Lugha ya Kichina ni lugha inayotumiwa na watu wengi zaidi duniani. Katika miaka ya karibuni, kadiri China inavyozifungulia mlango nchi za nje na uchumi wa China unavyoendelea kukua kwa kasi, ndivyo mawasiliano na maingiliano kati ya China na nchi nyingine duniani yanavyoendelea kuongezeka kwa kina. Makampuni na viwanda vingi vya nchi za nje vinawekeza mitaji na kuanzisha matawi nchini China, ambapo idadi ya watu wanaotembelea China, wanaokuja kusoma na wanaokuja kufanya biashara hapa China inaongezeka siku hadi siku. Lugha ya Kichina ikiwa chombo cha kuifahamu China inatiliwa maanani na serikali na idara za elimu za nchi mbalimbali duniani.
Miongoni mwa wageni wanaojifunza Kichina, wengi wao ni wa nchi jirani za China, kama vile, Vietnam, Thailand, Korea ya Kusini na Japan, kwani utamaduni wa nchi hizo unafanana na utamaduni wa China, na nchi hizo zinafanya mawasiliano ya mara kwa mara na China.
Ofisa wa wizara ya elimu ya Vietnam Bw. Vu Minh Tuan alisema kuwa vijana wengi nchini Vietnam wanapenda kujifunza lugha ya Kichina.
"Hivi sasa wanafunzi nchini Vietnam wanapenda kujifunza lugha ya Kichina. Mbali na vyuo vikuu, vituo vingi vya Kichina pia vimefungua masomo ya Kichina, na wanafunzi wengi wanatumia muda wao baada ya masomo kujifunza Kichina."
Mbali na Vietnam, watu wa nchi zote za Asia ya Kusini Mashariki wana hamu kubwa ya kujifunza lugha ya Kichina. Vyuo vikuu vingi na shule nyingi za msingi na sekondari za nchi hizo zimeanza kufundisha lugha ya Kichina, zaidi ya hayo, baadhi ya idara za jamii pia zinafundisha masomo ya lugha ya Kichina. Kwa mujibu wa takwimu, idadi ya watu wanaojifunza lugha ya Kichina kwenye sehemu ya Asia ya Kusini Mashariki imefikia milioni 1.6.
Kwenye sehmu ya Asia ya Mashariki, watu wengi wa Japan na Korea ya Kusini wanajifunza Kichina, vyuo vikuu vipatavyo 200 vya Korea ya Kusini vimeanza kufundisha masomo ya lugha ya Kichina, na lugha ya kichina imekuwa moja ya somo ambalo wanafunzi wanatakiwa kufaulu kabla ya kujiunga na chuo kikuu; Nchini Japan hivi sasa kuna watu zaidi ya milioni 2 wanaojifunza lugha ya Kichina, na idadi ya shule za sekondari zinazoweka masomo ya Kichina imeongezeka kwa mara 10 katika miaka hiyo 20.
Kerstin Storm ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Minstel cha Ujerumani, wakati alipokuwa anasoma katika shule ya sekondari alikuwa anaipenda nchi ya China na lugha ya Kichina, lakini shule yake ya sekondari ilikuwa haifundishi masomo ya lugha ya Kichina, ilipofika anapojiunga na chuo kikuu, msichana huyo alichagua kujifunza lugha ya Kichina. Baada ya kujifunza kwa miaka minne, hivi sasa msichana huyo anaweza kuongea kichina vizuri, alimwambia mwandishi wetu wa habari akisema:
"Hivi sasa, kuna nafasi nyingi za ajira nchini China, kwani makampuni mengi ya Ujerumani yanaanzisha matawi yake nchini China, na uhusiano wa kibiashara kati ya China na Ujerumani unasonga mbele siku hadi siku, hivyo naona kuwa kujua lugha ya Kichina kutanisaidia katika kutafuta ajira."
