Bw. Patrick Mutume mwenye umri wa miaka 47 ni ofisa wa Idara ya utangazaji ya Wizara ya upashanaji habari ya Zimbabwe. Mwezi Julai, mwaka huu?alipokuwa masomoni nchini China, alipata ugonjwa wa ghafla, ambao ulimfanya atokwe na damu kwenye sehemu kubwa ya kichwa chake. Baada ya juhudi za siku 50 zilizofanywa na madaktari wa China, maisha ya Bw. Patrick ambaye alikuwa hatarini kufa yaliokolewa. Serikali ya Zimbabwe ilishukuru sana msaada wa China, na rais Robert Mugabe alitoa shukurani kwa China.
Siku moja ya mwezi Septemba?balozi wa Zimbabwe nchini China Bw. Christopher Hatikuri Mutsvangwa alitangaza kwa furaha kwenye Hospitali ya Tiantan ya Beijing kuwa, madaktari wa China wamefanikiwa kuokoa maisha ya ofisa wa Zimbabwe Bw. Patrick Mutume. Alitoa shukrani za dhati kwa serikali na watu wa China, akisema:
"Niko hapa kwa ajili ya kushukuru misaada ya kibinadamu ya serikali na watu wa China, nashukuru kwa kuwa mmeweza kuokoa maisha ya Bw. Patrick Mutume. Sasa Bw. Patrick Mutume yupo kipindi cha kupata nafuu, na kuweza kurudi Zimbabwe."
Bw. Patrick alikuja Beijing tarehe 5, mwezi Julai, kushiriki kwenye Semina ya maofisa wa Idara ya usimamizi ya Radio na Televisheni ya mwaka 2005" iliyoendeshwa na Wizara ya Biashara kwa ajili ya maofisa wa nchi zinazoendelea. Hiyo ni moja kati ya semina mbalimbali zinazoandaliwa na China kwa ajili ya kutoa misaada kwa nchi za nje. Katika miaka ya hivi karibuni, China imekuwa ikitilia mkazo uendelezaji na ushirikiano na nchi zinazoendelea kwenye sekta ya kuwaandaa wataalamu, na watu kutoka nchi za nje kushiriki kwenye semina na mafunzo mbalimbali nchini China wanazidi kuongezeka. Mwaka 2004, zaidi ya waafrika 1600 walishiriki kwenye semina ya Wizara ya Biashara ya China.
Siku ya pili baada ya Bw. Patrick kuja China, wakati alipokuwa kwenye ufunguzi wa semina alianza kutokwa na damu kichwani, na maisha yake yalikuwa hatarini. Aliyekuwa mkuu wa semina hiyo ambaye ni meneja mkuu wa Kampuni kuu ya Ushirikiano wa Kimataifa wa uchumi na teknolojia ya Radio na Televisheni ya China Bw. Cheng Lin alishuhudia kila kitu kilivyokuwa. Akisema:
"Kwenye ufunguzi huo, Bw. Patrick alikuwa mtu wa saba kutoa hotuba. Hotuba yake ilikuwa nzuri, alitoa shukurani kwa semina hiyo, na kutaka kufahamiana na marafiki wengi zaidi. Ufunguzi ulipomalizika, watu walijiandaa kupiga picha ya pamoja, lakini Bw. Patrick alikuwa bado amekaa, alisema hawezi kuinua miguu yake kutokana na uchovu wa safari ndefu. Lakini alishindwa kunywa maji. Wakati huo, niliona hali ni ya hatari, nikaamua kupiga simu ya dharura kuomba gari la wagonjwa lije!"
Gari la wagonjwa lilifika kwa wakati. Baada ya kupimwa kwa hatua ya mwanzo, aligunduliwa kuwa shinikizo lake la damu lilikuwa juu sana, na alipelekwa kwenye Hospitali ya Tiantan ya Beijing, ambayo ni hospitali maarufu inayotoa matibabu ya ugonjwa wa mishipa ya damu ya moyo na kichwa nchini China. Akiwa njiani kuelekea hospitali, daktari aliambiwa kuwa, Bw. Patrick alikuwa na ugonjwa wa shinikizo kubwa la damu kwa miaka mitano, lakini hakutumia dawa yoyote, kila alipokuwa anashindwa kufanya alilazwa kitandani tu. Kutochukua hatua yoyote kudhibiti hali ya ugonjwa wake ni chanzo muhimu cha kutokea kwa ugonjwa huo ghafla.
