Wanafunzi 137 wa Chuo Kikuu cha Sayansi ya Kilimo cha Kaskazini Magharibi, ambao bado wanaendelea na masomo, hivi karibuni walialikwa kufanya kazi kama wasaidizi wa mkurugenzi wa kamati ya wakazi mkoani Shaanxi, watashughulikia vijiji 71 na sehemu 4 za wakazi.
Wanafunzi hao 137 waliochaguliwa kutoka wanafunzi 537, wote ni mahodari na wenye ujuzi mkubwa, wakiwemo wanafunzi wanaosomea kilimo, misitu, maji, mambo ya bustani, upashanaji wa habari, vyakula, mazingira, uchumi na sayansi ya wanyama.
Wanafunzi hao wakiwa makada wa sehemu hiyo wanakwenda vijijini mara moja kwa wiki, kushiriki kwenye uthibitishaji wa uamuzi kuhusu shughuli za sehemu hiyo, kutumia ujuzi wao katika kueneza sayansi na teknolojia ya kilimo vijijini, kuwasaidia wakulima watumie sayansi na teknolojia ya kisasa katika kilimo na kuwasaidia wakazi wenye matatizo ya kiuchumi, na kuwaburudisha wakazi kwa maonesho mbalimbali.
Wanafunzi hao wanasema kuwa wanaithamini fursa hiyo, watatumia ujuzi na busara zao katika kuongeza uzalishaji wa kilimo, kuongeza mapato ya wakulima na kuendeleza vijiji.
Katika miaka ya karibuni, wanafunzi wengi wanaohitimu kutoka vyuo vikuu wana shida kubwa katika kupata ajira, lakini wanafunzi wanaohitimu kutoka shule za ufundi mjini Harbin hawana shida kama hiyo, bali wana nafasi nyingi za ajira.
Mkuu wa Shule ya Ufundi ya Ngazi ya Juu ya Harbin alifahamisha kuwa, kabla wanafunzi wa shule hiyo hawajahitimu, viwanda vikubwa na vya wastani vinakuja kuchagua wafanyakazi wao kati ya wanafunzi hao.
Wanafunzi wa shule nyingine ya ufundi, yaani Shule ya Ufundi ya Biashara mkoani Heilongjiang, wote wamaahidiwa kupata ajira baada ya kuhitimu.
Idara ya nguvukazi ya mkoa wa Heilongjiang imefahamisha kuwa, hivi sasa kuna shule 28 za ufundi mjini Harbin, kwa jumla zina wanafunzi elfu 18, na wanafunzi 3500 waliohitimu mwaka huu wameajiriwa na viwanda mbalimbali.
Kwa nini viwanda vinapenda kuwaajiri wanafunzi wanaohitimu kutoka shule za ufundi? Wataalamu wanaeleza kuwa, wanafunzi hao wanajua vizuri kutumia elimu waliyoipata kwenye katika uzalishaji; hawana majivuno, wanaweza kuvumilia kazi ya ufundi ambayo ni kazi ya kuchosha, wala hawana tabia ya kuhamahama kutoka kiwanda kimoja hadi kingine; na sababu nyingine ni kuwa viwanda vinaweza kuwaajiri wanafunzi hao kwa mishahara isiyo mikubwa.
Mkoa wa Shaanxi utasamahe kabisa mikopo ya wanafunzi wa vyuo vikuu, ambao wanajitolea kwenda vijijini na sehemu maskini kufanya kazi kwenye shule na hospitali za huko na kusaini mikataba ya miaka mitano au zaidi. Hii ni sera iliyotolewa na mkoa wa Shaanxi hivi karibuni ili kuwahamasisha wanafunzi wanaohitimu kutoka vyuo vikuu wafanye kazi kwenye mashina.
Sera hiyo inaeleza wazi kuwa, mkoa huo utatoa misaada kwa wanafunzi 1000, kila mwanafunzi atapewa msaada wa yuan za Renminbi elfu 6 kwa mwaka, baada ya wanafunzi hao kuhitimu, wakijitolea kwenda kufanya kazi vijijini na kusaini mikataba ya kazi ya miaka 6 au zaidi, hawatalazimika kurudisha misaada hiyo, isitoshe, watapewa yuan nyingine za renminbi elfu 30.
Sera hiyo ya mkoa wa Shaanxi siyo tu inaweza kuwasaidia wanafunzi wanaohitimu kutoka vyuo vikuu, bali pia inaweza kutatua tatizo la upungufu wa wataalamu vijijini na sehemu maskini.
Idhaa ya Kiswahili 2005-09-28
|