Tarehe 25 waziri wa mambo ya nje wa China Bwana Li Zhaoxing na waziri wa mambo ya nje wa Jamhuri ya Senegal Bwana Tidiane Gadio walisaini taarifa ya pamoja ya Jamhuri ya Watu wa China na Jamhuri ya Senegal kuhusu kurejesha uhusiano wa kibalozi kwa niaba ya serikali zao. Nchi hizo mbili zimerejesha rasmi uhusiano wa kibalozi kuanzia siku hiyo.
Taarifa hiyo imeainisha kuwa, serikali ya China inaunga mkono juhudi za serikali ya Jamhuri ya Senegal katika kulinda mamlaka ya nchi na kukuza uchumi. Nayo serikali ya Jamhuri ya Senegal imesema inatambua kuwa, kuna China moja tu duniani, serikali ya Jamhuri ya Watu wa China ni serikali pekee halali inayowakilisha wachina wote, na Taiwan ni sehemu moja isiyotengeka ya ardhi ya China.
Idara na watu wa fani mbalimbali za Senegal wamepongeza kurejeshwa kwa uhusiano wa kibalozi kati ya Jamhuri ya Senegal na Jamhuri ya Watu wa China. Wizara ya mambo ya nje ya Senegal tarehe 25 ilitoa taarifa ikisema kuwa, kurejeshwa kwa uhusiano wa kibalozi kati ya Senegal na China ni uamuzi wa kihistoria baada ya rais Abdoulaye Wade wa Senegal kufanya utafiti wa kina kuhusu hali ya kisiasa duniani. Uamuzi huo unalingana na maslahi ya kimsingi ya wananchi wa Senegal.
Taarifa hiyo imesema kuwa, huo ni uamuzi sahihi wa Senegal kuhusu hali ya sasa ya dunia, ambao utaboresha sura ya Senegal ya kimataifa. Pia taarifa hiyo imesisitiza kuwa, serikali ya Senegal itafanya juhudi zote kufanya ushirikiano wa kunufaishana na Jamhuri ya watu wa China.
Balozi wa kwanza wa zamani wa Senegal nchini China Bwana Ali Dioum alisema kuwa, kurejeshwa kwa uhusiano wa kibalozi kati ya Senegal na China ni uamuzi wa kihistoria na wenye busara uliotolewa na viongozi wa nchi hizo mbili. Nchi hizo mbili zina msimamo mmoja katika mambo mengi ya kimataifa. Katika mkondo wa hivi sasa wa utandawazi duniani, Senegal kamwe haiwezi kujitenga na China, bali inapaswa kuimarisha ushirikiano kati ya kusini na kusini kwa kuitegemea China, ili kuwanufaisha watu wa Senegal na watu wa nchi za Afrika.
Bwana Dioum aliyekuwa balozi wa Senegal nchini China kuanzia mwaka 1973 hadi 1981 aliainisha kuwa, katika miaka 25 tokea mwezi Desemba mwaka 1971 tangu nchi hizo mbili zianzishe uhusaino wa kibalozi hadi mwezi Januari mwaka 1996 wakati nchi hizo mbili ziliposimamisha uhusiano huo, China ilikuwa imetoa mchango mkubwa katika kuhimiza maendeleo ya uchumi, jamii na utamaduni ya Senegal, watu wa nchi hizo mbili pia wamejenga urafiki mkubwa wa jadi. Uamuzi wa serikali ya Senegal kurejesha uhusiano wa kibalozi na China umesahihisha kosa lake la kidiplomasia la kuiunga mkonoa Taiwan katika miaka kumi iliyopita, hivyo umekaribishwa na wananchi wa nchi hiyo.
Baadhi ya viongozi wa vyama vya kisiasa na watu mashuhuri wa kijamii wa Senegal katika siku za karibuni walitoa maoni yao kupitia vyombo vya habari, wakiisifu kwa kauli moja serikali ya Senegal kwa uamuzi wake wa kurejesha uhusiano wa kibalozi kati yake na Jamhuri ya Watu wa China, na kueleza matakwa ya kukuza ushirikiano wa kirafiki wa kunufaishana kati ya nchi hizo mbili.
Gazeti la Le Soleil la kiserikali la Senegal tarehe 26 lilichapisha makala iitwayo "Watu wa Senegal na Watu wa China warejesha uhusiano baada ya kutengana kwa miaka kumi", lilitumia kurasa tano kuchapisha habari na makala kuhusu kurejeshwa kwa uhusiano wa kibalozi kati ya Senegal na China, makala ambayo imepambanua kinaganaga mchakato wa kurejesha uhusiano wa kibalozi kati ya Senegal na China, kujulisha kutoka pande zote hali ya maendeleo ya China katika sekta za kisasa, kidiplomasia, kiuchumi, kiutamaduni, na kijamii. Gazeti hilo pia limechapisha makala ndefu ya mhariri iitwayo "kutazama historia, ilivyo sasa na siku zijazo". Makala hiyo imeainisha kuwa, "kurejesha uhusiano wa kibalozi kati yake na China ni hatua muhimu ya kidiplomasia iliyochukuliwa na serikali ya Senegal kutokana na kuzingatia maslahi ya muda mrefu ya kitaifa na kutafakari maendeleo ya siku zijazo duniani." Makala hiyo pia imesema kuwa, "Kwa upande wa kijiografia China inaonekana iko mbali nasi, lakini kwa upande wa kimkakati, China iko karibu nasi. Kuipuuza China kunamaanisha kukata njia ya kufanya mazungumzo na nchi yenye uwezo mkubwa."
Idhaa ya kiswahili 2005-10-28
|