Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-10-21 21:15:41    
China kutoa mafunzo ya sarakasi kwa vijana kutoka Afrika

cri

Wasikilizaji wapendwa, mliyosikiliza sasa hivi ni muziki ya maonesho maalumu ya sarakasi, yaliyofanyika tarehe 14 mwezi Septemba kwenye Jumba la Maonesho ya michezo ya sanaa la Tianqiao la Beijing. Maonesho hayo mazuri yaliyofanywa na wasanii kutoka Sudan, Ethiopia, Tanzania na Kenya, yaliwafurahisha watazamaji.

Sarakasi ni sanaa inayopendwa na nchi za Afrika. Katika miaka ya 70 na 80 ya karne iliyopita, China iliwahi kutoa mafunzo kwa vikundi kadhaa vya wachezaji wa sarakasi kutoka kwenye nchi za Afrika. Baada ya kurudi nyumbani kutoka China, wachezaji hao waliunda vikundi vya sarakasi na kufanya maonesho nchini mwao na katika nchi za nje, na kushiriki kwenye mashindano ya kimataifa ya sarakasi na kusifiwa sana. Baada ya kuanzishwa kwa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika, ushirikiano kati ya pande hizo mbili umeingia kwenye kipindi kipya. Kwa msingi wa baraza hilo, kutokana na matakwa ya nchi za Afrika, wizara ya utamaduni ya China imeanzisha tena mradi wa kutoa mafunzo ya sarakasi kwa vijana wa Afrika. Kuanzia mwaka 2002, wizara ya utamaduni ya China iliifanya shule ya sarakasi ya Wuqiao ya Hebei iwe kituo cha kutoa mafunzo kwa wanasarakasi kutoka nchi za Afrika. Hadi sasa shule hiyo imewaandaa wanafunzi 36 kutoka Tanzania, Kenya, Ghana na Ethiopia, na maonesho yaliyofanyika tarehe 14 hapa Beijing yalifanywa na kikundi cha tatu cha wanafunzi wa shule ya sarakasi ya Wuqiao.

Mabalozi wa nchi mbalimbali za Afrika nchini China walialikwa kutazama maonesho hayo, wakiwemo balozi wa Kenya Bi. Ruth Solitei na kaimu balozi mdogo wa Tanzania Bw. Augustine Ngonyani. Bi. Solitei alisema, Kenya inaishukuru sana China kwa juhudi zake za kutoa mafunzo kwa wasanii wa sarakasi wa Afrika, akisema:

Viongozi hao walifurahishwa na maonesho hayo mazuri. Kabla wachezaji hao kupanda jukwaani, wanaonekana ni watu wa kawaida, lakini wakati wanapokuwa jukwaani wote walikuwa wasanii hodari, wanaonesha vizuri kila sehemu ya mchezo, kwa mfano, sehemu moja inaoneshwa mtu mmoja akiwabeba watu watatu, lakini yeye mwenyewe alisimama kwenye ubao uliowekwa kwenye gurudumu. Kwa mtu wa kawaida ni vigumu sana kusimama kwenye ubao uliowekwa kwenye gurudumu, sembuse kuwabeba watu watatu. Muziki wa Afrika, na wachezaji wa Afrika wenye ukarimu mkubwa, vyote vimeipatia sarakasi ya jadi ya China sura mpya.

Wakati maonesho hayo yalikuwa yakiendelea, makofi makubwa kama hayo yalisikika mara kwa mara. Watu kutoka nchi mbalimbali waliwasiliana kwa macho na kutikisa vichwa mara kwa mara wakifurahia maonesho hayo, wakati huohuo sarakasi imekuwa lugha moja inayotumika kote duniani.

Baadhi ya wachezaji hao waliwahi kupata mafunzo ya sarakasi kwenye nchi zao, lakini mafunzo hayo hayakuwa kamilifu sana, baada ya kujifunza nchini China, kiwango chao cha sarakasi kimeinuka kwa udhahiri. Kitu cha kawaida kama vile bakuli, kofia, kiti, na meza kikifika mikononi mwao, kitabadilisha sura yake, hali hiyo inawafurahisha sana watazamaji, na pia imewafanya wafahamu zaidi sarakasi.

Kabla maonesho hayo hayajaanza, mwaandishi wetu wa habari alipata fursa ya kukutana na wasanii hao, mkubwa kabisa ana umri wa miaka 18, na mdogo kabisa ana umri wa miaka 12, ni kama mwanafunzi wa shule ya msingi. Walipozungumzia maisha hapa China, wote walifurahi na kukubali kuongea na mwandishi wetu wa habari.

Kati ya watoto hao wanaopendeza, kuna msichana mmoja mrembo mtanzania anayeweza kuongea vizuri kichina, anaitwa Joan Mwanga. Aliendesha maonesho hayo kwa kichina, wakati maonesho hayo yalipofika katikati, aliimba wimbo mmoja unaoitwa Mapenzi yangu kwako ni kama Mwezi, ambao uliwafurahisha sana watazamaji. Alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa, kichina chake kinatokana na kuishi kwake China kwa miaka mitatu, na wachezaji hao pia wanaweza kuongea kidogo Kichina, kwa kuwa wana vipindi vya kujifunza Kichina kila wiki. Alisema, wasanii hao watarudi nyumbani kwao muda mfupi baada ya maonesho, lakini yeye atabaki hapa China kuendelea na mafunzo.

Konsela wa wizara ya utamaduni ya China Bi. Zhang Jiping alifahamisha kuwa, katika miaka 25 iliyopita mbali na kuanzisha kituo cha kutoa mafunzo ya sanaa kwa watu wa nchi za Afrika, China imepeleka wataalamu katika nchi mbalimbali za Afrika kutoa mafunzo ya uchoraji, dansi na sarakasi, hatua hiyo imekaribishwa na nchi za Afrika. Kaimu Balozi mdogo wa Tanzania Bw. Augustine Ngonyani alisema:

Sarakasi ni sanaa ya jadi ya China, walimu wa sarakasi hawakubali kumfundisha mtu yeyote, lakini wachina wanatoa mafunzo ya sarakasi kwa watu wa Afrika, hali hiyo inathibitisha kwa mara nyingine kuwa, watu wa Afrika ni marafiki na ndugu wa wachina!

Idhaa ya Kiswahili 2005-10-21