Msichana Kerstin Storm alisema, hivi sasa watu wengi nchini Ujerumani wanajifunza Kichina, na idadi hiyo bado inaongezeka. Wakati alipokuwa anasoma katika chuo kikuu, darasa moja la lugha ya Kichina lilikuwa na wanafunzi 10 tu, hivi sasa darasa moja lina wanafunzi 40. Msichana huyo anasema kuwa, kama yeye mwenyewe, wajerumani wengi wanaojifunza lugha ya kichina wanaona kuwa kujua Kichina kutawasaidia katika kutafuta ajira, lakini sababu za baadhi ya watu kujifunza Kichina ni kuwa wanapenda utamaduni na historia ya China.
Katika nchi nyingine za Ulaya, mafunzo ya lugha ya Kichina yanaenezwa, kwa mfano, watu elfu 30 nchini Ufaransa wanajifunza Kichina, idadi hiyo ni kubwa zaidi kuliko nchi nyingine za Ulaya; Uingereza inashirikiana na idara husika za China kutunga vitabu vya kiada vya Kichina kwa shule za Sekondari; nchini Russia, makampuni mengi yanashindana na wizara ya mambo ya nje kutoa mishahara mikubwa ili kuwaajiri watu wanaojua lugha ya Kichina.
Hivi sasa, idadi ya watu wanaojifunza lugha ya Kichina inaongezeka kwa kasi zaidi kuliko idadi ya watu wanaojifunza lugha nyingine. Mwenyekiti wa baraza la vyuo vikuu vya Marekani Bw. Gaston Caperton, ambaye alishiriki kwenye Baraza la Lugha ya Kichina Duniani lililofanyika hapa Beijing, alisema kuwa asilimia 30 ya vyuo vikuu vya Marekani vimefungua masomo ya lugha ya Kichina, na Software ya kufundisha Kichina iliyotengenezwa na serikali ya China na Marekani inatumika katika shule za msingi na sekondari nchini Marekani. Bw. Caperton alisema:
"Tunafanya juhudi katika kueneza lugha ya Kichina katika shule za msingi, sekondari na vyuo vikuu, na kuwafundisha wanafunzi utamaduni wa China. Napenda kujenga daraja la mawasiliano kati ya China na Marekani."
Kwa mujibu wa takwimu, hivi sasa watu zaidi ya milioni 30 duniani wanajifunza lugha ya Kichina kwa njia mbalimbali. Kadiri idadi ya watu wanaojifunza lugha ya Kichina inavyoongezeka, ndivyo mahitaji ya nchi mbalimbali ya walimu wa Kichina yanavyoongezeka. Ili kukidhi mahitaji hayo ya nchi mbalimbali, China imechukua hatua nyingi, kwa mfano imeanzisha kikundi kimoja kuongoza na kuratibu mafunzo ya Kichina katika nchi za nje, kutenga fedha nyingi zaidi kutunga vitabu vya kiada vya Kichina vya aina mbalimbali, kuwaandaa walimu wengi zaidi wa Kichina na kuwapeleka walimu hao na watu wanaojitolea katika nchi za nje. Aidha, China imeanzisha taasisi 27 za Confucious katika sehemu mbalimbali duniani ili kuwafundisha watu lugha ya Kichina na kueneza utamaduni wa China. Mwenyekiti wa Baraza la Lugha ya Kichina Duniani, ambaye pia ni mjumbe wa taifa wa China Bi. Chen Zhili alisema:
"Katika siku zijazo, tutaendelea kufanya ushirikiano na nchi mbalimbali duniani katika kutoa mafunzo ya lugha ya Kichina, na kuzisaidia nchi na sehemu zenye mahitaji hayo. Tutatenga fedha nyingi zaidi kwa ajili ya mafunzo ya lugha ya Kichina, na kutoa huduma nzuri zaidi za mafunzo ya lugha ya Kichina kwa nchi za nje."
Idhaa ya Kiswahili 2005-09-07
|