Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-10-11 20:35:55    
Ujenzi wa forodha wahimiza maendeleo ya uchumi na biashara ya nje ya Xinjiang

cri

Mkoa unaojiendesha wa Xinjiang Uigur ulioko sehemu ya kaskazini magharibi ya China unapakana na nchi nane zikiwa ni pamoja na Russia, Kazakhstan, Pakistan na India na ni mkoa wa unaopakana na nchi nyingi zaidi. Kwenye mpaka wa mkoa huo wenye urefu wa kilomita zaidi ya 5,600, zimejengwa forodha 17. Baada ya kuendelezwa kwa miaka mingi, forodha hizo zimekuwa njia za moja kwa moja za biashara na nchi za Asia ya kati na sehemu za pembezoni mwake. Hivi sasa Xinjiang imekuwa mstari wa mbele katika ufunguaji mlango kwa nje na umuhimu wa ujenzi wa forodha hizo wa kuhimiza maendeleo ya kasi ya mambo ya uchumi na biashara ya Xinjiang umekuwa dhahiri siku hadi siku.

Miongoni mwa forodha nyingi mkoani Xinjiang, ile inayojulikana zaidi ni forodha ya mlima wa Ala iliyoko sehemu ya kaskazini magharibi ya mkoa huo, ambapo kuna njia ya reli na barabara za kuingia Kazakhstan, forodha hiyo imekuwa pekee ya ngazi ya kwanza ya taifa kwenye sehemu ya kaskazini magharibi ya China. Kiongozi wa kamati ya usimamizi wa forodha ya mlima wa Ala Bw. You Zhanjun alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa, mizigo iliyopita kwenye forodha hiyo mwaka jana ilifikia tani milioni 9.4, forodha hiyo ilitoa fedha za ushuru kwa serikali Yuan za Renminbi zaidi ya bilioni 3 mwaka jana na kuwa forodha ya kwanza kupitisha bidhaa nyingi, kasi ya maendeleo na ufanisi mkubwa kwenye sehemu ya kaskazini magharibi ya China. Bw. You alisema,

"Mwaka 1994, tani laki 4.3 tu za mizigo zilipita kwenye forodha yetu, lakini ilipofika mwaka 1999 mizigo iliyopita ilifikia tani milioni 3.67 ambazo zilizidi uwezo wake wa usanifu. Tokea mwaka 2001, mizigo iliyopita kwenye forodha ya mlima wa Ala iliongezeka kwa 25% kwa mwaka, na inatazamiwa kuzidi tani milioni 11 mwaka huu."

Habari zinasema kuwa hivi sasa forodha hiyo inachukua nafasi ya pili kwa miaka 9 mfululizo kwa wingi wa bidhaa kupita miongoni mwa forodha 4 kubwa zenye njia ya reli. Tangu kuanza kazi?forodha hiyo imetoa fedha za ushuru Yuan zaidi ya bilioni 13 kwa serikali. Takwimu mpya zinaonesha kuwa katika miezi 8 ya mwanzo ya mwaka huu, mizigo iliyopita kwenye njia ya reli ya forodha hiyo imezidi tani milioni 7 likiwa ni ongezeko la 20% kuliko mwaka jana katika kipindi kama hiki.

Pamoja na kupanuka kwa uwezo wa kupita kwa mizigo, wasimamizi wa forodha hiyo katika miaka michache iliyopita walifikiria kubadilisha hali ya kuwa njia ya kupita kwa mizigo kuwa eneo lenye shughuli mbalimbali za kiuchumi. Kiongozi wa kamati ya usimamizi ya forodha ya mlima wa Ala Bw. You Zhanjun alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa, kutokana na uzoefu wa miaka michache iliyopita, wazo lao hilo limebadilika kuwa mambo halisi. Alisema,

"Tokea mwaka 2001, tulianza kuendeleza sekta ya usindikaji kwenye sehemu ya forodha, tulifanya uchambuzi kwa makini juu ya bidhaa zinazoagizwa kutoka nchi za nje na kufanya utafiti kuhusu mauzo yake, hivyo tulishawishi wafanyabiashara husika waje kufanya shughuli za usindikaji kwa mali-ghafi ambazo ni mwafaka kusindikwa kwenye sehemu ya mlima wa Ala. Kutokana na jitihada zetu, hivi sasa viwanda 12 vimehamia sehemu hiyo vikishughulikia usindikaji wa mbao, ngozi na manyoya pamoja na uyeyushaji wa madini."

Kampuni ya biashara ya Linyuan mkoaji Xinjiang inashughulikia usindikaji wa mbao, hapo zamani mbao zilizohitajiwa na kampuni hiyo zilitokana na magogo yaliyoagizwa kutoka nchi za nje, ambayo yalipita kwenye forodha ya mlima wa Ala, kisha yalipelekwa kupasuliwa katika kiwanda cha mbao kilichoko Ulumuchi, mji mkuu wa mkoa wa Xinjiang umbali wa kilomita zaidi ya 400 kutoka huko. Lakini hivi sasa kampuni hiyo imejenga kiwanda cha kupasua mbao kwenye sehemu ya mlima wa Ala. Mkurugenzi wa ofisi ya usimamizi ya kampuni hiyo Bw. Lu Yongjun alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa katika muda wa mwaka zaidi ya moja wamepata ufanisi mzuri wa uchumi.

