Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-09-08 15:01:26    
Wageni wanaopenda kuishi vichochoroni mwa Beijing

cri

Wageni wengi kutoka ng'ambo wanaofanya utalii au kuja kufanya kazi mjini Beijing hupenda kutembelea vichochoro vya Beijing, baadhi yao hata wanapenda kuishi katika nyumba za kupanga na hoteli za watu binafsi zilizoko vichochoroni. Muda si mrefu uliopita, mwandishi wetu wa habari aliwakuta wageni kadhaa wanaopenda kuishi katika nyumba za vichochorini hapa mjini Beijing.

Vichochoro vya Beijing vinahusiana barabara na mtindo wa ujenzi wa mji mkongwe wa Beijing. Sehemu ya makazi ya zamani ya watu wa Beijing huundwa na nyumba mbalimbali zilizojengwa kwa kuzingira ua, na njia zilizounganisha nyumba hizo huitwa vichochoro. Vichochoro vya Beijing vimekuwa na historia zaidi ya miaka 800, na nyumba zilizojengwa katika vichochoro hivyo ni makazi muhimu ya watu wa Beijing siku za zamani, pia ni sehemu zilizohifadhi vizuri mila na desturi za wakazi wenyeji wanaoishi kizazi kwa kizazi mjini Beijing.

Kichochoro cha Juer kiko katika sehemu ya mashariki ya mji wa Beijing, kina urefu zaidi ya mita 400, historia yake imefikia zaidi ya miaka 400, zamani maofisa na watu wengi wa ngazi ya juu walikuwa wanaishi huko. Hivi sasa, kwenye kichochoro hicho bado kuna nyumba nyingi za aina hiyo. Nyumba hizo na mtindo wa maisha ya huko unawavutia sana wageni.

Katika kichochoro cha Juer, mwandishi wetu wa habari alimkuta mhandisi wa ujenzi kutoka Ujerumani Bwana Berna Hard Sauerbier, ambaye ameajiriwa kufanya kazi katika taasisi moja ya utafiti wa ujenzi ya Beijing. Bw. Berna Hard alikuja Beijing kutoka Berlin muda mfupi uliopita, na alikuwa anatafuta nyumba ya kupanga kichochoroni. Alisema kuwa, alichagua kuishi huko kutokana na kupenda hali ya vichochoro vya Beijing. Anasema:

"Naona hapa ni mahali pazuri sana, nyumba zinaonekana zilijengwa zamani sana, lakini baada ya kufanyiwa ukarabati, maisha ya wakazi wa huko yamepata urahisi zaidi kuliko zamani. Kwenye ua wa nyumba, imepandwa miti na maua, watu wazima wanapunga upepo, huku watoto wakicheza, hali hiyo ni nadra kuonekana nchini Ujerumani. Nyumba za vichochoroni zimekuwa majengo yanayojaa harufu nzito ya maisha ya raia wa Beijing, zimekuwa sehemu moja ya historia ya mji huo."

Hivi sasa, kwenye kichochoro cha Juer kuna familia 200 hivi, na familia 40 kati ya hizo ni wageni kutoka Uingereza, Marekani, Ufaransa, Ujerumani na Israel. Kuna makarani wanaofanya kazi katika mashirika yaliyowekezwa na wafanyabiashara kutoka ng'ambo, waandishi wa habari, wanafunzi na wanaojiajiri.

Bwana Kong Baorui ni mwandishi wa habari kutoka Israel, jina hilo la kichina alipewa na rafiki yake mchina, jina lake ni Baruh Kohen. Bw. Kong Baorui alikuja Beijing zaidi ya miezi 7 iliyopita, yeye ni mwandishi wa habari wa kujiajiri katika gazeti moja la Kiingereza mjini Beijing.

Ingawa Bw. Kong Baorui alikuja Beijing muda mfupi uliopita, lakini anajua kuwasiliana na majirani zake kwa lugha ya Kichina. Alisema kuwa japokuwa bado hajajua kuzungumza Kichina sanifu, lakini marafiki zake wanapenda kuzungumza naye . Akisema:

"Wakazi wa hapa ni wakarimu na wachamgamfu. Hata nikiongea vibaya kwa Kichina, hunioneshea urafiki na ukarimu wao, hiyo inanifurahisha sana."

