletea wafugaji hao shida kubwa katika kupata matibabu. Hivi karibuni, mwandishi wetu wa habari alitembelea wilaya ya Zhongba, kusini magharibi mwa Tibet, na ametueleza jinsi hali ya huko ilivyo kwa hivi sasa.
Bw. Blo bzang Bstan a`dzin, mwenye umri wa miaka 41, ni mfugaji wa wilaya hiyo. Hivi karibuni, mke wake amepata ugonjwa wa moyo, hivyo alimpeleka kwenye hospitali iliyo umbali wa kilomita 600 kutoka kwenye malisho yake. Daktari alimwambia kuwa mke wake anapaswa kulazwa hospitalini. Baada ya kumaliza utaratibu wote wa kulazwa, wasiwasi wa Bw. Blo bzang Bstan a`dzin ulipungua, alimwambia mwandishi wetu wa habari akisema:
"Madaktari kijijini wanajua kutibu magonjwa madogo tu, kama vile, mafua, maumivu ya kichwa na kuharisha, lakini madaktari hao hawajui kutibu ugonjwa mkubwa, ndiyo maana wagonjwa hawana budi kwenda kwenye hospitali ya wilayani."
Wilaya ya Zhongba iko kwenye sehemu yenye mwinuko wa mita 5000 kutoka usawa wa bahari, ni wilaya yenye eneo kubwa isiyo na wakazi wengi. Wafugaji wapatao elfu 20 wanaishi kwenye wilaya hiyo yenye eneo la kilomita za mraba elfu 40. Ilipofika miaka ya 60 ya karne iliyopita, ndipo hospitali ya kwanza ya huko ilijengwa, yaani Hospitali ya Umma ya Wilaya ya Zhongba. Hospitali hiyo imetekeleza wajibu wake wa kuwahudumia wafugaji wa sehemu hiyo kwa miongo kadhaa, wakipatwa na magonjwa makubwa, wanakwenda kutibiwa kwenye hospitali hiyo. Ili kuboresha hali ya hospitali hiyo, mwaka jana kutokana na misaada ya idara ya afya ya sehemu hiyo, jengo jipya lenye vitanda zaidi ya 100 lilijengwa, na jengo hilo la kupendeza pia limekuwa alama ya sehemu hiyo.
Bw. Nyima Dondrup ni mpasuaji wa hospitali hiyo, daktari huyo mzee mwenye umri wa miaka 60 amefanya kazi katika hopitali hiyo karibu miaka 30, anawafahamu wafugaji wengi wa huko, akiwemo Bw. Blo bzang Bstan a`dzin. Kila mtoto na mke wa Bw. Blo bzang Bstan a`dzin wanapokwenda kwenye hospitali hiyo, watamwona daktari huyo. Katika miaka hiyo daktari huyo ameshuhudia hali ya hospitali hiyo ikiboreshwa siku hadi siku. Alisema:
"Hivi sasa, kama hospitali ya kawaida, hospitali yetu ina idara ya upasuaji?idara ya magonjwa ya ndani?idara ya magonjwa ya watoto na idara ya magonjwa ya wanawake. Zamani, tulikuwa hatuna vifaa vya kutosha vya matibabu, lakini hivi sasa, tumekuwa na vifaa vya aina nyingi, kama kifaa cha upimaji wa moyo na vingine vingi."
Kwa kuwa hakuna wakazi wengi wilayani, hivyo daktari Nyima Dondrup na wenzake wanakwenda vijijini mara kwa mara kuwatibu wagonjwa. Katika siku za zamani, kutokana na hali duni ya mawasiliano, walikuwa wanakwenda vijijini kwa miguu au kwa kupanda farasi. Daktari Nyima Dondrup alijivunia kwa uhodari wake katika kupanda farasi, alisema uhodari huo unatokana na mazoezi ya mara kwa mara wakati alipokwenda vijijini kuwatibia wagonjwa. Ili kuwahudumia wafugaji vizuri zaidi, mwaka jana hospitali hiyo ilinunua gari moja, madaktari wanapanda kwenda kuwatibia wagonjwa, hivyo farasi wa daktari Nyima Dondrup hatumiki tena.
Kila ifikapo majira ya joto na ya mpukutiko, daktari huyu na wenzake wanakwenda vijijini kuwatibu wagonjwa. Kwani wakati huo, wafugaji wanabeba chakula wanachoweza kutumia kwa miezi kadhaa na kusafiri umbali mrefu kulisha mifugo yao, kama wakati huo wakipatwa na ugonjwa, ni vigumu kwao kupata matibabu. Daktari Nyima Dondrup alisema kuwa wilaya ya Zhongba ina vijiji 60, ingawa kuna madaktari katika kila kijiji, lakini mbali na magonjwa madogo kama maumivu ya kichwa, madaktari hao hawajui kutibu magonjwa mengine makubwa. Wilayani humo kuna madaktari 20 tu wanaojua kutibu magonjwa makubwa, na kila mwaka madaktari hao wanakwenda vijijini mara tatu au nne na kutibu karibu aina zote za magonjwa.
Hivi sasa, ingwa wilaya hiyo haina tena tatizo la upungufu wa dawa na madaktari, lakini mkuu wa idara ya afya ya wilaya hiyo Bw. Zhao Huijun anaona kuwa, bado kuna matatizo kwenye shughuli za afya za wilaya hiyo, hivyo idara hiyo itachukua hatua kutatua matatizo hayo, Bw. Zhao alisema:
"Kwanza kabisa tunapaswa kuinua kiwango cha utaalamu wa madaktari; pili, tutaongeza idadi ya madaktari; tatu, tutakamilisha zaidi utaratibu wa matibabu, ili kuwarahisishia wafugaji kupata matibabu."
Kadiri hali ya afya inavyozidi kuboreshwa siku hadi siku, ndivyo wafugaji wa wilaya hiyo wanavyopata huduma kamili za afya. Katika muda mrefu uliopita, kutokana na mazingira mabaya na uchumi unaendelea polepole mkoani Tibet, serikali ya China inachukua sera maalum ya kumpatia kila mkulima au mfugaji ruzuku fulani kwa mwaka, lakini akipatwa na ugonjwa mkubwa, ruzuku hiyo bado haitoshi, hivyo utaratibu mpya wa matibabu ya ushirikiano unaenezwa katika sehemu nyingi za Tibet, yaani gharama za matibabu zitalipwa na serikali kuu, serikali ya mitaa na wafugaji au wakulima wenyewe, hivyo mzigo kwa matibabu wa wafugaji au wakulima utapungua. Wilaya ya Zhongba ilianza kutekeleza utaratibu huo tangu mwaka jana. Hivi sasa, wafugaji wote wa wilaya wa Zhongba wanashiriki kwenye utaratibu huo mpya, ambapo wanalipa yuan 10 za renminbi kwa mwaka, watarudishiwa asilimia 70 ya gharama za matibabu, hawana wasiwasi tena kuhusu gaharama za matibabu.
Idhaa ya Kiswahili 2005-08-24
|