Kuanzia tarehe 15 hadi 29 Septemba, ujumbe wa Radio China kimataifa ulifanya ziara ya kikazi nchini Kenya, Tanzania na Zimbabwe, ambapo ulikutana na viongozi, maofisa na wataalamu husika wa Shirika la utangazaji la Kenya, KBC, Taasisi ya utangazaji ya Tanzania, na Radio Tanzania, Zanzibar, pande mbili mbili zilifikia makubaliano kuhusu ushirikiano katika sekta ya habari.
Makubaliano yaliyofikiwa kati ya Radio China kimataifa na Radio Tanzania Dar es Salaam na Radio Tanzania Zanzibar kuhusu kukubali matangazo ya idhaa ya Kiswahili ya Radio China kimataifa yarushwe hewani kwa kupitia masafa ya FM ya Radio Tanzania Dar es Salaam na Radio Tanzania Zanzibar yakitekelezwa yatawafurahisha wasikilizaji wetu wengi walioko nchini Tanzania.
Sasa tunawaletea maelezo kuhusu mkutano kati ya ujumbe wa Radio China kimataifa na wasikilizaji wa CRI walioko Nairobi, Kenya.
Tarehe 16 Septemba, wasikilizaji wa Radio China kimataifa walioko Nairobi walikusanyika pamoja kwenye Bustani ya China iliyoko katika sehemu ya Gigiri, Nairobi, ambao walibadilishana maoni na ujumbe wa Radio China kimataifa ulioongozwa na Naibu mkurugenzi mkuu wa Radio China kimataifa Bwana Chen Minyi, wajumbe wa ujumbe huo ni pamoja na mama Chen, mkurugenzi wa idhaa ya Kiswahili ya CRI, na wakurugenzi wa idara ya habari ya nchini ya CRI na idara ya kazi ya wasikilizaji, na katibu wa mawasiliano na nje wa idara ya wataalamu ya CRI. Balozi wa China nchini Kenya Bwana Guo Chongli siku hiyo pia alihudhuria mkutano huo.
Balozi Guo Chongli alipotoa hotuba aliipongeza Radio China kimataifa kwa juhudi zake za kuandaa vipindi vinavyokaribishwa sana na wasikilizaji wa Afrika, wakiwemo wa Kenya. Alisisitiza kuwa vipindi vya Radio China kimataifa vinavyorushwa kupitia shirika la utangazaji la Kenya KBC vimewapa wasikilizaji wa Kenya chaguo lingine la kuelewa mambo ya mashariki ya dunia, jambo hilo linasaidia sana kuongeza maelewano kati ya watu wa China na wa Afrika.
Anasema vipindi vya Radio China kimataifa si kama tu vinawafahamisha wasikilizaji habari zinazotokea nchini China na duniani, na maelezo baada ya habari, bali pia vinawafahamisha historia na utamaduni wa jadi wa China, pamoja na kipindi cha kujifunza lugha ya kichina. Alieleza imani yake kuwa, marafiki wa nchi za Afrika wanaweza kujua mambo mengi zaidi kuhusu dunia hii baada ya kusikiliza vipindi vya Radio China kimataifa, na Radio China kimataifa pia itaongeza juhudi zake katika kuwahudumia wasikilizaji wake walioko barani Afrika.
Naibu mkurugenzi mkuu wa Radio China kimataifa Bwana Chen Minyi aliwajulisha wasikilizaji hali ya Radio China kimataifa na mpangilio wa vipindi vyake, alisema kuwa ikiwa ni radio ya serikali kuu, Radio China kimataifa kila siku inatangaza vipindi kwa lugha 43 zikiwemo lugha 38 za kigeni na nyingine za sehemu mbalimbali za China, na jumla ya muda wa matangazo yake kwa siku ni zaidi ya saa 400. Vipindi vya Radio China kimataifa vinakaribishwa sana na wasikilizaji wake duniani. Mwaka jana Radio China kimataifa ilipata barua zaidi ya milioni 1.8 kutoka kwa wasikilizaji wake walioko sehemu mbalimbali duniani.
Bwana Chen alisema kuwa, Radio China kimataifa inatilia maanani sana kukuza urafiki kati yake na wasikilizaji wa nchi za Afrika. Tangu kuanzishwa kwa uhusiano wa kibalozi kati ya China na nchi za Afrika, Radio China kimataifa imeanzisha matangazo ya lugha ya Kiswahili na kihausa, hasa lugha ya Kiswahili ambayo ni moja ya lugha kubwa kabisa za kienyeji barani Afrika. Licha ya kutangaza vipindi vyake kwenye masafa mafupi, kuanzia mwaka 2002, Radio China kimataifa pia imeanza kutangaza vipindi vya Kiswahili na kiingereza kwa kupitia kampuni ya MIH ya Afrika ya kusini na Shirika la utangazaji la Kenya KBC.
Bwana Chen Minyi aliwafahamisha wasikilizaji wetu kuwa, kutokana na makubaliano kati ya serikali ya China na Kenya, Radio China kimataifa itajenga kituo chake cha FM huko Nairobi Kenya, kituo hicho kikikamilika, muda wa vipindi vya lugha mbalimbali vya Radio China kimataifa vitakavyotangazwa huko Nairobi vitaongezwa kufikia saa 20 kwa siku, wasikilizaji wetu wa Kenya watasikiliza vizuri zaidi matangazo ya Radio China kimataifa.
Wasikilizaji wa Kenya waliohudhuria mkutano huo wote walipiga makofi kushangilia habari hiyo nzuri. Na walitoa maoni yao moja baada ya mwingine. Wakisema kuwa wanafuarahia sana muda wa matangazo ya idhaa ya Kiswahili ya Radio China kimataifa ulioongezwa kuwa saa moja kuanzia tarehe 1 Septemba, na wameishukuru Radio China kimataifa kufuatilia sana kuwasiliana na wasikilizaji wake wa Afrika.
Wasikilizaji wapendwa, wiki ijayo tutaendelea kuwaletea maelezo kuhusu ujumbe wa Radio China kimataifa uliofanya ziara ya kikazi nchini Kenya, Tanzania na Zimbabwe.
|