Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-09-16 19:34:13    
Wafanyabiashara binafsi wa China wanaojiendeleza katika nchi za Afrika

cri

Tangu China ianze kufanya mageuzi na kufungua mlango, maingiliano ya kiuchumi na kibiashara kati yake na nchi za Afrika yanaimarika siku hadi siku. Serikali ya China inawahimiza wanakampuni na wafanyabiashara wa China kuwekeza barani Afrika, ambao pia wanakaribishwa sana na nchi za Afrika kuwekeza vitega uchumi barani humo, ili kuhimiza maendeleo ya uchumi wa huko.

Katika sehemu ya biashara huria ya Kinshasa, mji mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, kuna maduka mengi yanayouza bidhaa za aina mbalimbali yanayoendeshwa na watu kutoka Lebanon, Japan, Korea ya Kusini, India, Pakistan na China. Wafanyabiashara wa China wamechukua nafasi kubwa katika sehemu hiyo kwa kuuza viatu, kofia, masanduku, nguo, mataulo, na mahitaji mengine ya kimaisha. Kwa jumla wafanyabiashara binafsi zaidi ya 500 wa China wanafanya biashara za aina mbalimbali mjini Kinshasa, ambao wengi wanatoka Beijing, Shanghai, Wenzhou na Chongqing.

Licha ya soko huria la Kinshasa, katika soko huria la biashara kwenye nchi nyingine nyingi, pia kuna wafanyabiashara kutoka China, kama vile soko la Kamwala la Lusaka, mji mkuu wa Zambia, na soko la Makato la Addis Ababa, mji mkuu wa Ethiopia. Wafanyabiashara wa China kwenye masoko huria hayo huanzisha biashara kwa mitaji midogo, na kujiendeleza kwa haraka kutokana na kufanya kazi kwa bidii na moyo wa kujituma.

Miongoni mwa wafanyabiashara wa China waliotangulia kufika barani Afrika mwanzoni mwa miaka ya 90 katika karne iliyopita, wengi wao wamewahi kuuza bidhaa ndogo ndogo kwenye soko huria, kama vile dawa za kuua viroboto na mende, dawa za kuchua, saa za kitarakimu, na nguo. Bwana Wang kutoka Beijing anayejulikana sana mjini Addis Ababa ndiye aliyeanza kwa kuuza dawa za kuuza viroboto.

Bwana Hu Herong aliyeanza biashara kwa kuendesha shamba kwenye kitongoji cha Lusaka, mji mkuu wa Zambia alitoka kijiji kimoja ambacho kiko nyuma kimaendeleo mkoani Henan. Ili kusaidia familia yake, Bwana Hu Herong alipaswa kuacha masomo baada ya kuhitimu tu shule ya sekondari ya chini, na kuanza kuuza matunda. Katika majira ya mchipuko ya mwaka 1991, Bw. Hu ambaye alikuwa bado hajafikia umri wa miaka 20 aliagana na jamaa zake akifuatana na mwanakijiji mwenzake kwenda Zambia. Baada ya kuchapa kazi kwa miaka 14, sasa Bw. Hu Herong amejiendeleza sana akijishughulisha na biashara za sekta nyingi kama vile kilimo, kuendesha mkahawa, kuuza vifaa vya ujenzi, kuendesha duka, na kushona nguo.

Bwana Wu Jiangtao aliyehitimu kutoka chuo kikuu cha usalama wa umma aliacha kazi nchini China mwaka 1992 na kwenda Zimbabwe na pesa za dola za kimarekani 2000 tu. Alisema kuwa, wachina wengi walishindwa kufahamu hali ilivyo ya Afrika, kwa kweli hali ya kiuchumi kwa baadhi ya nchi na sehemu za Afrika ni nzuri zaidi kuliko wachina wengi wanavyofikiria, zina uwezo mkubwa wa kibiashara. Bw. Wu Jiangtao alisafirisha bidhaa za China nchini Zimbabwe, na kuagiza sanamu za uchongaji za mawe na vitu vingine kutoka Zimbabwe kuuza nchini China. Sasa Bw. Wu Jiangtao amekuwa mfanyabiashara maarufu nchini Zimbabwe, hata chakula cha ndege maalum ya rais wa nchi hiyo kinatolewa na kampuni yake.

Katika nchi za Afrika kuna sekta nyingi zinazofaa kuendeshwa kwa kiwango kidogo, kama vile mashamba madogo, viwanda vidogo vya kutengeneza vyombo vya plastiki, malisho ya wanyama, kusindika mafuta, mikate na biskuti, kuunga vyombo vya umeme, baiskeli, pikipiki na kompyuta, au kuendesha studio ya kusafisha picha, kuchapisha kadi na kutoa nakala.

Hivi sasa wafanyabiashara wengi wa China wanaendesha mikahawa na kuuza nguo katika nchi za Afrika. Barani Afrika, kuna tofauti kubwa ya kiuchumi kati ya watu matajiri na maskini, mikahawa ya kichina inawavutia zaidi matajiri wanaochukua asilimia 10 ya idadi ya watu, lakini bidhaa za China zenye sifa bora na bei nafuu zinapendwa sana na asilimia 90 ya wakazi wa kawaida wa nchi za Afrika.

Idhaa ya Kiswahili 2005-09-16