Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-09-05 21:28:20    
Rasilimali za utalii nchini China

cri

China ni nchi kubwa yenye mito na milima mizuri, na utamaduni adhimu. China ina makabila mengi yenye mila na desturi tofauti na inajulikana sana duniani kwa uzalishaji wa mazao ya jadi na asilia pamoja na mapishi mazuri ya chakula ya aina mbalimbali. China ina rasilimali nyingi za utalii na uwezo mkubwa wa shughuli za utalii katika siku za baadaye. Pamoja na maendeleo ya uchumi wa China na kutekelezwa kwa sera za kufungua mlango, sekta ya utalii imekuwa ni yenye ongezeko jipya la maendeleo ya uchumi. Hivi sasa sehemu zenye mandhari nzuri za utalii zinaongezeka kwa mfululizo katika sehemu mbalimbali za China, ambapo idadi ya watalii wanaotembelea China kutoka nchi za nje inazidi kuongezeka kutokana na kuboreshwa kwa miundo-mbinu nchini China.

China ni moja ya nchi ambazo ni asili ya ustaarabu duniani, historia na utamaduni adhimu, vitu ambavyo vimekuwa rasilimali yenye thamani kubwa ya utalii.

Miongoni mwa mabaki mengi maarufu ya kihistoria nchini China, pango kubwa la sanamu za askari na gari la kukokotwa na farasi la shaba lililoko karibu na kaburi la mfalme wa kale wa enzi ya Qing vinasifiwa kuwa ni moja ya maajabu nane duniani, na kuvutia watalii zaidi ya milioni moja kwa mwaka. Mbali na hayo, picha za kutani ndani ya mapango ya Mogao, mjini Denghuang zinachukuliwa kuwa ni sanaa adimu ya dunia. Ukuta mkuu wenye urefu wa kilomita elfu 5 ni kitu ambacho watalii wanatarajia kukiona kila wanapofika China. Aidha China ina makabila 56 yenye historia, utamaduni, mila na desturi maalumu pia vinawavutia sana watalii.

Na sasa tunawaelezea mandhari nzuri ya kimaumbile nchini China.

China ina rasilimali nyingi za maumbile, licha ya Jiuzaigou, Zhangjiajie na Huanglong, ambazo zimeorodheshwa kuwa mabaki ya kimaumbile ya dunia, kuna sehemu nyingine zenye mandhari nzuri ya kimaumbile zikiwa ni pamoja na Guilin ya sehemu ya kusini magharibi, milima ya Changbai ya sehemu ya kaskazini mashariki, milima ya Wasichana Wanne ya mkoa wa Guzhou na misitu ya sehemu ya joto ya Xishuangbanna ya mkoa wa Yuannan pamoja na mandhari ya misitu ya minazi ya kisiwa cha Hainan pia ni mandhari nzuri ya kimaumbile.

MILIMA NA MITO YA GUILIN

Mji wa Guilin uko katika mkoa unaojiendesha wa kabila la wazhuang, kusini magharibi ya China, hali ya hewa ya huko ni ya vuguvugu na yenye unyevunyevu; hakuna baridi kali katika majira ya baridi, wala joto kali katika majira ya joto, na katika majira yote ya mwaka miti na majani huonekana ya rangi ya kijani, wastani wa hali-joto kwa mwaka ni nyuzi 19 za sentigredi.

Guilin ina mazingira bora ya kimaumbile, kutokana na utafiti wa kijiolojia, Guilin ilikuwa bahari kubwa kabla ya miaka milioni 300. kutokana na kuhamahama kwa ardhi ya dunia, mawe ya chokaa yaliyokuwa chini ya maji ya bahari yaliinuka juu na kuwa ardhi, baada ya kupigwa na upepo, jua na mvua kwa miaka mingi, yakawa milima inayopendeza, mapango marefu ya kupendeza na mito iliyopita chini ya ardhi. Sura nzuri ya milima, mto Li, mashamba na vijiji vimekuwa mandhari nzuri ya pekee, ambayo vinajulikana kwa "Mandhari ya Guilin inatia fora duniani".

Guilin ni mji wa kale wenye historia ya miaka mingi, ambao uliojengwa miaka 2,110 iliyopita. Hivi sasa, Guilin ina sehemu 109 za hifadhi za vitu vya kali za ngazi za taifa, mkoa na mji. Mashairi yaliyotungwa na wasomi wa enzi mbalimbali ya kusifu milima na mto wa Guilin na sanamu za kibudha, yako katika mapango ya milimani, hususan yako katika Guihai na genge la Mo la mlima wa magharibi. Sehemu maarufu zenye mandhari nzuri katika mji wa Guilin ni pamoja na mlima wa Pilian, bustani ya nyota 7, chemchem ya Longsheng, mawe ya filimbi na mlima wa pua ya ndovu.

Hivi sasa, mji wa Guilin una mahoteli 28 ya ngazi ya nyota ya wageni, mashirika 18 ya utalii na watembelezaji na wakalimani wa lugha za nchi za kigeni wapatao zaidi ya 1,000. Katika miaka ya karibuni, ujenzi wa miundo-mbinu imekuwa ikikamilishwa hatua kwa hatua, hivi sasa kuna njia ya safari za ndege zaidi ya 40 zinazofika kwenye miji mikubwa ya nchi za nje.

Idhaa ya Kiswahili 2005-09-05