"Kwani hapa kuna njia ya reli, magogo yanaletwa hapa, sisi tunapasua magogo hapa hapa, hali hiyo inatunufaisha, kwa hiyo tumefika hapa kujenga kiwanda cha mbao, ama sivyo gharama ya kusafirisha magogo hadi Ulumuchi ingeongezeka mara kadhaa. Katika kipindi cha kwanza tuliwekeza Yuan za Renminbi milioni 15, hivi sasa tuna wafanyakazi zaidi ya 380 ambao 70% ni wakazi wa hapa."

Bw. Lu Yongjun alisema kuwa thamani ya uzalishaji ya kampuni yao mwaka jana ilifikia Yuan milioni 80. Kampuni yao imenuia kuwekeza Yuan milioni 50 tena ili kufanya kiwanda chao kilichoko kwenye sehemu ya mlima wa Ala kuwa kituo cha usindikaji wa mbao cha kampuni yao.

Kutokana na mpango uliowekwa, hadi kufikia mwaka 2010 uwezo wa kupitisha mizigo wa forodha yao utafikia tani milioni 50, wakati huo thamani ya biashara ya nje na uzalishaji mali wa viwanda pia itaongezeka kwa mara kadhaa.

Forodha ya Huoerguosi iliyoko katika wilaya inayojiendesha ya wakazakh mkoani Xinjiang pia inapakana na nchi ya Kazakhstan, lakini tofauti yake ni kuwa forodha hiyo hivi sasa inachukua nafasi ya kwanza nchini kwa ukubwa wa barabara inayoenda nchi ya nje. Forodha hiyo inajulikana sana kutokana na shughuli za biashara na utalii wa sehemu ya mpakani. Mwaka jana idadi ya wafanyabiashara na watalii waliopita kwenye forodha hiyo ilizidi laki 5, mizigo iliyopita katika forodha hiyo ilizidi tani laki 4, jumla ya thamani ya biashara ya nje ilifikia dola za kimarekani milioni 570.

Ili kuimarisha maingiliano ya uchumi na biashara ya China na Kazakhstan na kuhimiza maendeleo na ustawi wa sehemu za mpakani za nchi hizo mbili, serikali za nchi mbili za China na Kazakhstan zilisaini mkataba mwezi wa Septemba mwaka 2004 na kujenga kituo cha ushirikiano wa sehemu ya mpakani cha kimataifa cha China na Kazakhstan chenye eneo la kilomita za mraba 14. Kiongozi wa wilaya inayojiendesha ya wakazakh Bw. Zhang Guoliang alipohojiwa na mwandishi wetu wa habari alisema kuwa, hivi sasa shughuli za maandalizi ya ujenzi wa kituo hicho zinaendelezwa vizuri. Alisema kuwa baada ya ujenzi wa kituo hicho cha ushirikiano kukamilika, kituo hicho kitakuwa na uwezo mkubwa wa kushughulikia mambo ya uwekezaji, biashara, usindikaji, usafirishaji na ununuzi wa bidhaa, utalii na mapumziko. Shughuli za kituo hicho zitainua kiwango cha ufunguaji mlango kwa nje kwa sehemu hiyo hata kwa mkoa mzima wa Xinjiang.

"Kutokana na kituo hicho tutaweza kuimarisha uhusiano kati ya China na nchi za Ulaya ya mashariki, Russia na nchi za Asia ya kati, kwa kuwa kituo hicho itakuwa na uwezo wa kama eneo la biashara huria, kitanufaika kutokana na sera za eneo la biashara huria, hivyo kitaweza kuvutia viwanda vingi zaidi kutoka sehemu ya ndani ya China, sehemu ya Hong Kong na Taiwan pamoja na viwanda vya nchi za nje, hivi sasa viwanda na kampuni nyingi za nchini na nchi za nje vimeeleza kuwa vinanuia kujiendeleza katika sehemu yetu."

Habari zinasema kuwa pamoja na uendelezaji wa ufunguaji mlango na maendeleo ya forodha za mkoa wa Xinjiang, kampuni na viwanda vingi vikubwa vya sehemu ya mashariki na vya nchi za nje vitatumia njia za forodha za Xinjiang kusafirisha bidhaa zao kwa nchi za Asia ya kati, Asia ya magharibi na Ulaya ambazo hivi sasa zinasafirisha bidhaa zao kwa uchukuzi wa baharini. Takwimu zinaonesha kuwa katika nusu ya kwanza ya mwaka huu, thamani ya bidhaa zilizopita katika forodha mbalimbali za Xinjiang ilizidi dola za kimarekani bilioni 3. Kuimarika kwa maeneo la ushirikiano wa uchumi ya forodha na sehemu ya mpakani kunafanya Xinjiang kuelekea kituo cha usindikaji wa bidhaa zinazosafirishwa kwa nchi za nje na mali-ghafi za nishati na madini zinazoagizwa kutoka nchi za nje. Hivi sasa mkoa wa Xinjiang umekuwa kituo muhimu cha biashara ya kimataifa kwenye sehemu ya kaskazini magharibi ya China.

Idhaa ya Kiswahili 2005-10-11