Baada ya kufika Hospitali ya Tiantan, madaktari walithibitisha mara moja kuwa Bw. Patrik alitokwa na damu kichwani kutokana na ugonjwa wa shinikizo kubwa la damu. Ugonjwa huo ni hatari sana na unaweza kusababisha kifo, tena ni vigumu kutibiwa. Wakati huo huo, Patrick alitokwa na damu kwa kiasi kikubwa. Kutokana na uzoefu wa madaktari, mtu akiwa na hali hiyo, uwezekano wa kupoteza maisha kutokana na ugonjwa huo ni asilimia 100. Daktari Zhang Xingquan wa Hospitali ya Tiantan ya Beijing anasema:
"Hali ya mgonjwa huyo ilikuwa mbaya sana, hata pumzi yake ilisimama kwa muda. Tulimpeleka mara moja kwenye Chumba cha wagonjwa mahututi. Baada ya hatua za uokoaji, hali yake ilidhibitiwa kimsingi."
Baada ya hali ya ugonjwa kudhibitiwa kimsingi, Hospitali ya Tiantan ilimweka Bw. Patrick kwenye chumba cha wagonjwa mahututi. Kwenye chumba hicho, wataalamu walishiriki kwenye kazi ya matibabu, na kumwokoa Bw. Patrick kutoka kwenye hali mbalimbali za hatari. Baada ya siku 49, Bw. Patrick aliokolewa.
Daktari Wang Chunxue anasema: "Ni watu wachache sana wanaoweza kuokolewa kama ilivyokuwa kwa Bw. Patrick. Yeye ni mtu mwenye imani kubwa na kutoa ushirikiano mzuri katika hatua ya matibabu."
Baada ya kupata fahamu, Bw. Patrick aliwekwa kwenye chumba cha hali ya juu. Kutokana na Bw. Patrick kutozoea chakula cha kichina, hospitali alimwajiri mpishi anayeweza kupika chakula cha kimagharibi. Mbali na hayo, wagonjwa wengine walionesha moyo mwema kwa mgonjwa huyo mgeni. Siku moja Bw. Patrick alimwambia wauguzi kuwa anataka kula matufaa, wagonjwa waliokaa wadi nyingine walimletea mara moja. Aidha, viongozi wa Wizara ya biashara ya China na Kampuni kuu ya ushirikiano wa kiuchumi na teknolojia ya Radio na Televisheni ya China walimtembelea mara kwa mara, na kumtia moyo apate nafuu mapema.
Mbali na hayo, kuna jambo jingine lililomfurahisha sana Bw. Patrick. Baada ya Bw. Patrick kulazwa hospitali, Wizara ya biashara ya China ilimpokea mke wake kuja China kumtembelea. Tarehe 29, mwezi Agosti, mke wake alijifungua mtoto wa kiume. Hali hiyo ilimfurahisha sana Bw. Patrick mwenye binti wawili.
Wakati Bw. Patrick alipokuwa anatibiwa nchini China, Rais Mugabe wa Zimbabwe alitembelea China, na kutoa shukrani kwa Wizara ya Biashara ya China. Ubalozi wa Zimbabwe nchini China unaona kuwa, uokoaji wa China kwa Bw. Patrick unaonesha urafiki mwema wa China kwa waafrika.
Hivi sasa, Bw. Patrick na mkewe wamerudi Zimbabwe, na wamemwacha kwa muda mtoto wao kwenye hospitali ya Beijing. Bw. Patrick alisema kuwa, wanaamini sana kuwa madaktari wa China watamtunza vizuri mtoto wao. Baada ya kupanga vizuri maisha yao nchini kwao, mke wa Bw. Patrick atakuja Beijing tena na kumchukua mtoto wao na kurudi naye Zimbabwe.
Idhaa ya Kiswahili 2005-10-07
|