Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-10-05 17:49:02    
Tekenolojia ya kuleta joto ndani ya nyumba kwa kutumia joto la ardhini yaenezwa hatua kwa hatua nchini China

cri

Hivi sasa majira ya joto yamekwisha, na siku za baridi zitawadia ambapo watu watatumia kiyoyozi au chombo cha kuleta joto katika kupambana na baridi kali, lakini vilevile vyombo hivyo hutumia nishati nyingi, na kuwafanya watu watoe malipo makubwa ya matumizi ya umeme. Hivi sasa, tatizo hilo limetatuliwa kwenye baadhi ya sehemu za Beijing, watu wa huko wanatumia joto la ardhi kwa kudhibiti joto la nyumbani.

Majira ya China ni tofauti na ile ya Tanzania, hivi sasa nchini China majira ya joto yamekwisha na majira ya baridi yanakaribia, mwezi mmoja uliopita, joto kali na unyevunyevu mjini Beijing uliwafanya wakazi wa Beijing wasijisikie vizuri, lakini wakati mwandishi wetu wa habari alipoingia kwenye jengo la Huaxia lililopo kwenye sehemu ya magahribi ya mji wa Beijing, alisikia upepo ukivuma, upepo huo haukuletwa na kiyoyozi, bali jengo hilo linatumia teknolojia ya kutumia joto la ardhini kwa kuleta joto nyumbani. Siyo tu katika majira ya joto, bali pia hata katika majira ya baridi ya mwaka jana, teknolojia hiyo iliwapatia wafanyakazi wa jengo hilo joto la kutosha.

Kampuni ya Huaqing ni kampuni yenye uzoefu mkubwa katika kutumia joto la ardhini, meneja wa kampuni hiyo Bw. Huang Xueqin alisema kuwa, sehemu fulani yenye kina kirefu ardhini joto lake linadumu kuwa kati ya nyuzi 15 na 18 na halibadiliki kwa mwaka mzima, na joto la sehemu hiyo ya ardhini linaweza kutumika. Alisema, joto la ardhini linaweza kupatikana kwa njia mbili, ya kwanza ni kwa kuchimba visima na kutumia maji ya joto ya chini ya ardhi, nyingine ni kutandika mabomba chini ya ardhi ili kutumia moja kwa moja joto la ardhini. Lakini njia ya kwanza inazuiliwa na masharti magumu, yaani huwezi kuchimba visima kila sehemu, aidha, wafanyakazi wanatakiwa kurudisha maji ardhini baada ya kutumia joto lake, ili kubana matumizi ya maji. Njia ya pili, kutandika mabomba ardhini kwa kupata joto la ardhini, ni rahisi zaidi kutekelezwa, na jengo la Huaqing ni kutumia linatumia njia hiyo kupata joto kutoka ardhini. Bw. Huang Xueqin alisema:

"Tunatakiwa kuchimba visima vyenye kimo cha mita 100 au 120, na vyenye kipenyo cha sentimita 15, na tunaweka mabomba yenye umbo la U ndani ya visima hivyo, na kuvifunika. Maji ya chini ya ardhi yanazunguka kwenye mabomba hayo, na joto la maji linapatikana wakati maji yanapopita kwenye mabomba hayo. Kwani joto la maji hayo ni dogo kuliko joto la hewa katika majira ya joto, tukiwa ndani hatusikii joto, kadhalika, wakati wa majira ya baridi, hatuoni baridi kwa sababu joto la maji hayo ni kubwa zaidi kuliko joto la hewa."

Katika miaka ya karibuni, baadhi ya hoteli, mikahawa na majengo ya makazi ya hapa Beijing yamenufaika kwa kutumia teknolojia hiyo.

Mtaa wa Beiyuan wa Beijing ni mtaa mkubwa zaidi unaotumia joto la ardhini, wakazi wa mtaa huo wananufaika na matumizi ya joto la ardhini. Bibi Wangyao alihamia kwenye mtaa huo mwaka mmoja uliopita, alimwaambia mwandishi wetu wa habari akisema:

"Hivi sasa tunatumia joto la ardhini kuleta joto la nyumbani, hivyo kiyoyozi cha nyumbani kwangu hakitumiki tena, na bila ya kiyoyozi, nyumba yangu inakuwa na nafasi zaidi."

Mhandisi mkuu wa Idara ya Upimaji wa Ardhi Bw. Ran Weiyan alipohojiwa na mwandishi wetu wa habari alisema kuwa faida, kubwa ya kutumia joto la ardhini ni kubana matumizi ya nishati. Alisema:

"Kiyoyozi kinatumia joto la hewa ya nje kuleta joto nyumbani, lakini kama ifikapo majira ya baridi, hewa ya nje yenyewe ni baridi sana, kiyoyozi hakiwezi kufanya kazi kwa ufanisi. Lakini joto la maji ya chini ya ardhi halibadiliki kwa mwaka mzima, na ni rahisi kupatikana na kutumika."

Bw. Sun Yan anayeshughulikia mambo ya mtaa wa Beiyuan, alisema, wakazi wa mtaa huo wamenufaika sana tangu waanze kutumia joto la ardhini:

"Wakazi wa hapa wameridhishwa na faida ya kiuchumi tangu joto la ardhini lianze kutumika kwenye mtaa huo, kwani njia hiyo imebana matumizi ya nishati, hivyo gahrama ya umeme imepungua kwa kiasi kikubwa."

Bw. Huang Xueqin wa kampuni ya Huaqing alisema kuwa, joto la ardhini ni nishati mbadala nzuri, halileti uchafuzi wowote kwa mazingira, alisema:

"Nishati hiyo ni safi, inatoka kwenye maji ya chini ya ardhi, hata maji hayo yanahifadhiwa vizuri, hivyo kutumia joto la ardhini kunaambatana na mwito wa taifa wa maendeleo endelevu."

Hivi sasa, Mpango wa Kutumia Joto la Ardhini Mjini Beijing wa Karne ya 21 umetolewa, kwenye mpango huo. Serikali ya Beijing imethibitisha sehemu zinazotumia au zitakazotumia joto la ardhini, eneo la jumla la sehemu hizo limezidi mita za mraba milioni 13. Tarehe 1 mwezi Januari mwaka 2006, sheria ya kwanza ya nishati inayoweza kutumika tena itatolewa rasmi, kwa mujibu wa sheria hiyo. Serikali itatenga fedha maalum kwa ajili ya kuunga mkono shughuli za kutumia nishati inayoweza kutumika tena, teknolojia hiyo ya kutumia joto la ardhini kuwa kuleta joto nyumbani itaenezwa zaidi nchini China.