Kutokana na muda kwenda na kutokea kwa maendeleo ya kasi ya sayansi na teknolojia ya kisasa, kati ya mifumo minne ya matibabu ya jadi iliyowahi kuleta athari kubwa kwa binadamu duniani, yaani matibabu ya kichina, matibabu ya kitibet, matibabu ya India ya kale na matibabu ya kiarabu ya kale, ni matibabu ya kichina na ya kitibet tu yaliyohifadhiwa kikamilifu hadi leo, na kupata maendeleo na uvumbuzi siku hadi siku, na kutoa mchango mkubwa katika kuwasaidia binadamu kupambana na magonjwa na kujenga mwili.
Chuo kikuu cha matibabu cha Tibet kiko karibu na sehemu ya hifadhi ya kimaumbile ya ardhi oevu ya Lalu mjini Lahsa. Naibu mkuu wa chuo kikuu hicho Bwana Chilai Wanjie anasema:
"Matibabu na dawa za kitibet ni sehemu moja muhimu ya utamaduni wa kabila la watibet, ambayo yamejifunza mambo mengi kutoka kwa matibabu ya kichina na ya India ya kale, na kuunda mfumo wake pekee kutokana na hali yake maalum ya kuwepo kwenye uwanda wa juu wa Tibet, matibabu ya kitibet yamekuwa na historia ya miaka 2800."
Bwana Chilai Wanjie alisema kuwa, katika zama hii ambapo matibabu ya kisasa yanaendelea kwa haraka sana, wakazi wa kabila la watibet bado wanaamini tiba ya kitibet kutokana na mfumo wake kamili na wa kipekee wa kutambua ugonjwa na kuutibu, mitishamba yote ya dawa za kitibet haina vitu vyenye uchafuzi.
"Ili kuendeleza matibabu na dawa za kitibet, serikali ya China imetoa sera ya kipaumbele katika kuokoa na kuendeleza utamaduni wa matibabu na dawa za kitibet, iliidhinisha kwa mahsusi na kuanzisha chuo kikuu cha matibabu ya kitibet miaka 12 iliyopita."
Hivi sasa, chuo kikuu cha matibabu ya kitibet kina wanafunzi zaidi ya 700 na walimu 140 hivi, kina kozi mbili za matibabu ya kitibet na dawa za kitibet, na kinaweza kuwaandaa wanafunzi wenye shahada ya pili. Hadi leo chuo kikuu hicho kimewaandaa madaktari elfu kadhaa kwa mikoa ya Tibet, Qinghai, Gangsu na Sichuan.
Zaidi ya hayo, chuo kikuu cha matibabu ya kitibet pia kimeanzisha kituo cha utafiti wa dawa za kitibet na kiwanda cha kutengeneza dawa za kitibet, ambacho kinaweza kutengeneza aina 24 za dawa zenye ufanisi maalum zinazotibu ugonjwa wa kisukari, na homa ya maini, na dawa nyingine zaidi ya 200 za kawaida. Pia kimefanya maingiliano na vituo vya utafiti na vyuo vikuu vya matibabu vya nchini na nchi za nje na sifa yake inajulikana duniani.
Katika hospitali ya Tibet, waandishi wetu wa habari walimkuta mgonjwa Langjie Chiren aliyeugua shinikizo la damu alipimwa na mkuu wa hospitali hiyo Bwana Gesan Pingcuo. Mgonjwa Chiren alipofika hospitali alijisikia kizunguzungu na kushindwa kupumua vizuri, mgongo wake ulikuwa unamwuma vibaya, hata alishindwa kutembea peke yake. Alisema kuwa, baada ya kupewa tiba ya kitibet kwa wiki tatu, sasa shinikizo lake la damu limeshuka na kutulia, anaweza kutembea mwenyewe. Anasema:
"Mkuu wa Hospitali hiyo Bwana Gesan licha ya kukagua wodi kila siku, kila akipata nafasi huzunguka na kuonana na wagonjwa na kuuliza hali ya maendeleo ya wagonjwa. Isitoshe, usimamizi wa hospitali hiyo na ustadi wa kuwatibu wagonjwa ni mzuri, nimeridhishwa sana."
Daktari wa kitibet si kama tu anatakiwa kuwa na uwezo wa kutambua ugonjwa na kutoa tiba kwa wagonjwa, bali pia anatakiwa kutambua na kutengeneza dawa za kitibet. Yaliyo tofauti ni kwamba, baada ya maendeleo ya miaka 1000, utengenezaji wa jadi wa dawa za kitibet umeacha njia ya kutumia mikono, na badala yake ni kuwa, hivi sasa dawa zinatengenezwa kwenye kiwanda cha kisasa. Kiwanda cha dawa za kitibet cha Qizheng cha Linzhi mkoani Tibet ni maarufu sana katika kutengeneza dawa za kitibet.
Mkuu wa kiwanda hicho Bwana Cairang Zhaxi alisema kuwa, njia sahihi ya kuendeleza dawa za kitibet za jadi ni kutumia teknolojia ya juu ya kisasa na kujiingiza katika soko huria. Anasema:
"Mafanikio ya dawa za chapa ya Qizheng kunategemea kuunganishwa kwa dawa za jadi za kitibet na mbinu ya utengenezaji wa kisayansi."
Bw. Cairang alisema kuwa, dawa za jadi za kitibet hutengenezwa kuwa vidonge, ambayo yana dosari kadhaa za kuathiri ufanisi wake. Hivi sasa wametumia teknolojia ya kisasa na kuongeza ufanisi wake ipasavyo.
Katika karakana ya kufunga dawa ya kiwanda cha dawa za kitibet cha Qizheng, waandishi wetu wa habari wameona aina tofauti za dawa kama vile dawa za vidonge, za unga, za kuchua na za kubandika. Dawa hizo zote zinatengenezwa na kufungwa kwa mitambo, mchakato wake unafanana na uzalishaji wa dawa za magharibi.
Idhaa ya kiswahili 2005-09-22
|