Kutokana na maendeleo ya uchumi wa vijijini nchini China, pato la wastani la wakulima wa China linaongezeka siku hadi siku, na wakati hali ya maisha ya wakazi wa vijijini inapoinuka, maisha yao ya kiutamaduni na burudani pia yamekuwa mazuri siku hadi siku. Sasa tunawaletea maelezo ya mwandishi wetu wa habari aliyeshuhudia jinsi wanakijiji wa kijiji cha Furaha wanavyofurahia maisha yao.
Kijiji cha Furaha kiko katika kitongoji cha mji wa Pingxiang cha mkoa wa Jiangxi, kusini mwa China. Mwandishi wetu wa habari alipokaribia kufika kwenye kijiji hicho, aliona nyumba maridadi za wakulima zilizojengwa chini ya mlima, huku akisikia midundo ya ngoma ya kikundi cha nyimbo na ngoma kilichoundwa na wanakijiji, ambacho kila siku kinafanya mazoezi kwenye uwanja wa kujengea mwili.
Mchezaji wa kikundi hicho mwenye umri wa miaka 58 Bi. Liu Wenzhi alisema kuwa, wanawake wengi wa kijiji hicho licha ya kupiga ngoma iliyofungwa kiunoni, pia wanapenda kucheza dansi ya Yangko, na dansi ya watu wawili wawili, michezo hiyo si kama tu inawasaidia kujenga mwili bali pia inawaburudisha. Shughuli za aina mbalimbali za kiutamaduni zimekuwa kivutio kikubwa cha kijiji cha Furaha. Bi. Liu Wenzhi akisema:
"Katika siku za kawaida, wakati wa asubuhi wanawake wa kijiji hicho hufanya usafi nyumbani au kwenda shambani, alasiri wakiwa na muda hukusanyika kwenye uwanja wa mazoezi ya kujengea mwili wakiimba nyimbo na kucheza dansi, au kufanya mazoezi ya kujengea mwili. Sisi sote tunapenda kutoa mchango katika kuendeleza burudani na shughuli za kiutamaduni za kijiji chetu."
Katika wakati wa mapumziko ya kilimo, wanakijiji wengi wa kijiji cha Furaha pia wanapenda kusoma vitabu kwenye chumba cha kusomea, kucheza chesi, kucheza mpira wa meza, kusikiliza muziki au kutazama filamu.
Shughuli hizo za kiutamaduni za kijiji cha Furaha zilianza kuendeshwa baada ya kijiji hicho kupata maendeleo miaka kadhaa iliyopita. Tangu mwishoni mwa miaka ya 70 ya karne iliyopita China ilipoanza kufanya mageuzi na kufungua mlango, kijiji cha Furaha kilitilia maanani kustawisha uchumi wake na kupata mafanikio makubwa. Viongozi wa kijiji hicho waliwaongoza wanakijiji kuendesha shughuli za aina mbalimbali za kiuchumi, kama vile kufuga mifugo kwa njia ya kisayansi, na kuendeleza kilimo cha kimaumbile. Pato la wakulima limeongezeka mwaka hadi mwaka, na kiwango cha maisha yao kinainuka siku hadi siku. Hivi sasa, kijiji hicho kina vituo vingi vya kilimo cha kimaumbile ambavyo ni pamoja na maua na miche ya miti, mpunga chotara na matunda yasiyotumia dawa au mbolea za kemikali, mazao ya kilimo kutoka kwenye kijiji hicho yanasafirishwa kwenye mikoa mingi nchini China.
Wakulima waliopata maendeleo wa kijiji cha Furaha wanajishirikisha katika shughuli za huduma za umma na kufuatilia hifadhi ya mazingira. Mwanakijiji Liu Huilan alisema :
"Ili kuhifadhi mazingira tunafukia takataka chini ya ardhi. Kwa mfano, sisi tunatumia makaa ya mawe, kila familia inachimba shimo la takataka uani la kuwekea mabaki ya makaa ya mawe au takataka za nyumbani. Takataka hizo zilizofukiwa ardhini si kama tu hazitachafua mazingira, bali pia zitakuwa mbolea nzuri kwa mboga na miti ya matunda."
Hivi sasa, asilimia 90 ya eneo la kijiji cha Furaha limepandwa miti na nyasi, na familia nyingi hata zimejenga vyoo vya kuhifadhi mazingira. Mazingira ya kijiji cha Furaha yamekuwa mazuri siku hadi siku. Wanakijiji pia wamechangisha fedha kujenga barabara ya saruji yenye upana wa mita 12 na urefu zaidi ya kilomita 7 inayounganisha familia zote 185 za kijiji hicho.
Mazingira mazuri na hali ya uchangamfu ya kijiji cha Furaha imewavutia watalii wengi. Na shughuli za utalii wa kimaumbile pia zimeleta faida kubwa kwa wanakijiji. Mkuu wa kijiji cha Furaha Bwana Liu Deshang alisema kuwa, kijiji cha Furaha kinazichagua familia zinazoishi kwa masikilizano na kuwa na usafi kama familia bora zenye ustaarabu ambazo zinaruhusiwa kuendesha mikahawa ya kifamilia na kuwapokea watalii, hatua hiyo imewahamasisha wanakijiji wote kutilia maanani hifadhi ya mazingira, na kufuata maadili, akisema:
"Familia zisizotimiza masharti yaliyowekwa haziruhusiwi kuendesha mikahawa ya kifamilia na kuwapokea watalii. Hivyo familia zote zinagombea kupewa sifa ya familia bora zenye ustaarabu ili ziweze kunufaika kutokana na kuwapokea watalii. Mwaka jana familia zaidi ya 30 zilipewa sifa hiyo, na kiasi hicho kimefikia 80 mwaka huu."
Idhaa ya Kiswahili 2005-10-13
|