Kuanzia tarehe 15 hadi 19 Agosti, rais Kibaki wa Kenya alifanya ziara ya kitaifa nchini China. Hii ni mara yake ya kwanza kuitembelea China tangu ashike madaraka ya urais wa Kenya, yeye pia ni rais wa kwanza wa Kenya kuitembelea China katika miaka 11 iliyopita tangu mwaka 1994. Balozi wa China nchini Kenya Bwana Guo Chongli aliyefuatana na rais Kibaki katika ziara yake nchini China alisema:
"Rais Kibaki alikuja China akiongoza ujumbe mkubwa wenye wajumbe 18, wakiwemo mawaziri 7, ambao ni waziri wa mambo ya nje, waziri wa fedha, waziri wa mawasiliano ya simu na habari, waziri wa utalii na waziri wa serikali za mitaa, jambo hilo limeonesha kuwa serikali ya Kenya inatilia maanani sana uhusiano kati yake na China."
Kutokana na maelezo ya balozi Guo Chongli, rais Kibaki aliwahi kusoma katika chuo kikuu cha uchumi cha London, na kushika nyadhifa nyingi za ngazi ya juu katika serikali ya Kenya. Tangu rais Kibaki ashike madaraka, serikali ya Kenya imechukua sera za kidiplomasia za kufanya ushirikiano na pande nyingi, na kutoa sera ya kutupia macho mashariki. Yaani inadumisha uhusiano wa jadi kati yake na nchi za magharibi, huku ikiimarisha maingiliano na nchi za mashariki, na ziara yake hii nchini China ni kitendo halisi cha kutekeleza sera hiyo ya kutupia macho mashariki.
Mwaka huu ni mwaka wa kuadhimisha miaka 600 ya Zheng He kusafiri mbali baharini, ambaye aliwahi kuongoza kikosi chake kufika pwani ya Kenya. China na Kenya zimeshirikiana kufanya shughuli nyingi za kuadhimisha tukio hilo. Msichana mmoja mwenye umri wa miaka 19 anayeishi kwenye kisiwa cha Lamu Bi. Mwamaka Shariff anayesemekana kuwa ni wa kizazi cha baharia wa China, alialikwa kuja nchini China kushiriki kwenye shughuli za maadhimisho hayo, viongozi wa China walikutana naye, na serikali ya China pia imempa nafasi ya kusoma katika chuo kikuu nchini China. Baada ya kurudi nchini Kenya, jamaa zake wa Mombasa walifanya sherehe kubwa ya kumkaribisha, gazeti la Daily Nation la Kenya lilichapisha makala kuhusu safari yake nchini China kwa kurasa tatu kamili, hadithi yake inajulikana sana nchini Kenya.
Rais Kibaki alihusisha ziara yake hii nchini China na safari ya Zheng He nchini Kenya. Alipofanya mazungumzo na rais Hu Jintao wa China alisema kuwa, kabla ya miaka 600 iliyopita, msafiri mkuu wa China Bwana Zheng He alifika Kenya akiongoza msafara mkubwa wa merikebu, sasa yeye amefika China mwenyewe pamoja na ujumbe wake. Anatumai kuwa, ziara yake hii pia itasukuma mbele maendeleo ya uhusiano wa kirafiki kati ya Kenya na China.
Kama rais Kibaki alivyotarajia, ziara yake hii nchini China kweli ilipata mafanikio makubwa. Balozi wa Kenya nchini China Bi. Ruth Solitei alimwambia mwandishi wetu wa habari akisema:
"Rais wetu wa Kenya safari yake yalianza Shanghai, ambapo alikutana na meya wa Shanghai, pia akakuwa na mkutano na wanabiashara wa huko Shanghai. Alipokuja hapa Beijing, alikutana na rais Hu Jintao, ambao walizungumza kuhusu mambo ya uhusiano kati ya nchi hizo mbili. Na pia tukakamilisha makubaliano tofauti, ambayo ni pamoja na kuruhusu ndege yetu ya Kenya kufika hapa China. Pia alienda Shenchen na Hongkong."
Rais Kibaki alipata picha nzuri sana kuhusu utamaduni wa China na maendeleo makubwa yaliyopatikana nchini China. Alipokuwa mjini Beijing alitembelea ukuta mkuu na kasri la kifalme. Kwenye ukuta mkuu, aliuliza kwa kinaganaga kuhusu historia ya ujenzi wa mradi huo mkubwa, na kusifu sana uvumbuzi na busara za watu wa China. Alipotembelea mji wa Shanghai na mji wa Shenzhen, ambayo ni mji mkubwa kabisa wa viwanda na mji mpya wa kisasa kusini mwa China alisema kuwa, uzoefu wa kukuza uchumi wa China kweli unastahili kuigwa na Kenya, aliwakaribisha wanakampuni wa China kuwekeza vitega uchumi nchini Kenya.
Balozi Guo Chongli alisema kuwa, serikali ya China pia inatilia maanani sana kukuza uhusiano na Kenya, rais Hu Jintao, spika wa bunge la umma la China Bwana Wu Bangguo na waziri mkuu Wen Jiabao wote walikutana naye. Akisema:
"Alipokuwa mjini Beijing, pande hizo mbili zilisaini mikataba mitano kuhusu kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na kiteknolojia kati ya serikali za nchi hizo mbili, serikali ya Jamhuri ya Watu wa China kuipatia Kenya mikopo yenye riba nafuu, kufanya ushirikiano wa utangazaji wa radio kati ya idara kuu ya radio, filamu na Televisheni ya China na wizara ya habari na mawasiliano ya simu ya Jamhuri ya Kenya. Idara ya utalii ya Kenya ilifanya sherehe ya kufungua tovuti ya utalii kwa lugha ya Kichina ili kuwavutia watalii wengi zaidi wa China kuitembelea Kenya.
Kutokana na mkataba, Radio China Kimataifa itaanzisha kituo cha FM huko Nairobi, kitakuwa kituo cha kwanza cha FM kuanzishwa na serikali ya China barani Afrika, ambacho kitawawezesha wasikilizaji wa Kenya, hasa wa sehemu ya Nairobi kusikiliza sauti nyingi zaidi kutoka China, jambo hilo litazidisha maelewano kati ya watu wa China na Kenya.
Tarehe 21 mwezi Agosti rais Mwai Kibaki wa Kenya aliwasili mjini Nairobi baada ya kumaliza ziara yake ya siku tano nchini China. Kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Nairobi rais Kibaki alisema kuwa, ziara yake hii nchini China ilikuwa imepata mafanikio makubwa, alitoa shukrani nyingi kwa ukarimu wa serikali ya China na juhudi zake katika kuisaidia Kenya. Alisema kuwa, China inapata maendeleo siku hadi siku, na njia ya China ya kuendeleza uchumi imeweka mfano mzuri kwa Kenya na nchi nyingine zinazoendelea. Anatarajia kuwa, maingiliano na ushirikiano kati ya Kenya na China katika maeneo mbalimbali utapiga hatua kubwa zaidi.
2005-09-09 Idhaa ya Kiswahili
|