Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-09-02 21:35:40    
Baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika lina mustakabali mzuri

cri

Tarehe 22 na 23 Agosti, mkutano wa nne wa maofisa waandamizi wa Baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika ulifanyika mjini Beijing, ambapo wajumbe wa nchi 46 za Afrika, wachunguzi wa mashirika 6 ya kikanda ya Afrika, mabalozi wa Afrika nchini China na wajumbe wa China walihudhuria mkutano huo, wakijadiliana kuhusu namna ya kuimarisha ushirikiano kati ya pande hizo mbili. Mkutano huo umeonesha matakwa ya kisiasa na ari ya China na nchi za Afrika ya kuzidisha ushirikiano kati yao.

Baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika lilianzishwa mwaka 2000, na linaendelea vizuri chini ya ufuatiliaji na juhudi za pamoja za pande mbili za China na Afrika. Katika miaka mitano iliyopita, uhusiano wa ushirikiano kati ya China na Afrika uliendelea vizuri katika sekta za siasa, uchumi na biashara, utamaduni na sayansi na teknolojia.

Kwanza, China imeongeza misaada kwa nchi za Afrika. Kuanzia mwaka 2004 hadi mwezi Mei mwaka huu, kwa nyakati tofauti, China ilitoa misaada 167 kwa nchi 46 za Afrika. China pia ilisaini mikataba ya kujenga miradi mingi na nchi za Afrika, na kuzisaidia nchi za Afrika kujenga miundombinu ya barabara, shule, hospitali na miradi ya usambazaji maji. Inasemekana kuwa katika miaka kadhaa ijayo, China itaongeza misaada mingine kwa nchi za Afrika katika ujenzi wa miundombinu na sekta ya kilimo. Katibu mkuu wa kamati ya China inayoshughulikia mambo ya ufuatiliaji ya baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika Bi. Xu Jinghu alisema:

"Mwaka 2004, thamani ya uwekezaji wa moja kwa moja wa wanakampuni wa China barani Afrika ilifikia dola za kimarekani milioni 135. Na kuanzia mwaka 2004 hadi mwezi Mei mwaka 2005, wanakampuni wa China waliwekeza na kuanzisha mashirika 116 katika nchi za Afrika. Hadi sasa China imesaini "mkataba wa kuhimiza na kulinda uwekezaji" na nchi 25 za Afrika.

Wakati utoaji misaada na uwekezaji wa moja kwa moja wa China barani Afrika unapoongezeka kwa kiasi kikubwa, biashara kati ya China na Afrika pia imeongezeka kwa haraka. Mwaka 2004, thamani ya biashara kati ya China na nchi za Afrika ilifikia dola za kimarekani bilioni 29.5, ikiongezeka kwa asilimia 58.9 ikilinganishwa na mwaka uliotangulia. Mfumo wa biashara kati ya pande hizo mbili pia umeelekea kuwa mzuri siku hadi siku, ambapo urali mbaya wa kibiashara kati ya China na Afrika umepunguzwa zaidi, thamani ya bidhaa zilizoagizwa na China kutoka Afrika imeongezeka kwa kiasi kikubwa. Ilipofika mwezi Mei mwaka 2005, China ilisaini "mkataba wa kutotoza ushuru maradufu" na nchi 41 za Afrika. Hali ya mwaka huu ya kibiashara kati ya China na nchi za Afrika ni ya kuridhisha, thamani ya biashara imeongezeka kwa asilimia 43 hivi kuliko mwaka jana wakati kama huu.

