Siku za karibuni nchi za Ulaya zimeongeza majadiliano na kuimarisha ushirikiano katika mapambano dhidi ya homa ya mafua ya ndege kutokana na kuwa ugonjwa huo umegunduliwa katika sehemu kadhaa za nchi za Ulaya. Maofisa wa nchi za Ulaya na vyombo vya habari vinawaambia watu wasiwe na wasiwasi kuhusu homa ya mafua ya ndege.
WHO na Kamati ya Umoja wa Ulaya zilifanya mkutano wa siku tatu kuanzia tarehe 24 huko Copenhagen, mji mkuu wa Danmark, wataalamu na wajumbe kutoka nchi 52 walishiriki kwenye mkutano huo, katika siku hiyo mkutano wa mawaziri wa kilimo wa Umoja wa Ulaya pia ulifanyika katika mji huo. Mikutano hiyo miwili ina lengo moja, nalo ni kujadili na kuandaa hatua za kukinga na kuzuia homa ya mafua ya ndege barani Ulaya.
Katika siku kadhaa mfululizo ugonjwa wa homa ya mafua ya ndege umekuwa unagunduliwa huko na huko barani Ulaya. Nchini Uingereza, kasuku aliyeingizwa kutoka Amerika ya kusini amegunduliwa kuwa na virusi vya H5N1 vya homa ya mafua ya ndege. Kwenye ukingo wa ziwa karibu na mji mkuu wa Sweden, Stockolm, bata pori aliyekufa amegunduliwa kuwa na virusi vya homa ya mafua ya ndege. Katika sehemu ya Nasice, mashariki mwa Croatia baada ya kumfanyia uchunguzi bata maji aliyekufa pia vimegunduliwa virusi vya H5N1. Kadhalika, katika sehemu ya Tambov kilomita 500 mashariki ya Moscow pia umegunduliwa ugonjwa huo, na katika sehemu ya Peniche katikati ya Ureno waligunduliwa bata maji na shakwe wakiwa wamekufa, lakini matokeo ya uchunguzi wa virusi bado hayajatolewa.
Baada ya kugundua kasuku mwenye virusi vya homa ya ndege Uingereza iliomba Kamati ya Umoja wa Ulaya ipige marufuku kuingiza ndegepori hai kutoka sehemu zote nje ya Ulaya. Tarehe 24 mkutano wa mawaziri wa kilimo wa Umoja wa Ulaya ulijadili ombi hilo la Uingereza. Baada ya mkutano huo mwanakamati wa Kamati ya Afya ya Umoja wa Ulaya Bw. Karkos Kyprianou alitangaza kuwa Kamati ya Umoja wa Ulaya itakubali ombi la Uingereza. Habari zinasema kuwa tokea tarehe 24 Ujerumani imetaka mifugo yote ifugwe katika hali ya karantini, na kuanzia siku hiyo Slovakia pia imepiga marufuku kuingiza mifugo hai au nyama ya mifugo kutoka nchi za nje.
Mkurugenzi wa ofisi ya WHO barani Ulaya Bw. Gudjon Magnusson tarehe 24 alipohutubia mkutano uliofanyika mjini Copenhagen alisema, pindi nchi za Ulaya zikishirikiana na kufanya juhudi, homa ya mafua ya ndege haitaweza kutulia barani Ulaya, na alisisitiza kuwa wakati ugonjwa huo unapoanza tu kutokea hapa na pale barani Ulaya, juhudi za kukinga na kudhibiti kabisa zisilegee.
Katika siku ambapo ugonjwa wa homa ya mafua ya ndege ulipotokea barani Ulaya, sekta ya mifugo ilipigwa pigo kali, biashara ya mifugo imepungua kwa asilimia 70, 30 na 20 katika nchi za Ugiriki, Italia, Ufaransa. Uchunguzi wa maoni ya raia unasema kuwa katika nchi za Hispania na Italia, wakazi zaidi ya asilimia 50 wanahofia ugonjwa huo utalipuka nchini mwao. Nchini Ufaransa asilimia 40 pia wamekuwa na wasiwasi huo. Katika siku za karibuni watu wa Ulaya wamezidi kushikwa na hofu kuhusu ugonjwa huo na kuwa mbioni kununua dawa za kinga. Magazeti ya Ulaya yanatangaza kuwa WHO inaposisitiza maandalizi ya kukinga homa ya mafua ya ndege pia inawaambia watu wasiwe na wasiwasi. Tarehe 14 Oktoba WHO ilitangaza kuwa hivi sasa ugonjwa wa homa ya mafua ya ndege unaibuka tu miongoni mwa ndege na haujatokea miongoni mwa wanadamu. Kwa hiyo WHO imetuliza tahadhari kwenye ngazi ya tatu kati ya ngazi sita kwa jumla.
Maofisa wa nchi mbalimbali za Ulaya pia waliwaambia watu wasiwe na wasiwasi, kwani ugonjwa huo unaenea tu miongoni mwa ndege na uwezekano wa kuwaambukiza wanadamu ni mdogo sana.
Idhaa ya kiswahili 2005-10-25
|