Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-08-31 20:34:34    
Vyuo vikuu mjini Shanghai vyafanya juhudi kubwa katika kuwasaidia wanafunzi wenye matatizo ya kiuchumi

cri
Vyuo vikuu mjini Shanghai vimefanya juhudi kubwa katika kuwasaidia wanafunzi wenye matatizo ya kiuchumi kwa njia mbalimbali ili waendelee na masomo, njia hizo ni pamoja na kutoa mkopo, kuwalipia gharama za masomo, kuwapatia fursa za kazi za baada ya muda wa masomo, kusamehe gharama ya masomo na kuwapatia marupurupu.

 

Wakati muhula mpya wa mwaka 2005 ulipoanza, ili kuwasaidia wanafunzi wapya kutoka kwenye familia maskini kulipia gharama za masomo yao, vyuo vikuu mbalimbali mjini Shanghai vimevumbua njia mbalimbali za kuwasaidia wanafunzi hao, njia hizo zimeondoa wasiwasi kwa wanafunzi hao unaosababishwa na umaskini.

Mwanafunzi Lin Xiaoxuan kutoka wilaya ya Shunchang, mkoani Fujian, alifanikiwa kujiunga na Chuo Kikuu cha Tongji huko Shanghai akiwa na matokeo mazuri katika mtihani wa kujiunga na katika chuo kikuu, kiongozi wa chuo kikuu hicho alimwandikia barua moja kumtia moyo Pamoja na barua hiyo, kiongozi huyo alimtumia kijitabu cha kanuni za Chuo Kikuu cha Tongji za kuwasaidia wanafunzi maskini, alisema anatumai kuwa Lin Xiaoxuan atakabiliana na taabu na changamoto kwa matumaini.

Zaidi ya hayo, chuo kikuu hicho kimempigia simu kila mwanafunzi mpya anayetoka vijijini na kumwuliza hali ya familia yake, halafu kitawatumia wanafunzi wenye matatizo ya kiuchumi yuan 300 kama posho ya usafiri wa kwenda Shanghai, hatua hiyo imewafanya wanafunzi hao wasikie ufuatiliaji wa chuo kikuu hicho kwao kabla hata hawajafika chuoni. Aidha, chuo kikuu hicho kimempatia kila mwanafunzi mpya anayetoka sehemu zilizokumbwa na mafuriko mwaka huu yuan 300 ikiwa ni gharama za vifaa vya masomo na maisha, ili kuwapunguzia mzigo wa kiuchumi wanafunzi hao na familia zao.

Chuo Kikuu cha Ualimu cha Huadong hivi karibuni kimewapatia wanafunzi fursa zaidi ya elfu 2 za kazi ya baada ya muda wa masomo, na kila mwanafunzi mwenye matatizo ya kiuchumi anaweza kupata kazi inayomfaa, hatua hiyo imewasaidia sana katika kulipia gharama za masomo na maisha ya kila siku. Wanafunzi wengi wenye matatizo ya kiuchumi wanafanya kazi kama walimu wa nyumbani, na wanafunzi wanaosoma katika sehemu mpya ya chuo kikuu hicho iliyoko katika kitongoji cha mbali watapewa yuan 14 kwa siku kama posho ya usafiri.

Ili kuwasaidia vizuri zaidi wanafunzi wenye matatizo ya kiuchumi, Chuo Kikuu cha Fudan hivi sasa kinajenga mradi wa kuwasaidia wanafunzi maskini kulipia gharama za masomo, yaani wanafunzi wenye matatizo ya kiuchumi wanaweza kuomba fedha zisizozidi yuan elfu 6 kwa kulipa gharama za masomo yao, na chuo kikuu hicho kinawahamasisha wanafunzi wanaonufaika na mradi huo wachangie mradi huo, na baada ya kuhitimu, wanafunzi pia wanaweza kuchangia mradi huo kwa kutuma ujumbe wa simu za mkononi, kwa mfano, mtu akiandika nambari 8 na kuituma kwa namba ya simu iliyowekwa na chuo kikuu hicho, maana yake ni kuwa atauchangia mradi huo yuan 8 kwa mwezi, hali kadhalika, akiandika nambari 15 na kuituma kwa namba hiyo hiyo, basi atauchangia mradi huo yuan 15 kwa mwezi.

Mwaka 2004, jumla ya fedha zilizotolewa na vyuo vikuu mjini Shanghai kuwasaidia wanafunzi wenye matatizo ya kiuchumi ilifika yuan milioni 32.35, na fedha hizo zimewanufaisha wanafunzi karibu elfu 21; Wanafunzi zaidi ya elfu 31 wamepata mikopo yenye thamani ya yuan milioni 264 iliyotolewa na taifa kwa ajili ya kuwasaidia wanafunzi maskini; Zaidi ya hayo, vyuo vikuu mbalimbali huko Shanghai vinaongeza nafasi za kazi za baada ya masomo kwa wanafunzi, katika mwaka 2004, ruzuku kwa ajili ya kazi za aina hiyo zilizidi yuan milioni 60, na kuwanufaisha wanafunzi elfu 85.

Idhaa ya Kiswahili 2005-08-31