Wakati wa mapumziko, Bw. Kong Baorui anapenda kunywa kahawa katika mkahawa mdogo ulioko kichochoroni. Anapenda huduma za huko, hasa ladha nzuri ya kahawa na keki ya jibini.

Wageni wanaoishi katika kichochoro cha Juer wanaelewana vizuri na wakazi wa huko, wakipata nafasi hupiga soga pamoja, na kusalimiana kwa uchangamfu. Muuzaji matunda Bi. Zheng Fengying mara kwa mara anawakuta wageni wengi wanaonunua matunda kutoka kwake. Anasema:

"Wageni hao wana adabu kubwa, kila wakija kununua matunda hunisalimia kwa Kichina. Mimi pia napenda kuwasalimia."

Hoteli zilizoko karibu na vichochoro vya Beijing pia zinapendwa sana na wageni watalii. Karibu na kichochoro cha Juer, kuna hoteli ya Qingzhuyuan inayoendeshwa na mtu binafsi. Hoteli hiyo ina vitanda 30, gharama kwa usiku mmoja kwa chumba ni yuan 210. Mwenye hoteli Bi. Zhao Shuhua alisema kuwa, hoteli hiyo ilianza kufanya biashara mwezi mmoja uliopita, lakini karibu kila siku inajaa wageni. Mwandishi wetu wa habari aliona kuwa, karibu wageni wote wa hoteli hiyo ni watalii kutoka ng'ambo, watumishi vijana wa hoteli hiyo wanawahudumia wageni kwa kuongea Kiingereza.

Mwandishi wa habari alimkuta mtalii kutoka Uingereza bwana Christopher Thornton na mchumba wake. Walikuja China wiki tatu zilizopita, walikuwa wametembelea miji ya Shanghai na Xi'an. Baada ya kufika Beijing, walifahamishwa na rafiki kuagiza chumba kwenye hoteli ya Qingzhuyuan, waliridhika na bei, huduma na mazingira yenye umaalum wa utamaduni wa Beijing wenye historia ndefu. Walisema:

"Hoteli hiyo ni nzuri sana, wageni kutoka nchi mbalimbali wanaishi pamoja kwa urafiki kama kuishi katika familia moja."

Hivi sasa mji wa Beijing umekuwa mji mkubwa wa kisasa, kwenye sehemu ya kibiashara, majengo marefu yamesimama hapa na pale, magari yanaenda na kurudi kwa wingi, yote hayo yanaonesha pilikapilika na ustawi wa mji mkubwa. Lakini kutokana na serikali ya Beijing kutilia maanani hifadhi ya vichochoro katika ujenzi na maendeleo ya mji huo, kama vile kudhibiti urefu wa majengo ya sehemu ya mji mkongwe, kutoruhusu kupanua barabara za mitaa hiyo, na magari yamepigwa marufuku kupita kwenye baadhi ya vichochoro. Hivyo kwenye vichochoro, hali asilia na hali ya utulivu inaonekana huko, hakuna kelele nyingi kama za barabarani. Baada ya matembezi ya siku nzima, kukaa kwenye hoteli hiyo ya kibinafsi iliyoko katika kichochoro, Bw. Christopher na wenzake wanajisikia kupumzika vizuri kiroho na kimwili.

Mji wa Beijing una vichochoro zaidi ya 1000 kama cha Juer, na vinasifiwa kuwa ni sehemu ya vivutio wanayoishi watu mjini Beijing. Kama mhandisi huyo wa ujenzi wa Ujerumani Bwana Berna Hard alivyosema, vichochoro vimekuwa sehemu moja ya utamaduni wa jadi wa Beijing, pia ni dirisha moja kwa wageni kujua hali ya mji wa Beijing wenye historia ndefu.

Idhaa ya kiswahili 2005-09-08