Zaidi ya hayo, China imefanya juhudi kubwa katika kuzipa nchi 28 za Afrika zilizo maskini kabisa duniani kipaumbele cha biashara. Kutokana na mikataba iliyosainiwa kati ya China na nchi 28 za Afrika zilizo nyuma kabisa kiuchumi duniani , kuanzia tarehe mosi Januari mwaka 2005, aina 190 za bidhaa za nchi 25 za Afrika zitaondolewa ushuru wakati wa kuingia nchini China, na nchi nyingine 3 ziko katika mchakato wa kubadilishana nyaraka. Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na idara ya forodha ya China, China imeagiza bidhaa zenye thamani ya dola za kimarekani milioni 138 kutoka nchi hizo 25 za Afrika, ambapo ushuru ulioondolewa umefikia dola za kimarekani zaidi ya milioni 3.7. Ili kutekeleza vizuri sera hiyo, China pia iliandaa semina kuhusu mambo ya forodha kwa maofisa husika wa baadhi ya nchi za Afrika zilizopewa sera hiyo ya kipaumbele.

Ili kuzisaidia nchi za Afrika kupata maendeleo endelevu, kwenye mkutano wa pili wa ngazi ya mawaziri wa baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika, maendeleo ya nguvukazi yalithibitishwa kuwa mradi muhimu wa ushirikiano kati ya China na Afrika katika siku zijazo. Serikali ya China imeongeza fedha katika shughuli za kuwaandaa wataalam wa sekta mbalimbali wa nchi za Afrika, na kuanzisha "mfumo wa uratibu wa ushirikiano wa maendeleo ya nguvukazi". Mwaka jana, China iliongeza fedha maradufu katika mradi huo, na kuandaa mafunzo zaidi ya 100 yaliyowashirikisha wanafunzi 2446 wa mambo mbalimbali ya kilimo, afya na matibabu, elimu, utamaduni, habari, forodha na kidiplomasia, kuwapa wanafunzi 332 wa nchi za Afrika nafasi za kusoma katika vyuo vikuu nchini China, na kuwatuma walimu zaidi ya 60 wa China kuzisaidia nchi za Afrika kuwaandaa wataalam. Mwaka huu, China inapanga kuwaandaa wataalam 3800 wa sekta mbalimbali, ili kufanya matayarisho mazuri kwa maendeleo ya siku zijazo ya nchi za Afrika.

Baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika limepata mafanikio mazuri, waziri msaidizi wa mambo ya nje wa China bwana Lu Guozeng alisema:

"Uzoefu wa miaka mitano iliyopita umethibitisha kuwa, baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika limekuwa utaratibu mzuri wa kufanya majadiliano na ushirikiano kati ya pande hizo mbili, limekuwa na umuhimu mkubwa siku hadi siku katika maendeleo ya uhusiano kati ya China na nchi za Afrika, na linakaribishwa na pande zote mbili na kufuatiliwa na jumuiya ya kimataifa."

Alipozungumzia kuhusu mustakabali wa kazi ya baraza hilo siku zijazo, katibu mkuu wa kamati ya China inayoshughulikia mambo ya baraza hilo Bi. Xu Jinghu alisema:

"Hali mpya imetoa mahitaji mapya kwa ushirikiano wa kirafiki kati ya China na nchi za Afrika. Kufuatana na maendeleo ya zama tulizonazo, kufanya uvumbuzi, na kuimarisha umoja na ushirikiano kati ya China na Afrika kumekuwa matakwa ya pamoja kati ya pande hizo mbili, na kunaendana na maslahi ya pamoja ya pande zote mbili."

Siku zijazo, katika upande wa kisiasa, China itadumisha maingiliano ya ngazi ya juu kati yake na nchi za Afrika, ili kuimarisha uaminifu, na kuanzisha uhusiano mpya wa kiwenzi wa kimkakati kati ya China na Afrika. Kwa upande wa kiuchumi na kibiashara, China itaendelea kutoa misaada kwa nchi za Afrika bila ya masharti yoyote.

Baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika limetoa mchango mkubwa katika kuhimiza urafiki kati ya China na Afrika na kuharakisha maendeleo ya Afrika. China itaendelea kushirikiana na marafiki wa Afrika, na kuzidisha ushirikiano wa kirafiki kati ya pande hizo mbili.

Idhaa ya Kiswahili 2005-09-02