Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-09-01 16:54:42    
Uhusiano kati ya Mjapan Bw. Ariga Motohiko na China

cri

Zaidi ya miaka 60 iliyopita, Bwana Ariga Motohiko alifika China akiwa mjumbe mmoja wa kikosi cha uendelezaji cha Japan, baadaye alijiunga na jeshi la ukombozi wa umma la China. Baada ya kurudi nchini Japan, Bw. Ariga alijishughulisha na jitihada ya urafiki kati ya Japan na China, na kutoa mchango mkubwa katika kuzidisha maelewano kati ya watu wa nchi hizo mbili.

Bwana Ariga Motohiko mwenye umri wa miaka 75 anaishi katika wilaya ya Nagano nchini Japan, ana afya nzuri, na ni mchangamfu. Nyumba ya Bw. Ariga siyo kubwa, lakini inaonesha upendo alio nao kwa China, vitabu kuhusu China vimejaa kwenye kabati , kwenye ukuta zimetundikwa picha za Bw. Ariga pamoja na marafiki zake wa China na zile zilizopigwa mbele ya shule ya msingi ya matumaini ya mkoa wa Mongolia ya ndani iliyojengwa kutokana na msaada wake.

Bw. Ariga alimwambia mwandishi wetu wa habari historia yake jinsi alivyokuja China zaidi ya miaka 60 iliyopita. Alisema kuwa, mwaka 1944, alipohitimu masomo ya shule ya msingi aliandikishwa kujiunga na kikosi cha vijana cha kuendeleza sehemu wanakoishi watu wa kabila la waman na wameng, kaskazini mashariki mwa China. Anasema:

"Wakati huo, serikali ya Japan ilituambia kuwa, tulitumwa katika sehemu ya Manzhou ili kujenga jamii nzuri pamoja na watu wa China, na baada ya kufika huko kwa miaka mitatu tutapewa ardhi, kama tukifanya kazi kwa bidii lazima tutakuwa na maisha mazuri huko nchini China. Mimi nilijiunga na kikosi hicho kutokana na matumaini mazuri ya kufanya kazi kwa bidii, halafu kuwakaribisha wazazi na ndugu zangu kuishi pamoja nami katika sehemu ya Manzhou. Lakini baada ya kufika tu kwenye sehemu ya Manzhou, ndoto yangu ilibadilika, niliyoyaona ni tofauti sana na yale niliyofikiria, Wajapan waliwabagua sana Wachina na Wakorea, na kuwafanya kama makuli."

Bw. Ariga hakuweza kusahau maisha yake akiwa katika kikosi cha uendelezaji. Kutokana na Urusi kutangaza kupambana na Japan, jeshi la Japan lilishindwa vibaya, wanaume wazima wote walilazimishwa kujiunga na jeshi, waliobaki kijijini walikuwa ni wazee, wanawake na watoto tu. Bw. Ariga mwenye umri wa miaka zaidi ya kumi wakati huo hakuwa na njia nyingine ila tu kurandaranda mitaani pamoja na watoto wengine. Ni wachina waliomwokoa yeye na watoto wengine wa Japan. Anasema:

"Kwa mara ya kwanza nilifahamishwa kuwa, Japan ilikuwa nchi ya kibeberu, lengo la wanajeshi wa Japan la kuivamia China ni kupora maliasili za China."

Bw. Ariga alisema kwa msisimko kuwa, wasingali kuwepo Wachina wema waliowapatia chakula na nguo, yeye na wenzake wasingekuwa hai hadi leo.

Katika majira ya mchipuko ya mwaka 1946, Bw. Ariga na wenzake zaidi ya 20 walipangiwa kusoma katika shule ya makada na chuo kikuu cha ualimu. Baada ya kumaliza masomo shuleni, Bw. Ariga alitumwa kufanya kazi katika idara ya uenezi ya makao makuu ya divisheni ya kwanza ya mkoa unaojiendesha wa Mongolia ya ndani, jukumu lake ni kueneza sera ya chama cha Kikomunisti cha China kuhusu mageuzi ya ardhi kwa njia ya kuonesha mchezo wa kuigiza. Anasema:

"Mwanzoni mwa mwezi Septemba mwaka 1946, mimi na wenzangu tulifika mjini Qiqihar, kujiandaa kurudi nchini Japan. Wakati huo, jeshi la Chama cha Guomintang lilifanya mashambulizi mara kwa mara dhidi ya sehemu zilizokombolewa na Chama cha Kikomunisti cha China. Ili kulipa fadhila tulizopewa na watu wa China na Chama cha Kikomunisti cha China, sote tuliacha mpango wa kurudi nchini Japan na tulijiunga na jeshi la ukombozi la watu wa China. Nilijifunza mambo ya uuguzi kwa miezi miwili katika hospitali ya jeshi la nchi kavu ya Qiqihar, halafu nikatumwa kufanya kazi katika hospitali ya kijeshi ya Nenjiang na sehemu nyingine kuwatibu majeruhi. Tarehe mosi mwezi Oktoba mwaka 1949, Jamhuri ya Watu wa China ilianzishwa, tulisikiliza kwa furaha kubwa hotuba iliyotolewa na mwenyekiti Mao Zedong kwenye roshani ya Tiananmen. Kuanzia siku hiyo, tulihamishwa kutoka hospitali ya kijeshi hadi hospitali ya makaa ya mawe ya Fuxin."

Mwezi Mei mwaka 1953, Bw. Ariga alikamilisha kazi na maisha ya miaka kumi hivi nchini China, na kurudi nchini Japan. Lakini jambo lililomhuzunisha ni kwamba, baada ya kurudi nchini Japan, alisimamiwa na kufuatwa na polisi wa Japan mara kwa mara na kutendewa vibaya na utawala wa Japan. Hata hivyo, Bw. Ariga aliendelea kujishirikisha na shughuli za urafiki kati ya Japan na China.

Hivi sasa Bw. Ariga ni mkurugenzi wa shirikisho la urafiki kati ya Japan na China la wilaya ya Nagano na mkurugenzi mkuu wa shirikisho la urafiki kati ya Japan na China la Toyoshinacyou la tarafa ya Azumi ya wilaya ya Nagano. Ili kuboresha hali ya mafunzo ya wanafunzi wa shule ya msingi wa China, Bw. Ariga alichangia fedha nyingi kujenga shule ya msingi ya matumaini ya kabila la wamongolia. Alisema kuwa, sasa yeye anashughulikia maingiliano kati ya wanafunzi wa shule za msingi wa Japan na China, kuzidisha maelewano kati yao kwa kuandikiana barua na kubadilishana michoro yao, ili wawe marafiki katika siku zijazo. Anaona kuwa, kuimarisha maingiliano kati ya vijana wa nchi hizo mbili kutaweka msingi mzuri kwa urafiki kati ya watu wa Japan na China.

Alipozungumzia kuhusu uhusiano wa hivi sasa kati ya Japan na China, Bw. Ariga alisema kuwa:

"Zamani kutokana na sera yenye makosa ya kitaifa, Japan ilizivamia China, Korea na nchi nyingine za Asia. Japan inapaswa kujikosoa kutokana na historia hiyo. Kwenye hekalu la Yakusumi vimewekwa vibao vya mizimu ya wahalifu wa kivita wa Japan waliowahi kuvamia China, lakini waziri mkuu wa Japan alikwenda mara kwa mara kwenye hekalu hilo kutoa heshima kwa vibao hivyo bila kujali upinzani wa China, Korea na nchi nyingine za Asia, jambo hili kamwe haliruhusiwi na watu.

Idhaa ya kiswahili 2005-09-01