Mkoani Tibet kuna majengo mengi ya kale ya aina ya Kitibet yanayovutia watalii wengi. Majengo hayo ni sehemu muhimu ya utamaduni wa Tibet. Hivi sasa namna ya kuhifadhi na kudumisha majengo hayo ni suala muhimu sana.
Bw. Choekyi Gyaltsen alishughulika na tatizo hilo kwa miaka mingi, na sasa ni mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Majengo ya Kale ya Kitibet. Bwana huyo alizaliwa mwaka 1948 katika ukoo wa kabila la Watibet mkoani Sichuan. Alipokuwa mtoto alikuwa kama wengi wengine alipata elimu ya madhehebu ya Kitibet ya Dini ya Buddha katika shule ya dini. Alipokuwa na miaka 18 alikuwa anafanya kazi ya ujenzi. Kutokana na hamu yake na kazi ya ujenzi, alijitahidi kujifunza ufundi wa ujenzi na lugha ya kawaida ya Kichina, akawa fundi mwenye kufahamu lugha mbili za Kitibet na Kichina. Kutokana na juhudi zake alichaguliwa na chuo cha usanifu wa majengo. Alipokuwa anasoma matokeo yake ya mtihani yalikuwa yanaongoza. Baada ya kuhitimu, alichaguliwa na Taasisi ya Utafiti wa Majengo ya Kitibet. Alisema, "Mwanzoni nilipatia uzoefu kutoka kwa mafundi na kusoma katika chuo, kisha nilijiendeleza kwa kujisomea. Utamaduni niliopata katika shule ya dini ulinisaidia sana katika ujuzi wangu wa majengo ya kale ya Kitibet."
Kuanzia mwaka 1980 aliongoza kikundi cha watafiti kufanya uchunguzi wa makini kwa majengo yote ya kale ya Kitibet, na ramani za majengo yote hayo, ikiwa ni pamoja na kasri la Potala, majumba ya utawa ya Jokhang na Norbu Lingka, na ramani hizo zilichapishwa kwenye vitabu. Mpaka sasa idara nyingi ikiwemo Idara Kuu ya Mambo ya Kale ya China zinaendelea kutumia vitabu hivyo. Ni sawa kusema kuwa Bw. Choekyi Gyaltsen na wenzake wametoa mchango mkubwa katika kuhifadhi majengo ya kale ya Kitibet.
Serikali ya China inatilia maanani sana hifadhi ya majengo ya kale ya Kitibet, na mara nyingi ilitenga fedha kwa ajili ya ukarabati. Mwaka 1987 Bw. Choekyi Gyaltsen alipewa jukumu la kurudisha kama zamani jengo la jumba la utawa la Samye. Jengo hilo lilijengwa katika karne ya nane, ni jumba lenye historia ndefu zaidi kati ya majengo yote ya kale ya Kitibet. Ndani ya jumba hilo kuna picha za ukutani na sanamu, ni moja ya hazina za utamaduni wa kabila la Watibet.
Kutokana na kuwa jumba hilo limeharibika vibaya sana, na ramani ya usanifu wa jumba hilo haipatikani, kitu kilichotegemewa kilikuwa ni picha tu iliyopigwa katika miaka ya 40 ya karne iliyopita. Bw. Choekyi Gyaltsen aliwatembelea wazee wengi na alisoma vitabu vingi, mwishowe alifanikiwa kutengeneza ramani ya jengo hilo. Ili awafahamishe wazee wa dini jengo litakavyokuwa baada ya kujengwa, alitengeneza sampuli yake. Alisema, "Wazee walipoona sampuli hiyo walisisimka na kusema, 'Hilo ndilo jengo tunalofikiri!"
Bw. Choekyi Gyaltsen aliongoza mafundi wake kukamilisha jengo hilo. Waumini wa dini na wataalamu wa majengo ya kale wanalisifu sana jengo hilo. Mpaka sasa sampuli aliyotengeneza iko ndani ya jumba hilo la Samye. Tokea hapo alishiriki kwenye ukarabati wa majengo mengi ya kale ya Kitibet.
Bw. Choekyi Gyaltsen alieleza kuwa majengo ya jadi ya Kitibet yanagawanyika katika aina ya makasri, makazi, hekalu na majumba ya watawa. Majengo hayo yamekusnya elimu nyingi za ufundi, na majengo hayo yote yanajengwa kutokana na hali ya mazingira yalipo. Alisema, "Majengo ya kale ya Kitibet, sio tu yana mtindo wake pekee katika utamaduni wa majengo ya taifa la China, pia yana mtindo usiopatikana duniani. Kuanzia marne ya 21 wasanifu wanatilia maanani ujenzi ulingane na mazingira ya kimaumbile, na majengo ya jadi ya Kitibet yana sifa hiyo,yana thamani kubwa kwa ajili ya utafiti wa majengo ya kale duniani."
Hivi sasa licha ya kuendelea na kushughulika na ukarabati wa majengo ya kale ya Kitibet, naye pia anafundisha katika Chuo Kikuu cha Uhandisi cha Tibet. Alisema, hivi sasa tatizo kubwa ni upungufu wa wataalamu wa majengo hayo, lakini hifadhi ya majengo hayo haitakuwa tena tatizo kama kukiwa na wataalamu wa kutosha.
Idhaa ya kiswahili 2005-09-26
|