Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-08-26 21:22:03    
China kuchukua hatua kuhimiza kuagiza bidhaa kutoka Kenya

cri

Katika miaka kumi iliyopita, ushirikiano wa uchumi na biashara kati ya China na Kenya umepata maendeleo makubwa. Lakini kutokana na miundo tofauti ya kiuchumi, hivi sasa bado kuna pengo kubwa la biashara kati ya nchi hizo mbili. Kutokana na hali hiyo, serikali ya China inafanya juhudi kuchukua hatua kuhimiza kuagiza bidhaa kutoka Kenya, na kuweka vitega uchumi katika nchi hiyo. Tarehe 8, mwezi Agosti, Wizara ya Biashara ya China ilituma ujumbe wa serikali wa kununua bidhaa nchini Kenya, na kufanya mazungumzo na wanaviwanda wa Kenya, ambapo pande hizo mbili zilijadili namna ya kupunguza pengo la biashara kati ya nchi hizo mbili.

Mazungumzo hayo yalifanyika tarehe 8, Agosti, kwenye Ofisi ya Uchumi na Biashara ya ubalozi wa China nchini Kenya. Wajumbe wa kampuni 7 kubwa za China, maofisa wa Ofisi ya uchumi na biashara ya Ubalozi wa China nchini Kenya, naibu mkuu wa Idara ya biashara ya nje ya Wizara ya biashara na viwanda ya Kenya, Kamati ya uendelezaji wa biashara ya nje ya Kenya, mkuu wa Chama cha viwanda na biashara cha Kenya na viwanda kutengeneza vya bidhaa nje vya Kenya walishiriki kwenye mazungumzo hayo.

Balozi mdogo wa biashara wa China nchini Kenya Bw. Li Yuan kwaza alielezea jinsi uhusiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya China na Kenya ulivyo. Akisema:

"Katika miaka kumi iliyopita, uhusiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya China na Kenya umepata maendeleo makubwa kwa hatua madhubuti, na ushirikiano wa kunufaishana kati ya pande zote mbili unaimarishwa siku hadi siku. Mwaka 2004, thamani ya biashara kati ya pande hizo mbili ilifikia dola za kimarekani milioni 366, ambayo imeweka rekodi mpya katika historia ya biashara kati ya pande hizo mbili. China na Kenya ina nguvu kubwa za kufanya ushirikiano wa biashara."

Bw. Li alieleza kuwa, viongozi wa nchi hizo mbili wanatembeleana mara kwa mara, hali hii imejenga mazingira mazuri kwa maendeleo ya ushirikiano wa uchumi na biashara kati ya pande hizo mbili. Katika miaka ya hivi karibuni, thamani ya biashara kati ya nchi hizo mbili inaongezeka kwa kiasi kikubwa. Bidhaa mbalimbali za China zinakaribishwa sana nchini Kenya, kama vile vyombo vya umeme nyumbani, nguo, vifaa vya ujenzi, dawa, mali ghafi ya bidhaa za kemikali, mashine na bidhaa za elektroniki. Kwa upande mwingine, bidhaa za Kenya zimeingia katika soko la China, kama vile chai ya Kenya, mkonge, kahawa, pareto, ngozi na vitu vya sanaa. Ingawa nchi hizo mbili zimefanya juhudi kubwa, lakini kutokana na miundo tofauti ya kiuchumi, bado kuna pengo kubwa la biashara kati ya pande hizo mbili, tena ni vigumu kubadilisha hali hiyo katika muda mfupi. Hivi sasa serikali ya China inachukua hatua kuhimiza kampuni za China kuongeza uwekezaji nchini Kenya, na kuagiza bidhaa kutoka nchi hiyo.

Kwenye mazungumzo hayo, naibu mkuu wa Idara ya biashara nje ya Wizara ya biashara na viwanda ya Kenya Bw. Manyara alitoa shukrani kwa juhudi za serikali ya China katika kupunguza pengo la biashara kati ya China na Kenya, akisema:

"Serikali ya China imetuma ujumbe wa ununuzi nchini Kenya kwa kuongeza uwezo wa Kenya kuuza bidhaa nchini China bila ya masharti yoyote. Jambo hilo ni nadra kutokea katika nyanja ya biashara."

Bw. Manyara alisema kuwa, Kenya na China zina urafiki mkubwa, na uhusiano huo mzuri umeweka msingi mzuri kwa maendeleo ya biashara kati ya pande hizo mbili. China ni soko kubwa lenye mustakabali mzuri kwa Kenya. Pia Bw. Manyara alieleza kuwa, bado kuna fursa nyingi kwa Kenya kupunguza pengo la biashara kati yake na China. Mwaka jana, thamani ya biashara kati ya Kenya na China ilifikia dola za kimarekani milioni 366, kati ya hizi bidhaa zilizoagizwa nchini Kenya ziliongezeka kwa asilimia 44.3, na ongezeko la bidhaa zilizouzwa nje lilifikia asilimia 94.3. Bw. Manyara anaamini kuwa, kutokana na juhudi za pamoja za serikali za nchi hizo mbili, pengo hilo litazidi kupunguzwa. Wakati huo huo ametumai kuwa, watalii wengi zaidi wa China watafanya utalii nchini Kenya, ili kuhimiza maendeleo ya uchumi na biashara ya Kenya.

Baada ya mkutano huo, mwandishi wetu wa habari alimhoji mwenyekiti wa Chama cha viwanda na biashara cha Kenya Bw. David Mburu Githere. Bw. Githere alisema:

Uhusiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya China na Kenya umepata maendeleo makubwa, mashirika mengi ya China yaliyoko nchini Kenya yametoa mchango mkubwa kwa maendeleo hayo.

Idhaa ya Kiswahili 2005-08-26