tarehe 2 mwezi Agosti mwaka huu, msichana Cirenzhuoma wa Tibet alijifungua salama mtoto wake wa kwanza. Usiku wa siku ya pili, mwandishi wetu wa habari alimwona katika hospitali ya wanawake na watoto ya sehemu ya Linzhi mkoani Tibet, alionekana amepona kiasi na alikuwa anamwangalia mtoto wake wa kike aliyelala karibu yake. Karibu na kitanda chake, kuna vitanda viwili vidogo ambavyo mume na mama yake walilala pale ili kuweza kumsaidia wakati wa usiku.
Bi. Zhuoma anaishi kwenye tarafa ya Bujiu katika wilaya ya Linzhi, ambayo iko umbali wa kilomita 40 kutoka hospitali hiyo. Bi. Zhuoma alisema,
"nilipokuwa mja mzito, baada ya kufanyiwa uchunguzi, niligunduliwa kuwa na dalili ya kukabiliwa na hatari, basi nikapewa matibabu hapa na kupona. Nimeanza kuwepo hapa hospitali katika siku za karibuni. Gharama siyo kubwa, tunaweza kumudu."
Bi. Zhuoma alisema kuwa, mtoto wake amepewa chanjo ya ugonjwa wa ini na kifua kikuu, mbali na hayo, pia alipewa ratiba ya kupewa chanjo za aina mbalimbali. Bi. Zhuoma alisema kuwa, baada ya kurudi nyumbani, atapeleka ratiba hiyo kwenye kituo cha huduma za afya cha tarafa, daktari wa kituo hicho watamkumbusha kwa wakati kumpeleka mtoto kupewa chanjo. Kutokana na mila za watibet, pia atakwenda kwenye hekalu la lama na kuomba jina la mtoto wake.
Mbali na Bi. Zhuoma, kuna wajawazito wengine 8 kwenye hospitali ya wanawake na watoto ya Linzhi. Wote wameacha desturi ya kujifungulia nyumabani, bali wamechagua kujifungulia hospitalini kutokana na msaada wa serikali.
Mkuu wa hospitali hiyo Bi. Cuoyong ni mwanamke mwenye umri wa miaka 30. alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa, hospitali hiyo ina vitanda 30 vya wagonjwa, na pia ina vifaa vingi vya aina mbalimbali. Katika miaka ya hivi karibuni, idadi ya wajawazito wa Tibet wanaokwenda kujifungulia kwenye hospitali hiyo imeongezeka mwaka baada ya mwaka. Katika mwaka 2004, kulikuwa na wajawazito 180, na kuanzia mwezi Januari hadi mwezi Julai mwaka huu, idadi hiyo imefikia 160, ikiwa ni asilimia 85 ya idadi ya jumla ya mwaka jana.
Bi. Cuoyong alieleza sababu ya wanawake waTibet wengi kuchagua kujifungulia hospitalini,
"Kutokana na kuwa tumeeneza mara kwa mara sera ya taifa ya uzazi wa mpango kwenye sehemu zote za wafugaji, na kutoa huduma za afya kwa wanawake na watoto, uzazi wa mpango na afya ya uzazi, pamoja na serikali kuendelea kuongeza fedha kwa ajili hayo, sera nyingi zenye manufaa zinawahamasisha wanawake kujifungulia hospitalini. Kwa mfano, wanawake wafugaji wakizaa watoto kwenye hospitali, watapewa msaada, pamoja na nguo na taulo kwa watoto wachanga."
Shughuli za huduma za afya kwa wanawake na watoto zilianzishwa rasmi kwenye mkoa wa Tibet katikati ya miaka ya 80 ya karne iliyopita. Baada ya juhudi za miaka 20, hivi sasa hospitali za wanawake na watoto zimejengwa kila sehemu mkoani Tibet, aidha, kwenye kila hospitali ya tarafa au wilaya, kuna madaktari wanaowajibika na huduma za afya kwa wanawake na watoto.
Msichana Zhen Dan wa kabila la waTibet mwenye umri wa miaka 28 ni daktari wa hospitali ya tarafa ya Bujiu anayehusika na huduma za afya kwa wanawake na watoto. Tarafa hiyo ina vijiji 13, na wafugaji na wakulima zaidi ya 2400. ili kumsaidia Zhen Dan kujifunza ujuzi kuhusu afya ya wanawake na watoto, hospitali hiyo iliwahi kumpeleka kwenye mkoani Jiangsu na Sichuan kusoma kwa miaka 5. Zhen Dan alipozungumzia kazi yake, alisema,
"zamani watu wa huku walikuwa hawataki kwenda kujifungulia hospitali, wala kufanyiwa uchunguzi wa afya zao. Lakini nilishikilia na kuwashawishi waje hospitalini, pia tulienda kwenye kila kijiji ili kuandikisha nani amekuwa mjamzito na nani amekaribia kujifungua."
Imefahamika kuwa, pamoja na maendeleo makubwa ya huduma za afya kwa wanawake na watoto, idadi ya vifo vya wajawazito na watoto wachanga imepungua dhahiri mkoani Tibet. Kwa mfano, ikilinganishwa na mwanzoni mwa miaka ya 50 ya karne ya 20, kiasi hicho kimepungua kutoka asilimia 5 hadi kufikia asilimia 0.31.
Ingawa mafanikio makubwa yamepatikana, lakini kutokana na Tibet kuwa na eneo kubwa na idadi kubwa ya watu, mawasiliano magumu na upungufu wa wataalam, hivi sasa kazi ya utoaji wa huduma za afya kwa wanawake na watoto bado ina kasoro kadhaa. Kwa ajili hiyo, sehemu mbalimbali za Tibet zimechukua hatua mbalimbali kuimarisha kazi hiyo.
Kwenye sehemu ya Shannan iliyoanzisha utamaduni wa kitibet, ili kuinua kiwango cha huduma za afya kwa wanawake na watoto katika kila tarafa na wilaya, serikali ya sehemu hiyo ilichukua hatua ya kuunganisha kazi ya kuandaa wataalam na kutoa misaada ya kiufundi. Mkurugenzi wa kitengo cha ukunga katika Hospitali ya Umma ambayo ni hospitali kubwa kabisa kwenye sehemu hiyo Bi. Cangjuezhuoma alieleza,
"kila mwaka hospitali yetu hupeleka madaktari kwenye kila wilaya, na kuwafundisha wahudumu wa afya kwenye ngazi ya shina kuhusu kuwatibu watoto wachanga, na kushughulikia matatizo ya wanawake wakati wa kujifungua."
Imefahamika kuwa, ili kuinua zaidi kiwango cha huduma za afya kwa wanawake na watoto kwenye sehemu hiyo, mkoa unaojiendesha wa Tibet umeweka mpango wa mradi wa ujenzi wa zahanati za wanawake na watoto, kujitahidi kujenga mfumo kamili wa huduma za afya kwa wanawake na watoto ndani ya miaka 5 ijayo, aidha, sehemu hiyo pia itaanzisha ujenzi wa mfumo wa huduma za afya kwa wajawazito na watoto chini ya umri wa miaka 7, kufuata utaratibu wa kufanya uchunguzi kabla ya wajawazito kujifungua, na kuwatembelea baada ya kujifungua, ili kusukuma mbele maendeleo kamili ya huduma za afya kwa wanawake na watoto katika mkoa wa Tibet.
|